![]() |
Na Mahmoud Zubeiry |
KATIKA mada yangu iliyopita nilisema, mustakabali wa klabu
ya Yanga utazamwe upya kufuatia, Mwenyekiti wake, Wakili Lloyd Baharagu Nchunga
kujiuzulu, baada ya vita kubwa aliyokuwa akipigwa na wapinzani wake.
Bado naendelea kusistiza; Nchunga anastahili sifa,
ameonyesha yeye ni Yanga damu. Si mroho wa madaraka. Ni mtu aliyeweka maslahi
ya Yanga mbele. Huyu ni mfano wa kuigwa. Lakini baada ya Nchunga kujiuzulu,
pamoja na kwamba mfanyabiashara Yussuf Manji ameahidi kuihudumia timu kwa mwaka
mmoja, bado ipo haja sasa ya mustakabali wa klabu hiyo kutazamwa upya.
Nilisema mustakabali wa klabu kutazamwa upya, kwa sababu
imeonekana ni vigumu mno Katiba kumlinda kiongozi aliye madarakani, iwapo kundi
fulani litaamua kwa dhati kuingia msituni kumng’oa.
Nilitoa mfano vita aliyopigwa Nchunga- ilikuwa kali na ikafikia
lazima aondoke kwa maslahi ya klabu. Alitengenezewa zengwe zito. Alipigwa kila
upande- hakuwa na namna yoyote zaidi ya kujinasua.
Walioongoza mapambano dhidi ya Nchunga, akina Ibrahim Akilimali,
Bakili Makele na wengine- ni wale wale ambao kwa zaidi ya miaka 10 wamekuwa
mstari wa mbele katika vurugu na migogoro kwenye klabu hiyo.
Kumbukumbu zipo, Bakili na Akilimali walishiriki kikamilifu
kumng’oa Mzee Rashid Ngozoma Matunda mwaka 1999 na hawa hawa walimtia
kashikashi nzito Wakili Imani Omar Madega, ingawa huyo walimshindwa.
Sioni kwa sababu gani hawa watakoma kwa mtu mwingine yeyote
atakayekuja baada ya Nchunga, kwa sababu wamekwishazoea. Baba wa Taifa, Mwalimu
Julius Kambarage Nyerere, aliwahi kutoa mfano mmoja enzi za uhai wake kuhusu
ubaguzi.
Alisema dhambi ya ubaguzi ni sawa na dhambi ya kula nyama ya
mtu, ukishakula nyuma ya mtu, hutaacha utaendelea kula.
Naweza kuuleta mfano huu katika hii desturi ya mapinduzi
kwenye klabu ya Yanga- naona kuna dalili za kutosha itaendelea tu hata ije katiba
ya aina gani.
Tena watu hawa wamepiga hatua kubwa, kiasi cha kuona bora
Yanga ife, lakini kiongozi fulani ang’oke madarakani. Inasikitisha.
Mapendekezo ya Manji kuhusu mabadiliko ya Katiba hata
yafanyiwe kazi- lakini kuna uwezekano likaibuka kundi la kumpinga na kupambana naye
kikamilifu. Hiyo ndio tabia ya Yanga.
Kwa ‘uhuni’ aliofanyiwa Nchunga, hakuna hakika kama atatokea
mtu mwingine mwenye hekima na kujiheshimu kufikiria kuongoza Yanga- inatia
woga. Lakini kwa nini ifikie huko, kweli tutegemee kuiona Yanga bora na ya kisasa
bila mtu mwenye hekima na upeo mkubwa?
Ndipo hapo unapoonekana umuhimu wa mustakabali wa Yanga
kutazamwa upya- kwa sababu wapo watu, kila sekunde ya maisha yao inaitegemea klabu
hiyo. Watu hao ukiwatazama sura zao, wako tayari hata kuua mtu, anayekuja na
sera za kutaka kuwatoa Yanga.
Jamal Malinzi alikiona cha moto, tu kwa kutaka fedha za
klabu zinapoingia ziende moja kwa moja benki- makomandoo walianza kumpiga vita
tangu hapo hadi akang’oka.
