| |||
Gazeti la Mwanaspoti la leo limeandika kwamba Mafisango alifariki jijini Dar es Salaam kwa ajali ya gari Alhamisi iliyopita na kuzikwa nje kidogo ya jiji la Kinshasa, Congo, juzi Jumapili jioni.
Olly Elenga, ambaye ni mtoto wa dada yake Mafisango aliyeshuhudia ajali hiyo jijini Dar es Salaam na kuikimbiza maiti ya mchezaji huyo Hospitali ya Muhimbili jijini Dar es Salaam ameeleza kuwa marehemu alikuwa amelewa sana siku ya tukio.
"Kilichotokea ni kwamba baada ya Mafisango kurudi Sudan, Jumanne, siku iliyofuata alizima simu kabisa akasema hataki kwenda popote.
Akanipa dola 100 nipeleke kwa dada mmoja waliyekutana naye kwenye ndege jana yake kwa ajili ya kukodi gari ile iliyopata ajali, tukapewa na dereva anayeitwa Bozi.
Mafisango hakuwahi kumiliki gari jijini Dar es Salaam. Lakini asubuhi ya Jumatano iliyopita (Mei 16) alimpigia simu nyota wa Yanga, Haruna Niyonzima `Fabregas' na kumwita kwake ili wajadili kuhusu mambo ya timu ya taifa ya Rwanda. Fabregas alikuja nyumbani kuanzia asubuhi na wakanywa pombe na baadaye wakaongezeka akina Redondo (Ramadhani Chombo).
"Wakakubaliana waende Kinondoni kwa Queen Suzy yaani yule dansa wa bendi ya FM Academia `Wana Ngwasuma', ambaye ana baa yake karibu na Mango Garden, basi ndio wakanywa hapo na baadaye mke wa Redondo, aliyewaandalia chakula akawaita nyumbani kwao ili wakale, walipofika kule wakanywa bia sana, hapo Mafisango alikuwa hapatikani kwenye simu kwani zilikuwa zinatumika simu za Redondo na marafiki wengine aliokuwa nao.
"Tulikaa sana kwa mke wa Redondo mpaka saa tano usiku. Mafisango alishalewa sana, alikuwa hafai akajilaza kitandani hapo kwa mke wa Redondo akawa ananiambia tuwashe gari twende Keko kulala lakini mke wa Redondo akamwambia 'shemeji nina hamu ya kwenda Ngwasuma' waliokuwa kwenye Ukumbi wa Maisha Club, akatuambia twende wote. Mafisango akakubali akamwambia ataenda kumfurahisha kwa heshima yake.
"Tumefika kule ndani tukanywa sana pombe akatuza wanamuziki, tulivyoondoka akang'ang'ania kuendesha gari badala ya yule Bozi (dereva) aliyekuwa anaendesha tangu mchana, tulikuwa watano kwenye gari pamoja na yeye, kila mara Bozi alikuwa anazozana na Mafisango kwa kuwa alikuwa anamwambia mbona Mafisango mbona haendeshi vizuri gari halafu iko kasi na anayumbisha usukani hautulii, yaani ilifika sehemu mpaka tunataka kumshusha yule Bozi, lakini akasema hashuki mpaka ahakikishe tumefika Keko na kupaki gari la bosi wake.
"Tulipofika pale Keko, taa zilituzuia tukasimama, zilipowaka za kijani tukaondoka lakini spidi Mafisango aliyotoka nayo pale ilikuwa kali ghafla tukavuka geti la kwanza la Veta tukaona guta mbele yetu, kwa vile gari ilikuwa kasi ikabidi Mafisango airudishe kulia kwa nguvu kumkwepa yule jamaa halafu baada ya kumpita akairudisha kushoto ndio hapo ikaingia kwenye mtaro ikapanda
ikapinduka na nikachanganyikiwa nilipoona kichwa cha Mafisango kimenasa ndani kwenye sehemu ya gia halafu gari imekwisha na yule dada (rafiki wa mke wa Redondo) aliyekuwa amekaa naye mbele naye akawa kabanwa ikabidi nimtoe.
Pia nikamtoa na Mafisango akiwa anavuja damu na wakati huo alishafariki. Nikasimamisha taxi nikamkimbiza Muhimbili kufika pale wakanihakikisha kwamba amekufa sikuamini.
Lakini Mafisango aliumia sana na kama si pombe aliyokunywa asingekufa."
Katika mazishi yake, watoto wake wote watatu walihudhuria ambao ni David, Patrina na Crespo aliyekuwa anaishi naye Dar es Salaam.
Crespo aliteka umati wa watu katika mazishi hayo kwani kila mmoja alitaka kumsogelea na kumtazama.
0 comments:
Post a Comment