Kikosi hatari cha Simba kilichoipiga Yanga 6-0, wa tatu kutoka kulia waliosimama ni King Kibadeni aliyepiga hat trick, rekodi ambayo haijavunjwa hadi leo kwenye mechi za watani |
MGOGORO wa mwaka 1976 ulioibuka na kuigawa
Yanga hadi kuzaliwa Pan African, ulisababisha athari nyingine kadhaa za
kihistoria kwenye klabu hiyo, zaidi ya mgawanyiko huo.
Baada ya mgogoro wa Yanga Kandambili na Yanga
Raizoni, rasilimali nyingi za klabu hiyo, yakiwemo mabasi ziliteketea. Lakini
pengine hilo inawezekana lisiwaumize sana wana Yanga, kuliko kipigo kutoka kwa
watani wao wa jadi, Simba, cha mabao 6-0.
Baada ya mgogoro huo, kwa sababu wachezaji
wote walimfuata mzee Tarbu Mangara aliyekuwa Mwenyekiti wa klabu hiyo, Yanga
walilazimika kuunda upya timu yao, wakisajili wachezaji wapya. Tangu mwaka
1977, Yanga walikuwa vibonde wa Simba hadi mwaka 1981, walipojikomboa.
Tangu kuanzishwa kwa Ligi ya Tanzania, mwaka
1965 hadi mwaka 1976 Yanga inakutwa na mgogoro huo, ilikuwa imekutana na watani
wao wa jadi, Simba kwenye mechi 10. Katika mechi hizo, Yanga walishinda saba,
Simba waliibuka kidedea mara mbili na mara moja ilikuwa ni sare.
Kati ya mara saba ambazo Yanga iliifunga
Simba, ndani yake kuna kipigo cha mabao 5-0, Juni Mosi mwaka 1968, enzi hizo
Simba bado ikiitwa Sunderland.
Siku hiyo, mabao ya Yanga yalitiwa kimiani na
Maulid Dilunga dakika za 18 kwa penalti na 43, wakati mengine yalifungwa na
Salehe Zimbwe dakika za 54 na 89 na kuhitimisha karamu ya mabao, lilifungwa na
Kitwana Manara 'Popat' dakika ya 86.
Kwa homa ya kipigo hicho, kwenye mchezo
uliofuata Machi 3, mwaka 1969, Simba waliishia njiani maeneo ya Chang'ombe na
kurejea klabuni kwao, wakihofia kutandikwa zaidi, hivyo watani wao wa jadi,
kupewa pointi za chee.
Baada ya hapo, timu hazikukutana hadi Juni 4,
mwaka 1972, Simba wakiwa madhubuti tayari kuweza kuhimili vishindo vya Yanga.
Katika mchezo huo, timu hizo zilitoka sare ya 1-1, tena Sunderland ikitangulia
kupata bao kupitia mshambuliaji wake, Willy Mwaijibe, dakika ya 11, kabla ya
Kitwana Manara kusawazisha dakika nane baadaye.
Juni 18, mwaka huo huo 1972, timu hizo
zilikutana tena na bao pekee la Leonard Chitete (sasa marehemu) lilitosha
kuendeleza ubabe wa Yanga kwa Simba.
Haidari Abeid 'Muchacho' alikomesha tabia ya
Simba kufungwafungwa na Yanga, katika mechi baina ya watani hao wa jadi, Juni
23, mwaka 1973, akifunga bao pekee lililowalaza mapema wana Jangwani, dakika ya
68.
Wakati Simba ikiamini imekwishapata dawa ya
Yanga, Agosti 10, mwaka 1974 katika mchezo uliowakutanisha watani hao wa jadi
nje ya Dar es Salaam, kwa mara ya kwanza, Uwanja wa Nyamagana mjini Mwanza,
Wekundu wa Msimbazi walikiona cha moto.
