Nchunga akitangaza kujiuzulu leo jioni hii ofisini kwake |
Hata hivyo, Nchunga amekataa kulihusisha tukio la kuvamiwa kwake usiku wa jana na kujiuzulu kwake, akisema kwamba amefikia uamuzi huo kuinusuru Yanga, kwa sababu wapo watu wako tayari Yanga ife, lakini wamng'oe yeye madarakani, kitu ambacho yeye hapendi kitokee.
Nchunga alisema kwamba majira ya saa nane usiku wa jana, alivamiwa na kundi la watu takribani 15, lakini hawakufanikiwa kufanya chochote kutokana na ulinzi mkali uliopo katika nnyumba hiyo.
"Kwanza mbwa walianza kubweka, walinzi wakashituka wakaomba msaada kwa walinzi wenzao, nasi tukapuga simu polisi, wakaja haraka sana na kukuta watu hao wamekwishakimbia,"alisema
TAARIFA YA KUJIUZULU KWA NCHUNGA:
LLOYD
NCHUNGA BIHARAGU
C/O
LLOYD ADVOCATES,
Morogoro/Bibi TIti
Mohamed Rd,7th Floor, J.K. Nyerere Pension towers
P.BOX 75111, Dar-Es- Salaam,Tanzania.
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI KUHUSU KUJIUZULU NAFASI
YA UENYEKITI WA KLAB YA YANGA.
Ndugu wana
Habari, najua kwamba taarifa hii itawafedhehesha wajumbe na wanayanga
wanaotuunga mkono,hasa ukizingatia maamuzi ya pamoja ya vikao vyetu vya kamati
ya utendaji vilivyopita kwamba hakuna wa kujiuzulu kati yetu mpaka tujue hatma
ya mkutano mkuu ambao tulipanga ufanyike tarehe 15 Julai 2012, ukiachia mbali shinikizo
la kujiuzulu linalotolewa na baadhi ya wazee na wanaojiita vijana wa klab, kwa
wajumbe wa kamati ya utendaji, na hasa mimi kama mwenyekiti.
Nawashukuru
wajumbe kwamba tulifanya kazi kwa pamoja na kwa ushirikiano mzuri, na hata pale
tulipotofautiana tulifanya hivyo kwa hoja na kufikia maazimio ambayo wote
tulikuwa tunawajibika nayo.
Tangu tumeingia
madarakani tumeweza kushirikiana na kupata mataji matatu katika kipindi cha
mwaka mmoja, yaani; Ngao ya Hisani 2010, Ubingwa wa ligi kuu ya Vodacom 2010/2011,
na Ubingwa wa Afrika Mashariki na Kati
(Kagame Cup), 2011. Zaidi ni kwamba tuliuwa uteja kwa watani wetu wa jadi kila
tulipokutana katika ligi ukiachia mbali mechi ya tarehe 6 Mei 2012, ambayo
tulifungwa goli 5 bila, na kuleta mtafaruku mkubwa katika klab yetu.
Hali kadhalika
tumeshirikiana mpaka tumeweza kuboresha
mkataba kati yetu na TBL kupitia Kilimanjaro Premium Lager, tumeingia mkataba
na kampuni ya NEDCO kuendeleza mali zetu katika mtaa wa mafia na
uwanja wetu wa KAUNDA baada ya kufikia hatua nzuri katika kupata hati miliki za
maeneo yote mawili. Nafahamu kwamba kampuni hiyo iko katika hatua za mwisho za
kumalizia michoro.
Hali kadhalika
tuliingia mkataba wa kuzalisha na kuuza bidhaa zenye nembo yetu na hasa baada
ya kufanya marekebisho yatokanayo na matakwa ya sheria kule BRELA na pia
mkataba na kampuni ya NEXUS LTD, ambayo itakuwa inatutafutia wadhamini wa nje
na ndani, kufanya promosheni zetu na kampeni kwa njia ya electronic kupitia
mitandao mbalimbali na kukusanya data za wanachama na kusajili wapya tukiwa na malengo ya kukusanya shilingi
300,000,000/= hadi 800,000,000/= kwa mwaka katika kipindi cha miaka mitatu.
Haya yote tuliyafanya tukilenga kujitegemea kujazia mapengo yaliyokuwa
yakitokana na kutegemea ufadhili wa mtu mmoja mmoja.
Kwa ridhaa yenu
tumekua tukiendelea na mazungumzo na makampuni mbali mbali kwa ajili ya
udhamini na kwa sababu maalum, nitazitaja katika hati ya makabidhiano kwa
kiongozi ajaye.
