Mabingwa watetezi Hispania |
MICHUANO ya Kombe la Mataifa ya Ulaya, Euro 2012 inayoandaliwa
kwa pamoja na Poland na Ukraine itakuwa ni fainali za 14 za michuano hiyo
kufanyika.
Lilikuwa ni wazo la Henri Delaunay, Katibu wa Shirikisho la
Soka Ufaransa, ambaye aliibuka na wazo hilo kwa mara ya kwanza kwenye bara
hilo, mwaka 1927.
Kwa mara ya kwanza alipata sapoti kidogo sana na michuano
hiyo haikuanza hadi mwaka 1960. Hadi mwaka 1980 ni timu nne tu zilikuwa
zinacheza hatua ya fainali, lakini sasa ni timu 16 na imekuwa moja ya michuano
mikubwa katika kalenda ya soka.
Michuano yote 13 iliyotangulia imeacha kumbukumbu kibao – BIN
ZUBEIRY inakuletea wasifu wa michuano
hiyo hadi kufikia fainali za mwaka huu.
Mfungaji wa bao la ubingwa fainali zilizopita za Euro,Torres amerejeshwa kikosini dakika za mwishoni, je atang'ara tena? |
1960
MICHUANO ya kwanza ilifanyika Ufaransa na bingwa alikuwa Soviet
Union. Mabingwa hao waliongozwa na kipa wao gwiji, Lev Yashin langoni kwenye
michuano hiyo. Kipa aliyeipa England taji la Kombe la Dunia, Gordan Banks alifunikwa
na kipa huyo.
1964
Hispania kwa sasa wanatawala katika ulimwengu wa soka,
lakini mafanikio yao ya kwanza yalikuja katika Euro ya 1964, wakati walipotwaa
taji hilo kwenye ardhi ya nyumbani katika timu iliyoongozwa na Luis Suarez. Kiungo
huyo aling’ara kwenye michuano hiyo, ambayo Hispania ilifunika mbaya.
1968
Michuano ya tatu ya Ulaya ilifanyika Italia na kama ilivyokuwa
Hispania 1964, pia michuano hii ubingwa ulichukuliwa na wenyeji. England ilifika
Nusu Fainali na ilifungwa na Yugoslavia katika mechi ya kusisimua, iliyokuwa na
upinzani mkali. Alan Mullery wa England alionyeshwa kadi nyekundu kwenye mechi
hiyo.
1972
Waliokuwa mabingwa watetezi wa Ulaya, Italia walishindwa
kufuzu kuingia kwenye fainali hizo, wakiangushwa na Ubelgiji waliokuwa wenyeji,
katika Robo Fainali. Pamoja na hayo, Ujerumani waliweza, waliwafunga wenyeji
hao na kufuzu kutinga fainali za michuano hiyo, ambako waliifunga iliyokuwa USSR
mabao 3-0 na kutwaa Kombe.
1976
Michuano ‘iliyong’ara’ ya Euro 1976 taji lilichukuliwa na Czechoslovakia
walioifunga Ujerumani Magharibi kwenye fainali kwa mikwaju ya penalti mjini
Belgrade. Lakini pia ilikuwa michuano ambayo Wales ilikaribia kufuzu.
1980
Mfumo wa michuano ulibadilika mwaka 1980, kwa timu nane
kuingia kwenye fainali, lakini mwonekano wa matokeo haukubadilika, kwa
Ujerumani kutwaa ubingwa. Pamoja na hayo, kulikuwa kuna ‘maajabu’ kadhaa ikiwemo
Ubelgiji iliyokuwa na vipaji babu kubwa kufika fainali, mmojawao akiwa ni
Jean-Marie Pfaff.
1984
Ufaransa walikaribia kutwaa taji la Kombe la Dunia mwaka
1982, kabla ya kupokonywa tonge mdomoni na Ujerumani Magharibi katika Nusu
Fainali ya kukumbukwa, lakini hakukuwa na maajabu katika ardhi ya nyumbani, wakati
Wafaransa walipoongozwa na gwiji wake Michel Platini kutwaa taji hilo.
1988
Ilikuwa ni michuano ambayo mshambuliaji wa Uholanzi, Marco
van Basten alikuwa hana wa kumfananisha naye, kutokana na kufunga mabao ambayo
yaliiwezesha nchi yake kutwaa Kombe. Pamoja na hayo, ilikuwa habari tofauti kwa
USSR, iliyoongozwa na kocha wake gwiji, Valery Lobanovsky walipokaribia kutwaa
taji.
1992
Denmark haikufuzu kwenye fainali hizo nchini Sweden, lakini
walipata nafasi kutokana na Yugoslavia kuwa katika vita vya wenyewe kwa wenyewe,
hivyo kushindwa kushiriki. Na vijana hao wakafanikiwa kutwaa ubingwa wa
michuano hiyo, wakiifunga Ujerumani kwenye fainali. Kim Vilfort, ambaye
alifunga kwenye fainali alielezea namna ambavyo Denmark walikuwa na maandalizi
mazuri kabla ya fainali hizo.
1996
Euro 96 – michuano ambayo ilipewa jina soka imerejea nyumbani.
England ilifika Nusu Fainali, lakini ikafungwa na Ujerumani kwa mikwaju ya penalti.
Ujerumani ilifanikiwa kutwaa taji hilo kwa kuifunga Czechs Uwanja wa Wembley. Mshambuliaji
wa England, Alan Shearer alifanya vitu adimu sana kwenye fainali hizo.
2000
England ilifanikiwa kuifunga Ujerumani, lakini hawakufanikiwa
kufuzu kutoka kwenye kundi lao na vijana wa Kevin Keegan walirejeshwa nyumbani
kimaajabu. Ufaransa walitwaa Kombe la Dunia nyumbani kwao mwaka 1998 na wakadhihirisha
ubabe wao kwa kutwaa taji la Ulaya pia kwenye fainali zilizoandaliwa kwa pamoja
na Ubelgiji na Uholanzi. Kiungo Emmanuel Petit aliyeng’ara kwenye michuano hizo
alielezea siri ya mafanikio ya nchi yao.
2004
Euro 2004: Ugiriki walipoibuka mabingwa. Ilikuwa unakwenda
kuwa mwaka wa Ureno, katika fainali ambazo walikuwa wenyeji, lakini wakafungwa
na Ugiriki 1-0 kwenye fainali. Cristiano Ronaldo aliumizwa sana na matokeo
hayo, kwani ulikuwa mwaka wa kufurahia mafanikio na timu yake ya taifa, lakini
ikashindikana.
2008
Katika michuano iliyoandaliwa kwa pamoja na Uswisi na Austria,
ambayo ilifana, Hispania waliibuka mabingwa baada ya miaka 44 ya kusubiri taji
la kimataifa. Hispania waliifunga 1-0 Ujerumani katika fainali, bao pekee la
Fernando Torres dakika ya 33 na sasa wanaingia kwenye fainali za mwaka huu
kutetea taji, wakiwa pia mabingwa wa dunia. Je, wataweza? Bila shaka hilo ni
jambo la kusubiri na kuona.
0 comments:
Post a Comment