Wekundu wa Msimbazi walianza vizuri kwa
kuwatungua Yanga bao la mapema dakika ya 16 tu ya mchezo, mfungaji akiwa ni
Adamu Sabu. Lakini zikiwa zimesalia dakika tatu mchezo kumalizika, mjini Dar es
Salaam, mashabiki wa Simba wakiwa wamekwishajikusanya kuanza misafara ya
kuelekea makao makuu ya klabu hiyo, Mtaa wa Msimbazi kushangilia ushindi,
walikuwa wanyonge ghafla baada ya mtangazaji wa Radio Tanzania (RTD), Ahmad
Jongo kutangaza bao la kusawazisha la Gibson Sembuli (sasa marehemu).
Kwa bao hilo, mchezo huo kwa sababu ulikuwa wa
kuamua bingwa, ilibidi uhamie kwenye dakika 30 za nyongeza. Dakika ya saba
Sunday Manara aliwainua vitini mashabiki wa Yanga waliokuwa Nyamagana kwa
kufunga bao la pili. Naam, huo ulikuwa ushindi wa mwisho wa Yanga kwa Simba,
kwani baada ya hapo, mgogoro wa Yanga Kandambili na Yanga Raizoni uliitafuna
klabu hiyo.
Hatimaye ikawadia siku chungu zaidi katika
maisha ya Yanga kwenye utani wao na Simba, ilikuwa ni Julai 19, mwaka 1977
kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, enzi hizo Simba ikinolewa na Mbulgaria,
Dimitar Samsarov.
Simba ikiwa na 'mziki' wake ule ule uliokuwa
ukichuana na Yanga tangu mwaka 1974, ilikutana na Yanga mpya kabisa iliyoundwa
na wachezaji kama kipa aliyekuwa Mwadui ya Shinyanga, Bernard Madale.
Yanga walishindwa kuimudu kasi ya Simba na
kujikuta wakitandikwa mabao 6-0, mabao ya Wekundu wa Msimbazi yakitiwa kimiani
na Abdallah Kibadeni katika dakika za 10, 42 na 89, Jumanne Hassan 'Masimenti'
dakika za 60 na 73, wakati Selemani Sanga alijifunga mwenyewe dakika ya 20.
Kipigo hicho kilikuwa sababu tosha ya kipa Madale kutupiwa virago Jangwani.
Lakini Yanga iliendelea kuchezea vipigo tu
walipokutana na Simba, japokuwa Oktoba 7, mwaka 1979 walipunguziwa dozi kwa
kiwango cha nusu nzima, kutoka bao sita hadi tatu.
Yanga ilichapwa 3-1 siku hiyo, mabao ya Simba
yakifungwa na Nico Njohole dakika ya tatu, Mohammed Bakari 'Tall' dakika ya 38
na Abbas Dilunga dakika ya 72, wakati lile la kufutia machozi la Yanga
lilifungwa na Rashidi Hanzuruni dakika ya nne.
Oktoba 4, mwaka 1980, Yanga ilipigwa tena
'nusu dozi' ya 6-0, mabao ya wana Msimbazi yakitiwa kimiani na Abdallah
Mwinyimkuu dakika ya 29, Thuwein Ally dakika ya 82 na Nico Njohole dakika ya
83.
Hatimaye saa ya ukombozi iliwadia Jangwani,
Juma Hassan Mkambi akiitwa 'Jenerali' enzi zake alikomesha uteja wa Yanga kwa
Simba, Septemba 5, mwaka 1981, kwa bao lake pekee dakika ya 42. Siku hiyo,
mabeki wa Yanga walifanya kazi kubwa ya kulinda bao hadi dakika 90 zilipotimia,
wana Jangwani wanainua mwali wao.
Naam, Mkambi alifuta uteja wa Yanga kwa Simba
na kuanzisha rasmi enzi za Jangwani kuwanyima raha wana Msimbazi, kwani katika
mechi iliyofuata, Aprili 29, mwaka 1982, bao la Rashid Hanzuruni dakika ya pili
tu ya mchezo liliifanya Simba ilale tena 1-0.