Aidha,
tumeshirikiana katika kufanya mambo mbali mbali ya kijamii, ikiwa ni pamoja na
sikukuu ya kuadhimisha miaka 77 ya Yanga, sikukuu za pasaka, kuchangia jamii na
waliokumbwa na maafa, na kongamano la vijana lililolenga kuwaamsha vijana kuitambua
nafasi yao katika Yanga ikiwa ni pamoja na kupata azimio la kuanzisha SACCOSS
ya Yanga, ambapo maombi yapo kwa msajili Manispaa ya Ilala.
Haya yote
nayataja ikiwa ni kuwashukuru kwa ushirikiano na ikiwezekana muweze kuyakamilisha
yaliyobaki ambayo mtaona yalikuwa mazuri.
Lakini pia
tulipopata matatizo tulikuwa pamoja.
Nichelee kusema tu kwamba tulisimama pamoja baada ya kujiuzulu Makamu
Mwenyekiti wetu Ndugu Davis Mosha na mjumbe wetu ndugu Seif A. Seif, Ali Mayayi, na wengineo,
kwani tulifungwa na katiba.Tulisimama pamoja pia katika suala la kujiuzulu
ndugu Yusuf M. Manji, aliyekuwa mdhamini mteule na mfadhili mkuu ambaye sasa
ameonyesha nia ya kurudi nanyi mkaridhia mkutane naye. Awali, tulitumia kila
jitihada za kumrejesha lakini ikashindikana.
Hata hivyo doa
limetupata baada ya kufungwa na watani wetu goli 5 bila, ambapo kuna wanachama
wanaoelewa na wasioelewa kabisa.
Ninachokiona
mimi ni usaliti wa hali ya juu uliombatana na matukio mbalimbali yaliyopita na
yanayoendelea hadi kujaribu kupindua uongozi wa halali wa kidemokrasia.
SIWATUHUMU WACHEZAJI MOJA KWA MOJA, isipokuwa
mfululizo wa matukio wiki tatu kabla ya mchezo ule na sasa, inaonyesha
kwamba kulikuwa na usaliti mkubwa ambao sisi hatukuweza kuubaini mapema.
Sioni mantiki
katika hoja kwamba wachezaji walikuwa wakidai mishahara, posho n.k. Au ati mtendaji wetu alishikiliwa Arusha kwa
deni la hoteli, ndiyo tuvune bao 5!
Kwa wanaoijua
Yanga, imewahi kuwa na madeni makubwa katika Hoteli mbali mbali, mawakala wa
ndege n.k, na baadhi tumeyakuta na sisi tumekuja tukayalipa. Hii imewahi
kutokea kabla na wakati akiwepo mfadhili, sembuse sisi tulioachwa baki, na bado
wachezaji walicheza kwa morali.
Hata hivyo,
utamaduni wa kutimuana baada ya matokeo mabaya ni dhambi ambayo itatula kama
hatutaiacha, kwani wenye hila na uchu wa madaraka wataendelea kutumia mbinu hiyo
ili kuuondoa uongozi wa kidemokrasia.
Baada ya
mapinduzi kushindikana na TFF kuonya kuhusu mapinduzi hayo, wazee kupitia
msemaji wao , Mzee Akilimali wamesikika katika kipindi cha Michezo cha Redio moja maarufu hapa nchini wakidai
kwamba ni bora Yanga ishushwe daraja au kufungiwa kuliko mimi kuendelea
kuongoza!
Hii
imenikumbusha HEKMA ZA MFALME SELEMANI akiamulia ugomvi wa wanawake wawili
waliokuwa wakigombea mtoto naye akaamuru wamgawane nusu kwa nusu. Yule mwenye
mtoto kweli alimuomba Mfalme amuachie mwenzie kuliko kumkata nusu.
Kwa hekma hiyo
nimeamua kujiuzulu nafasi yangu katika Uenyekiti wa Yanga kwani ni klab ninayoipenda hata kama
sio kiongozi kwa mujibu wa ibara ya 28 ya katiba yetu.
Vile vile siko
tayari kuona klab yangu ikisalitiwa au kuhujumiwa eti kwa sababu tu mimi ni
kiongozi.
Natumaini kamati
ya utendaji kwa pamoja na wale tuliowateua chini ya ibara ya 29(3) ya katiba ya
Yanga pamoja na bodi ya wadhamini, itawaongoza wanachama mpaka kufikia mkutano
mkuu kwa mafanikio zaidi.
Nitaendelea kuwa mwanachama mwadilifu na
nitatoa mchango wangu wa hali na mali pale nitakapo hitajika na nikiwa na uwezo wa kufanya hivyo.
YANGA DAIMA
MBELE, NYUMA MWIKO.
Wasalaam,
LLOYD NCHUNGA BIHARAGU.
Nakala kwa:-
Mama Fatma
Karume,Mdhamini
Francis Kifukwe,
Mdhamini
Bwana Yusuf
Manji – Kwa taarifa
0 comments:
Post a Comment