Bosi Fiorentina Delio Rossi atimuliwa baada ya kumpiga mchezaji wake.

KOCHA wa Fiorentina, Delio Rossi ametimuliwa baada ya kumpiga mchezaji wake katika mabishano ya kufanya mabadiliko.
Mchezaji wa zamani wa majaribio Manchester United, Adem Ljajic alipingana na uamuzi wa kocha wake kumtoa jana katika mechi ya Serie A dhidi ya Novara.
Rossi alikasirika na kuamua kumtoa nje na kumsukumia ngumi mshambuliaji huyo wa Kiserbia.
Rais wa Fiorentina, Andrea Della Valle alimfukuza kazi Rossi mara moja baada ya mechi hiyo, ingawa hadi sasa mrithi wake hajatangazwa.
Delio Rossi
Rossi akimtandika konde Ljajic.
"Nilipaswa kuchukua uamuzi huu. Hakuna namna ya kulielezea tukio lile," alisema Della Vale.
"Samahani kwa kocha ambaye ni mtu mzuri na ambaye hakustahili hii, lakini usiku huu amekumbana na hatua kali."
Tukio hilo lilitokea muda mfupi tu baada ya nusu saa ya mchezo, Fiorentina ikiwa imelala 2-0 dhidi ya wageni, ambao wanashika nafasi ya pili kutoka mkianiSerie A.
Linahitimisha miezi sita ya Rossi kupiga kazi klabu hiyo ya Tuscan.
Alichukua nafasi ya Sinisa Mihajlovic aliyetupiwa virago Novemba, lakini na amepigana kuiimarisha Viola msimu huu.
Fiorentina inashika nafasi ya 15 zikiwa zimebaki mechi mbili.
Manchester United ilikuwa ina makubaliano ya kumsajili Ljajic, ambaye sasa ana umri wa miaka 20, kutoka Partizan Belgrade, lakini ilighairi mwaka 2009 ikihofia itapata tabu kumpatia kibali cha kufanya kazi.
Rossi anakuwa kocha wa 19 kufukuzwa timu za Ligi Kuu Italia msimu huu, na hivyo kuvunja rekodi ya kufukuzwa makocha 15 msimu wa 1951-52.