Hiyo ilikuwa mechi ya kwanza kuwakutanisha
watani wa jadi, tangu kuanza kwa Ligi ya Bara kutoka Klabu Bingwa ya Taifa na
katika mchezo wa marudiano, Simba walikiona tena cha moto, walitandikwa 3-0, Septemba
18, mwaka huo, 1982.
Mabao ya Yanga siku hiyo yalitiwa kimiani na
Omar Hussein 'Keegan'
katika dakika ya pili na ya 85, wakati lingine
lilifungwa na Makumbi Juma 'Homa ya Jiji' au 'Bonga Bonga' dakika ya 62.
Tangu hapo, Yanga iliitesa Simba kwa miaka
sita mfululizo, hadi ilipokuja kujikomboa Agosti 23, mwaka 1986 kwa ushindi wa
mabao 2-1, wafungaji wakiwa ni marehemu Edward Chumila, dakika ya tisa na
Malota Soma dakika ya 51. Siku hiyo Omar Hussein alitangulia kuifungia Yanga
bao dakika ya 5.
Februari 10, mwaka 1983, timu hizo zilitoka
sare ya bila kufungana na kwenye mchezo wa marudiano, Aprili 16, mwaka huo,
Yanga ilishinda 3-1, mabao yake yakitiwa kimiani na Charles Boniface Mkwasa
dakika ya 21, Makumbi Juma dakika ya 38 na Omar Hussein dakika ya 84, wakati la
kufutia machozi la Simba lilifungwa na marehemu 'Super' Kihwelo Mussa dakika ya
14.
Septemba 10, mwaka 1983, Yanga iliichapa Simba
2-0, wafungaji wakiwa ni Lila Shomari aliyejifunga dakika ya 72, kabla ya Ahmad
Amasha kufunga la pili dakika ya 89, wakati kwenye mechi ya marudiano, Septemba
25, mwaka huo, timu hizo zilitoka sare ya 1-1. Sunday Juma 'Pikipiki'
alitangulia kuifungia Simba bao dakika ya 72, kabla ya Makumbi Juma kusawazisha
dakika tatu baadaye, dakika ya 75.
Machi 10, mwaka 1984, timu hizo zilitoka 1-1
tena, kipa Iddi Pazi 'Father' akitangulia kuifungia Simba bao kwa mkwaju wa
penalti dakika ya 20, kabla ya Omar Hussein kusawazisha dakika ya 72.
Julai 14, mwaka 1984, mdudu wa sare aliendelea
kutawala kwa watani wa jadi, kwani zilitoka 1-1 tena, Zamoyoni Mogella 'Golden
Boy' akitangulia kuifungia Simba dakika ya 17, kabla ya Abeid Mziba 'Tekero'
kusawazisha dakika ya 39.
Mei 19, mwaka 1985 mchezo ulimalizika kwa sare
ya 1-1 tena, Omar Hussein akianza kuifungia Yanga dakika ya sita kabla ya
Mohammed Bob Chopa kuisawazishia Simba dakika ya 30.
Yanga ilirejesha enzi za ubabe Agosti 10,
mwaka 1985, ilipopewa pointi za chee, baada ya Simba kutoroka uwanjani ikigomea
adhabu ya penalti, wakati Machi 15, mwaka 1986 zilitoka sare ya 1-1 tena, John
Hassan Douglas akitangulia kuifungia Simba dakika ya 20, kabla ya Abeid Mziba
kusawazisha dakika ya 44.
Katika mchezo wa marudiano, Agosti 23, 1986
ndiyo Chumila na Malota walizima ubabe wa Yanga kwa Simba rasmi.
Baada ya hapo, timu hizo zilikuwa zikifungana
kwa zamu, ingawa kipigo kikali zaidi kilikwenda kwa Yanga, Julai 2, mwaka 1994,
wakati Simba waliposhinda 4-1.
Hata hivyo, baada ya mchezo huo, Yanga
ilivunja tena kikosi kutokana na tuhuma za kuhujumiwa na wachezaji wake, safari
hiyo ikidaiwa aliyekuwa mfadhili mmoja wa klabu hiyo mwenye asili ya Kiasia,
aliwapa fedha wachezaji wafungwe ili kuwakomoa viongozi katika vita iliyokuwa
inaendelea baina yao.
