Kibadeni wa tatu kutoka kushoto |
KUCHEZA Simba au Yanga ni fahari kwa mchezaji
wa Tanzania. Lakini ni fahari zaidi iwapo atakuwa mchezaji ambaye atashiriki
mechi baina ya timu hizo.
Inakuwa fahari zaidi iwapo mchezaji atafunga
bao au mabao katika mechi ya watani wa jadi, kwani huwafanya maelfu ya
mashabiki wa timu yake walitaje jina lake na kushangilia kwa raha zao. Wengine,
hupewa zawadi kutokana na kufunga kwenye mechi hizo za watani.
Wapo waliolewa sifa na kupotea kwenye ramani
ya soka haraka, kwa sababu tu ya kuvimba kichwa baada ya kufunga mabao
mfululizo kwenye mechi za watani.
Said Sued 'Scud', alifunga bao pekee la ushindi
kwenye mechi ya watani wa jadi, akiwa anaichezea Yanga alitikisa nyavu za Simba
dakika ya saba katika mchezo wa Ligi Daraja la Kwanza Tanzania Bara, sasa Ligi
Kuu Mei 18, mwaka 1991.
Huo ukiwa msimu wake wa kwanza kwenye klabu
hiyo, hakika ilikuwa furaha kubwa kwake, kwani tangu hapo aliaminika na kuwa
mchezaji wa kudumu kwenye kikosi cha kwanza cha Yanga.
Chipukizi huyo wa wakati huo, alipata ngekewa
ya kuifunga tena Simba katika mchezo uliofuata wa marudiano wa ligi baina ya
watani wa jadi, likiwa pia bao pekee la ushindi Agosti 31, mwaka huo huo 1991,
jambo ambalo lilimfanya awe maarufu zaidi.
Lakini katika mastaajabu ya wengi, Scud
hakurejea kwenye kikosi cha Yanga cha mwaka 2002 na huo ukawa mwisho wa
umaarufu wake kwenye soka ya Tanzania.
Kama wapo wanaodhani Scud alifanya kubwa sana
katika historia ya watani wa jadi, watakuwa wapo mbali kabisa na ukweli, kwani
Abdallah Kibadeni (pichani kulia juu), maarufu kama Chifu Mputa ama King, au Ndululu kama
walivyokuwa wakimuita Wakenya, anaweza kusimama na kusema ana kubwa la
kujivunia katika historia ya mechi baina ya Simba na Yanga ambalo hadi kitabu
hiki kinaingia sokoni lilikuwa halijavunjwa.
Abdallah Kibadeni ndiye mchezaji pekee hadi
sasa aliyeweza kufunga mabao matatu peke yake katika mchezo mmoja kwenye mechi
za watani wa jadi katika Ligi.
Hiyo ilikuwa ni Julai 19, mwaka 1977 katika
Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, sasa Uwanja wa Uhuru, wakati Yanga
ilipotandikwa 6-0 na Simba.
Siku hiyo, Kibadeni alitikisa nyavu za Yanga
katika dakika za 10, 42 na 89, wakati mabao mengine ya Wekundu wa Msimbazi,
yalitiwa kimiani na Jumanne Hassan 'Masimenti' dakika ya 60 na 73 na jingine
Selemani Sanga wa Yanga alijifunga mwenyewe dakika ya 20 katika harakati za
kuokoa krosi ya Ezekiel Greyson 'Jujuman'.
Hivyo siku hiyo mbali na Simba kushangilia
kulipa kisasi cha kulala 5-0 kwa Yanga, Juni Mosi mwaka 1968, Kibadeni alikuwa
ana sherehe binafsi za kutumbukiza tatu peke yake kwenye mechi baina ya watani
hao, jambo ambalo liliwashinda wengi kabla yake kati ya waliowahi kuvaa jezi za
Simba au Yanga.
Hakuna cha Sunday Manara 'Computer' wala
Maulid Dilunga 'Mexico' aliyewahi kufanya hivyo zaidi ya King Kibadeni pekee.
0 comments:
Post a Comment