WACHEZAJI wawili Watanzania wameombewa Hati ya Uhamisho wa
Kimataifa (ITC) kwa ajili ya kucheza mpira wa miguu katika nchini za Denmark na
Jamhuri ya Czech.
Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Boniphace
Wambura ameiambia bongostaz.blogspot.com kwamba Chama cha Soka Denmark (DBU)
kimemuombea hati hiyo William Benard Okum kama mchezaji wa ridhaa ili ajiunge
na timu ya Brabrand IF.
Klabu ya zamani ya Okum ni Viko Pham FC ya Zanzibar.
Naye Samwel Jonathan Mbezi ameombewa hati hiyo na Chama cha Soka
Jamhuri ya Czech (FACR) ili aweze kuchezea timu ya Sokol Dolany akiwa mchezaji
wa ridhaa. Katika maombi hayo, FACR imeonesha kuwa Mbezi kwa sasa hana timu
anayochezea hapa nchini.
TFF inafanya mawasiliano na pande husika kabla ya kutoa hati
hizo kwa wachezaji hao kama walivyoomba DBU na FACR.
Wakati huo huo: Wambura amesema mechi maalumu ya hisani kwa
ajili ya kuchangia timu ya Taifa ya wanawake (Twiga Stars), kati ya timu hiyo
na wasanii wa filamu maarufu kama Bongo Movie itachezwa Mei 4 mwaka huu.
Kwa mujibu wa kampuni ya Edge Entertainment iliyoandaa mechi
hiyo itafanyika kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia saa 10 jioni kwa
kiingilio cha sh. 2,000, sh. 5,000 na sh. 10,000.
Twiga Stars kwa sasa hivi haina mdhamini na iko kambini
katika kambi ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) ya Ruvu mkoani Pwani inashiriki
michuano ya Afrika kwa Wanawake (AWC) ambapo Mei 26 mwaka huu itacheza na
Ethiopia jijini Addis Ababa. Fainali za AWC zitafanyika Novemba mwaka huu
nchini Equatorial Guinea.
0 comments:
Post a Comment