Hii haitaisha na wala asijidanganye mtu eti atakuja kukaa
Yanga kwa raha, hata siku moja! Manji mwenyewe ameshatukanwa sana na wavaa ndala-
yaani upo umuhimu wa mustakabali wa klabu hiyo kutazamwa upya.
TFF imeagiza uchaguzi ufanyike Julai kujaza nafasi za
wajumbe waliojiuzulu, akiwemo Mwenyekiti- vema, lakini kutokea hapo nini
mustakabali wa klabu? Hilo ndilo suala ambalo kila mwana Yanga anapaswa kujiuliza
kwa sasa.
Naposema wana Yanga, siwahusishi wale ambao wanategemea
klabu ili kulisha familia zao, na kwa ujumla kuendesha maisha yao. Hao si wana
Yanga, kwa sababu mwana Yanga mzuri ni yule ambaye anafikiria ataifanyia nini
klabu, si klabu imfanyie nini yeye.
Manji ana mapendekezo yake ya Katiba, ambayo anataka
yafanyiwe kazi na uongozi utakaoingia madarakani Julai- sidhani kama matakwa ya
Manji yatatekelezwa na kiongozi yeyote.
Hatari ambayo kiongozi yeyote wa Yanga anatakiwa kuiepuka ni
kupitisha Katiba ambayo mwisho wa siku, itaiondoa timu kuwa mali ya wanananchi
na kuwa mali ya mtu mmoja- kwa namna yoyote ile, kwani kufanya hivyo itakuwa
sawa na kuiuza klabu.
Lakini upo umuhimu sasa wa Yanga kuendana na mifumo ya
kisasa ya uendeshaji wa klabu hiyo- kwa kutangaza tenda za kuiendesha klabu na
watu kuingia mikataba na uongozi wa klabu, kuimiliki timu kwa muda fulani.
Kwa sasa Yanga inapata nini kwa mwaka? Sijui zaidi ya kelele
za madeni lukuki. Uongozi utakaoingia madarakani, utangaze tenda ya kuikabidhi
klabu kwa kampuni au mtu, kwa dau mathalani la Sh. Milioni 500 kwa miaka
mitatu.
Nitafafanua. Kwa mfano Rostam Aziz anaamua kuilipa Yanga
Milioni 500, anapewa mkataba wa kuimiliki klabu kwa muda wa miaka mitatu. Atasajili
timu, atalipa mishahara, ataingia mikataba ya udhamini ya miaka mitatu, lakini
Yanga itabaki kuwa vile vile na asili yake.
Mkataba utampa masharti muwekezaji, ambayo asipoyatimiza
atatakiwa kuiachia timu, apewe mtu mwingine- mfano kuhakikisha waajiriwa wote
wanalipwa kwa wakati, matokeo mazuri na kutokiuka miiko na asili ya klabu.
Wapo watu wana uwezo wa kujitokeza kuchukua dili hiyo- na
Yanga itanufaika mno. Kwa sasa Yanga haiingizi chochote- lakini vipi ikiwa
haiingii gharama yoyote na kila baada ya miaka mitatu, akaunti yake inapotokea
Milioni 500?
Fedha hizo zinaweza kutumika kwa miradi mingine ya maendeleo
ya klabu, kama ujenzi wa Uwanja na kadhalika, wakati mtu aliyeingia mkataba wa
kumiliki klabu, naye anatengeneza fedha nzuri kutokana na mikataba ya udhamini,
mauzo ya bidhaa zenye nembo ya klabu, mapato ya milangoni, mauzo ya wachezaji
na kadhalika, ikiwemo zawadi za mashindano.
Hayo ni mawazo yangu, lakini najua wapo wengine wana mawazo
mazuri katika kuijenga Yanga isiyo na migogoro na yenye manufaa, itakayokuwa
inawapa faraja mashabiki wake. Hoja ni kuutazama upya mustakabali wa klabu. Nawasilisha.
0 comments:
Post a Comment