Kikosi cha Yanga |
YANGA imeanza mazoezi leo baada ya mapumziko ya siku kadhaa,
chini ya uongozi halali uliochaguliwa kikatiba, chini ya Mwenyekiti wake,
Wakili Lloyd Baharagu Nchunga.
Ofisa Habari wa Yanga, Louis Sendeu ameiambia BIN ZUBEIRY
blog kwamba wachezaji wote wa timu hiyo walifanya mazoezi kwenye Uwanja wa
Tiper, Kigamboni, Dar es Salaam leo asubuhi.
Sendeu alisema kwamba program ya mazoezi itaendelea kesho
asubuhi na baada ya mazoezi hayo, timu itaingia kambini moja kwa moja.
Alipoulizwa kuhusu mpango wa Baraza la Wazee kuchukua timu,
Sendeu alisema; “Mimi sijui kuhusu wazee wamefikia wapi, nachojua timu bado ipo
chini ya uongozi halali, uliochaguliwa kikatiba chini ya Mwenyekiti wake
nchinga,”alisema.
Jana, Nchunga aliwaambia Baraza la Wazee la klabu hiyo,
waliotaka kuichukua timu kufuatia mgogoro unaoendelea klabuni, akisema
wamuonyeshe vielelezo vya vyanzo vyao vya mapato awape timu.
Lakini Nchunga amekataa ombi au taarifa ya kujiuzulu kwa
Mjumbe wa Kamati ya Usajili na Kamati ya Mashindano, Abdallah Ahmed Bin Kleb,
wakati huo huo akimkubalia Mjumbe wa Kamati ya Utendaji, Seif Ahmad Magari
kuachia ngazi.
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari asubuhi ya
jana, makao makuu ya klabu makutano ya mitaa ya Twiga na Jangwani, Dar es
Salaam, Wakili Nchunga alisema kwamba Kamati ya Utendaji katika kikao chake cha
juzi ilikubali kujiuzulu kwa Seif, lakini imekataa kwa Bin Kleb.
Kuhusu Wazee kuchukua timu, Nchunga alisema kweli alifanya
nao kikao na akawaambia atakuwa tayari kuwaachia timu waihudumie kwa mujibu wa
Katiba, lakini kwanza lazima watoe vielelezo juu ya vyanzo vyao fedha ili ajue
uhalali wake, wasije wakaiingiza klabu kwenye matatizo.
Alisema anahofia wasije wakawa wanapata fedha kutoka kwa
watu wenye kufanya biashara haramu ya dawa za kulevya- wakaiingiza Yanga kwenye
matatizo.
Nchunga alisema iwapo watamuhakikishia vyanzo halali vya
mapato, kwa mujibu wa Katiba atawaachia jukumu la kuihudumia timu na si kuhodhi
madaraka ya uongozi.
Kwa kuwa Wazee walitaka kuanzia kazi kwenye mechi dhidi ya
Simba Mei 5, mwaka huu, maana yake wakipewa timu, wao wataihudumia, lakini
mapato ya mechi watachukua akina Nchunga.
Baada ya kuifunga JKT Oljoro 4-1 wiki hii, wachezaji wa
Yanga walipewa mapumziko na juzi walikusanyika tayari kuanza mazoezi, ingawa
walikwama kwa sababu ya mvua.
0 comments:
Post a Comment