Baadhi ya wachezaji waliobakishwa kikosini
walikuwa ni Kenneth Mkapa, Constantine Kimanda, Sekilojo Chambua, Sanifu Lazaro
‘Tingisha’ na Mohammed Hussein ‘Mmachinga’, wengine wote walitimuliwa kwa
tuhuma hizo.
Baada ya hapo, Yanga iliundwa na wachezaji
waliokuwa wakiandaliwa na Tambwe Leya (sasa marehemu) katika kikosi cha pili,
ambao ni pamoja na Godwin Mashoto (sasa marehemu), Mzee Abdallah, Anwar Awadh,
Maalim Saleh ‘Romario’, Nonda Shaaban na wengineo, waliosajiliwa kutoka timu
mbalimbali kuimarisha kikosi kama Bakari Malima, Reuben Mgaza waliotoka Pan
African.
Baada ya hapo, Simba ilirejesha utemi wake kwa
Yanga kwa kuifunga mfululizo tangu mwaka 2004 hadi ilipojikomboa Oktoba 26,
mwaka 2008, kwa bao pekee la Ben Mwalala dakika ya 15 ya mchezo huo, Uwanja
mpya wa Taifa, Dar es Salaam.
Yanga ilikuwa imeifunga Simba kwa mara ya
mwisho katika mchezo wa kirafiki uliofanyika Aprili 20, mwaka 2003, Uwanja wa
CCM Kirumba mjini Mwanza, mabao 3-0 yaliyotiwa kimiani na Heri Morris, Salum
Athumani na Kudra Omar.
Katika Ligi Kuu, Yanga ilikuwa imeifunga Simba
kwa mara ya mwisho Agosti 5, mwaka 2000, mabao 2-0 yote yakifungwa na Iddi
Moshi Shaaban, anayechezea Villa Squad kwa sasa.
Moshi, aliyekuwa anacheza kwa mara ya kwanza
tangu ametoka kwenye fungate la ndoa yake, alifunga mabao hayo katika dakika za
37 na 47, wakati kwenye mechi iliyofuata Septemba 1, mwaka 2001, bao pekee la
Joseph Kaniki 'Golota' katika dakika ya 76 liliinyima raha Yanga siku hiyo.
Sekilojo Chambua, ambaye kwa sasa ni kocha,
aliinusuru Yanga kulala tena mbele ya Simba Septemba 30, mwaka 2001, baada ya
kuifungia bao la kusawazisha dakika ya 86, kufuatia Kaniki tena kutangulia
kufunga dakika ya 65 kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.
Agosti 18, mwaka 2002, Chambua tena aliinusuru
Yanga kulala, baada ya mwamuzi Victor Mwandike kuipa timu hiyo penalti dakika
ya 89 na kiungo huyo wa zamani kuukwamisha mpira kimiani.
Awali ya hapo, mkongwe Madaraka Suleiman 'Mzee
wa Kiminyio', alitangulia kuifungia Simba bao dakika ya 65, wakati mechi ya
marudiano Novemba 10, mwaka huo, timu hizo zilitoka sare ya bila kufungana.
Septemba 28, mwaka 2003, mabao ya Kudra Omary
dakika ya 42 na Heri Morris dakika ya 55, yaliinusuru Yanga kulala 2-0 mbele ya
Simba, kufuatia Emanuel Gabriel kufunga mapema katika dakika za 27 na 36,
wakati kwenye mchezo wa marudiano Novemba 2, mwaka huo, timu hizo zilitoka sare
ya bila kufungana.
Agosti 7, mwaka 2004, Shaaban Kisiga
alitangulia kuifungia Simba dakika ya 64, kabla ya Pitchou Kongo kusawazisha
dakika tatu tangu kuanza kipindi cha pili na Ulimboka Mwakingwe kufunga bao la
ushindi dakika ya 76.
