Dk Tamba |
WANACHAMA wa klabu ya Yanga, wakiwemo wazee kadhaa wa Dar es
Salaam wamemuomba, mwanachama mwenzao maarufu, Dk. Maneno Tamba kujitokeza
kuwania nafasi ya Uenyekiti wa klabu hiyo katika uchaguzi wa klabu hiyo,
uliopangwa kufanyika Julai 15, mwaka huu.
Habari ambazo BIN ZUBEIRY imezipata kutoka kwa mtu
wa karibu wa Dk. Tamba, zimesema kwamba wanachama wa klabu hiyo, walifika
mapema Jumatatu wiki hii ofisini kwa Dk. Tamba, Magomeni Mikumi, Dar es Salaam
na kumuomba agombee, wakimpa moyo ana sifa na uwezo.
“Walikuwa kama wanane hivi, kati yao watatu walikuwa wazee
kabisa, walifika hapa. Wakaomba kumuona Dk Tamba, msaidizi wa Dk Tamba akaenda kumuambia.
Dk akawaambia waingie, walipoingia sasa, nasikia yule msaidizi wake wakati
anawapelekea kahawa, ndio akasikia hayo mazungumzo,”kilisema chanzo hicho.
BIN ZUBEIRY iliwasiliana na Dk. Tamba juu ya habari hizo na
uamuzi wake, lakini akasema ni mapema mno kwa sasa kuzungumzia chochote juu ya
hilo, kwa sababu hakuwahi kufikiria suala hilo hata siku moja, hivyo inabidi
naye alifanyie kazi kwanza.
“Sheikh haya mambo mazito, wewe umepata habari hizi? Wewe
naye hatari sana,” alisema Dk. Tamba na kuanguka kicheko kabla ya kuendelea; “Wamekuja
wiki hii kweli, lakini inabidi nipate muda kwanza wa kulitafakari hili jambo na
kuwasiliana na wadau wangu kushauriana nao, klabu kubwa ile kaka,”alisema.
Kama kweli Dk Tamba ataamua kugombea Uenyekiti wa Yanga, anaweza
akapita kutokana na sifa zake.
Pamoja na kuucheza mpira wa miguu, kuwa na elimu nzuri, pia
Dk. Tamba ni mtu anayeheshimika mno na watu mbalimbali nchini, wakiwemo viongozi
wakubwa wa serikali, kutokana na shughuli za utabibu.
Ni mwadilifu na muumini safi wa dini ya Kiislamu, ambaye
anasali sala tano. Ana hekima, busara na anaijua soka kindakindaki- kwa sababu
ni mpenzi haswa wa mchezo huo. Dk Tamba anamiliki timu ya mpira wa miguu ya
wanawake ya Mburahati Queens, inayotoa wachezaji wengi timu ya taifa.
Sifa za ziada za Dk Tamba ni mbunifu, kwani pamoja na
shughuli zake za tiba za kijadi, ambazo humfanya aende kutoa huduma hadi nje ya
nchi, pia ni mfanyabiashara na ni miongoni mwa watu wa awali kabisa nchini
kutayarisha filamu ya Kitanzania na kuziingiza sokoni, ambazo zilifanya vizuri
mno, kama Nsyuka na Soka la Bongo.
0 comments:
Post a Comment