Kikosi cha Yanga msimu uliopita |
YANGA inaweza kushiriki michuano ya Kombe la Shirikisho la
Soka Afrika mwakani, iwapo itashika nafasi ya tatu mwishoni mwa Ligi Kuu ya
Vodacom Tanzania Bara.
Lakini hiyo ni iwapo tu, Simba SC itafanikiwa kuingia hatua ya
makundi ya Kombe la Shirikisho la Soka Afrika (CAF).
Hiyo ni kwa mujibu wa kanuni mpya za mashindano ya klabu
Afrika za Shirikisho la Soka Afrika (CAF), kwamba nchi ambazo kwa sasa zina
nafasi moja moja za kuingiza timu kwenye michuano ya klabu, zitakuwa zikiongezewa
nafasi moja moja katika michuano ambayo klabu yake imefanikiwa kuingia hatua ya
makundi.
Kwa mfano mwaka huu Sudan imeshirikisha timu nne kwenye
michuano hiyo, mbili Ligi ya Mabingwa na mbili Kombe la Shirikisho, kwa sababu
msimu uliopita iliingiza timu zake kwenye hatua za makundi za michuano yote
hiyo.
Tanzania bado ina nafasi moja moja tu ambazo hadi sasa
tayari Simba na Azam zimejihakikishia kucheza kwa msimu ujao.
Jioni hii, Simba SC imeonyesha dalili za kuifungulia njia
Tanzania kuingiza timu tatu kwenye michuano ya Afrika mwakani, moja Ligi ya
Mabingwa na mbili Shirikisho, baada ya kujiwekea mazingira mazuri ya kuingia
kwenye hatua ya Nane Bora ya Kombe la Shirikisho kwa kuifunga Al Ahly Shandy
mabao 3-0 katika mchezo wa kwanza wa hatua ya 16 Bora ya michuano hiyo, kwenye
Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Sasa Simba inahitaji sare yoyote au kufungwa si chini ya mabao
2-0, ili kuuungana na timu nane zitakazotolewa kwenye Ligi ya Mabingwa kuwania
kucheza hatua ya makundi ya Shirikisho.
Maana yake- Simba ikiitoa Al Ahly Shandy itacheza na timu
iliyotolewa Ligi ya Mabingwa ili kuwania tiketi ya kucheza hatua ya makundi.
Simba leo ingeweza kuondoka na ushindi mnono zaidi wa mabao
5-0, kama si kupoteza penalti kipindi cha kwanza na nafasi moja ya wazi mno
kipindi cha pili.
Kipindi cha kwanza cha mchezo huo, kilikuwa kigumu kwa
Simba, lakini baada ya kupata mawaidha ya kocha wao, Profesa Milovan Cirkovic,
Simba waliingia na mvua ya mabao kipindi cha pili na kuufanya Uwanja wenye
uwezo wa kumeza mashabiki 60,000 uchangamke.
Bao la kwanza la Simba lilifungwa na Haruna Moshi Shaaban
‘Boban’, dakika ya 66 baada ya kupokea pasi nzuri kutoka kwa Felix Mumba Sunzu
Jr.
Sunzu alipokea pasi ndefu ya Uhuru Suleiman Mwambungu,
ambaye aliuwahi mpira uliookolewa baada ya Simba kushambuliwa.
Sunzu alifanya kazi nzuri ya kumtoka beki wa Shandy, Fareed
Mohamed kabla ya kumpa pasi mfungaji.
Bao la pili la Simba lilifungwa na Patrick Mutesa Mafisango,
baada ya kazi nzuri iliyofanywa na Emmanuel Arnold Okwi kuwatoka mabeki wa
Shandy.
Bao la tatu la Simba lilipatikana dakika ya 86, mfungaji
Emanuel Okwi kufuatia gonga safi ya wachezaji wa Simba kwenye eneo la hatari la
Shandy.
Boban alikaribia kufunga tena kabla ya hapo, baada ya kupewa
pasi nzuri akiwa amebaki yeye na kipa, lakini akapiga juu ya lango.
0 comments:
Post a Comment