Bao pekee la Athumani Machuppa katika dakika
ya 82, liliipa ushindi wa 1-0 Simba dhidi ya Yanga Septemba 18, mwaka 2004,
wakati Aprili 17, mwaka 2005 kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro, Aaron
Mwinura Nyanda alitangulia kuifungia Yanga dakika ya 39, kabla ya Nurdin Msiga
kuisawazishia Simba dakika ya 44 na Machuppa kufunga la pili dakika ya 64.
Kwenye mchezo wa marudiano, Uwanja wa Sheikh
Amri Abeid mjini Arusha uliofanyika Agosti 21, mwaka 2005, Nicodemus Nyagawa
aliibuka nyota wa mchezo baada ya kufunga mabao yote mawili yaliyoipa Simba
ushindi wa 2-0 dhidi ya Yanga, dakika za 22 na 56.
Machi 26, mwaka 2006, baada ya Yanga
kuimarisha kidogo kikosi chake, ilianza kugoma kufungwa kwa kulazimisha sare ya
bila kufungana na Simba kama ilivyokuwa kwenye mchezo wa marudiano Oktoba 29,
mwaka huo, mechi zote zikichezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Julai 8, mwaka 2007 katika fainali ya Ligi
ndogo ya Bara, Moses Odhiambo alitangulia kuifungia Simba kwa mkwaju wa penalti
dakika ya pili tu ya mchezo, kabla ya Said Maulid 'SMG' kufunga la kusawazisha
dakika ya 55.
Mchezo huo ulihamia kwenye mikwaju ya penalti
na Simba ilishinda kwa mikwaju ya penalti 5-4 baada ya sare hiyo.
Oktoba 24 mwaka 2008, kwenye Uwanja wa
Jamhuri, Morogoro, Simba wakicheza 10 baada ya Henry Joseph kutolewa kwa kadi
nyekundu mapema tu dakika ya sita, iliibuka na ushindi wa bao 1-0, lililotiwa
kimiani na Ulimboka Mwakingwe dakika ya 23.
Aprili 27 mwaka 2009 katika mchezo wa
marudiano wa Ligi Kuu, timu zilitoka sare ya bila kufungana na Oktoba 26, mwaka
2008, Ben Mwalala alifunga bao dakika ya 15, ambalo lilidumu hadi mwisho wa
mchezo, hivyo kuifutia Yanga uteja uliodumu tangu mwaka 2004.
Bao la Mwalala lilikuwa la kishujaa na la
kihistoria kama ilivyokuwa kwa Jenerali Mkambi, Septemba 5, mwaka 1981.
Katika mchezo wa marudiano kwenye Ligi hiyo,
baina ya watani hao wa jadi, Aprili 19, mwaka 2009 Yanga ilinusurika kulala
2-1, kama si bao la Jerry Tegete dakika ya 90.
Ramadhan Chombo 'Redondo' alitangulia
kuifungia Simba kwa kichwa dakika ya 23, kabla ya Mwalala kusawazisha dakika ya
48 kwa shuti lililowababatiza mabeki na kutinga nyavuni. Haruna Moshi 'Boban'
aliifungia Simba bao lililoelekea kuwa la ushindi dakika ya 62, kabla ya Tegete
kuzima shangwe za wana Msimbazi, tena ndani ya dakika za lala salama.
Oktoba 31, mwaka 2009, bao pekee la Mussa
Hassa Mgosi katika dakika ya 26, lilitosha kuipa Simba ushindi wa 1-0 dhidi ya
Yanga, Uwanja mpya wa Taifa, Dar es Salaam, wakati Aprili 18, mwaka 2010 ilikuwa funga nikufunge kabla ya Weikundu wa
Msimbazi kutoka kifua mbele kwa ushindi wa 4-3.
Mabao ya Simba yalifungwa na Uhuru Suleiman
dakika ya tatu, Mgosi dakika ya 53 na 74 na Mkenya Hillary Echesa dakika ya 90
na ushehe, wakati wa Yanga yaolifungwa na Athumani Iddi dakika ya 30 na Jerry
Tegete dakika za 69 na 89.
