BINGWA wa zamani wa dunia wa ngumi za kulipwa uzito wa Super
Fly, aliyekuwa akitambuliwa na WBU, Magoma Shaaban Ngereza amefariki dunia usiku huu
katika hospitali ya Bombo, mkoani Tanga, imeelezwa.
Bondia maarufu wa zamani nchini, Ally Bakari ‘Championi’
ameiambia BIN ZUBEIRY usiku huu kwamba, Magoma aliyezaliwa Oktoba 21, mwaka 1980 mjini Tanga, amefariki majira ya saa 12
jioni.
Championi alisema kwamba Magoma alikuwa anaumwa kwa muda
mrefu na siku nne zilizopita alizidiwa na kukimbizwa katika hospitali hiyo,
kabla ya umauti kumfika leo.
Hadi anafariki dunia, Magoma (pichani kushoto) alikuwa amepigana jumla ya mapambano
16, akishinda 13, manane kati ya hayo kwa Knockout (KO), amepigwa matatu na
yote kwa KO na hakuwahi kutoka sare.
Magoma alipanda ulingoni kwa mara ya mwisho Julai 21, mwaka 2006
na Eugen Sorin Tanasie mjini Timisoara, Romania katika pambano ambalo alipigwa
kwa Technical Knocout (TKO) raundi ya pili.
Taji lake la kwanza kutwaa lilikuwa ni la IBF Afrika,
Septemba 12, mwaka 1998 akimpiga Mkenya Joseph Waweru kwa KO raundi ya kwanza,
Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.
Mei 11, mwaka 2000
alimpiga bondia ‘matata sana’ Totin Lukunim wa Thailand na kutwaa taji la IBF
Intercontinental, uzito wa Super Fly kwenye ukumbi wa PTA, Temeke, Dar es
Salaam.
Agosti 3, mwaka 2001 ndipo alitwaa ubingwa wa dunia wa WBU
baada ya kumpiga Ferid Ben Jeddou wa Tunisia kwa TKO raundi ya sita mjini Avezzano,
Abruzzo, Italia, kabla ya kupoteza taji hilo kwa kupigwa na Gabula Vabaza Julai
26, mwaka 2002 katika ukumbi wa Hemingways Casino, East London, Eastern Cape, Afrika
Kusini kwa KO raundi ya kwanza.
Mei 25, mwaka 2003 alipigwa na Mtanzania mwenzake, Mbwana
Matumla kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee, Dar es Salaam kwa TKO raundi ya nne.
Alijiunga rasmi na ngumi za kulipwa mwaka 1996, pambano lake
la kwanza akicheza Juni 3, mwaka huo na kumpiga Athumani Omari kwa pointi, Uwanja
wa Mkwakwani, Tanga.
Mungi aiweke pema peponi roho ya marehemu. Amin.
0 comments:
Post a Comment