KOCHA Roy Hodgson amesema anahitaji wachezaji wa England pamoja na mashabiki wa kandanda wamuunge mkono baada ya kukubali uteuzi kuwa meneja mpya wa timu ya taifa.
"Ninajiandaa kukabiliana na kibarua kilicho mbele yangu. Kila mtu anafahamu hii si kazi nyepesi lakini nina matumaini kila mmoja ataiunga mkono timu," alisema.
Meneja huyo mwenye umri wa miaka 64 ambaye hadi uteuzi wake alikuwa meneja wa West Brom, ndiye mtu pekee aliyeteuliwa na jopo la watu wanne waliomthibitisha baada ya kumsaili, kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Chama cha Kandanda cha England-FA, David Bernstein.
Bernstein alisema Hodgson aliteuliwa pekee kuwania nafasi hiyo mwezi mmoja uliopita.
Alikuwa ni meneja pekee aliyeombwa kwa ajii ya kibarua hicho licha ya dhana iliyokuwa imeenea akihusishwa meneja wa Tottenham Harry Redknapp kuziba nafasi iliyoachwa wazi baada ya Fabio Capello kujiuzulu mwezi wa Februari.
Hodgson, ambaye amesaini mkataba wa miaka minne, amekiri hana budi kuungwa mkono na wachezaji, wakiwemo waliotamka hadharani kumuunga mkono Redknapp.
Mshambuliaji Wayne Rooney aliandika kupitia mtandao wa kijamii wa Twitter baada ya Capello kuondoka: "Lazima Muingereza achukue nafasi yake. Mimi napendekeza Harry Redknapp." Mlinzi Rio Ferdinand naye kupitia mtandao huo wa kijamii aliandika: "Harry Redknapp ndiye atakuwa chaguo langu sana."
Lakini Hodgson, ambaye ameshawahi kufundisha timu 18 - zikiwemo timu tatu za taifa - katika kipindi chake cha miaka 36 ya ufundishaji kandanda, alisema yupo tayari kupata uungwaji mkono kutoka wachezaji.
Amesema Redknapp alimuachia ujumbe wa kumpongeza kwa njia ya simu.
0 comments:
Post a Comment