Baada ya mechi hiyo, kipa Mzungu wa Yanga,
Obren Curkovic kutoka Serbia aliondoka moja kwa moja kwenye klabu hiyo, kwa
aibu ya kufungwa mabao mengi na ya kuzembe, hasa la nne lililotiwa kimiani na
Mkenya Echesa kwa umbali wa zaidi ya mita 40.
Msimu uliofuata katika mechi ya kwanza ya Ligi
Kuu mjini Mwanza, Yanga ililipa kisasi Oktoba 16, mwaka 2010 kwa bao la Jerry
Tegete dakika ya 70. Ikumbukwe mapema katika kuuzindua msimu huo, Simba na
Yanga zilikutana katika mechi ya Ngao ya Jamii Agosti 18, mwaka 2010 na dakika 90 zilimalizika timu hizo zikiwa
hazijafungana.
Mchezo ukahamia kwenye mikwaju ya penalti na
Yanga ikashinda kwa penalti 3-1. Geoffrey Bonny, Stefano Mwasyika na Isaac
Bokaye walimtungua kipa wa Simba siku hiyo, Ally Mustafa ‘Barthez’ wakati
Mghana Ernest Boakye alikosa. Mohamed Banka ndiye mchezaji pekee wa Simba
aliyemtungua kipa wa Yanga, Mghana Yaw Berko siku hiyo, wakati Emanuel Okwi,
Uhuru Suleiman na Juma Nyosso walipoteza penalti zao.
Wababe hao katika soka ya Tanzania, walikutana
tena katika mchezo wa marudiano wa Ligi Kuu Machi 5, mwaka 2010 na dakika 90
zilimalizika timu hizo zikiwa zimefungana bao 1-1, Yanga wakitangulia kupata
bao dakika ya 59 kwa penalti mfungaji Stefano Asangalwisye Mwasyika.
Penalti hiyo ilitolewa baada ya mchezaji wa
Kizambia wa Yanga, Davies Robby Mwape kuangushwa kwenye eneo la hatari na Juma
Said Nyosso na refa Orden Mbaga akaamuru pigo hilo, ingawa watu walistaajabu
kwa nini hakutoa kadi nyekundu kwa beki wa Simba.
Mussa Hassan Mgosi Mgunya aliisawazishia Simba
dakika ya 73, akiuwahi mpira uliotemwa na Yaw Berko, kufuatia shuti la mpira wa
adhabu kutoka nje kidogo ya eneo la mita 18 lililopigwa na Mganda Emmanuel
Okwi.
Refa Orden Mbaga alizua tafrani uwanjani,
kwanza kwa kulikataa bao la kusawazisha la Simba, kisha akalikubali baada ya
kujadiliana na msaidia wake namba moja.
Mechi iliyopita, mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu,
Yanga ilishinda 1-0 bao pekee la Mzambia Mwape.
Lakini kipindi chote hicho Yanga imeshindwa
kulipa kisasi cha mabao 6-0 na kwa mwenendo ulivyo, hakuna dalili za kisasi
hicho kulipwa leo au kesho. Simba ilifungwa 4-1 na Toto Afrika ya Mwanza,
lakini ilikuwa madhubuti ilipocheza na Yanga Dar es Salaam msimu huo huo.
Kipigo cha 6-0 bado kinaendelea kutonesha donda la wana Yanga miaka nenda
rudi.
Wakati timu hizo zinakutana tena katika mechi ya
marudiano Jumamosi, bado 6-0 ni donda ndugu kwa Yanga. Simba ya sasa iko sawa,
imetoka kumpiga Al Ahly Shandy 3-0 katika mechi ya kwanza hatua ya 16 Bora
Kombe la Shirikisho na inaongoza ligi, zaidi inahitaji kushinda mechi hiyo ya
mwisho ili kujihakikishia ubingwa. Je, wana Yanga waendelee kusubiri iko siku
watafuta aibu hiyo auj hilo ndilo wamelala nalo?
0 comments:
Post a Comment