Messi |
MECHI kati ya vigogo vya Ulaya, Barcelona na AC Milan inaonekana
kuwa mechi pekee ya kucheza kwa kushambuliana katika mechi za marudiano za Robo
Fainali ya Ligi ya Mabingwa wiki hii, huku Real Madrid na Bayern Munich zote ni
kama zimekwishafuzu na Chelsea wana nafasi nzuri.
Mabingwa watetezi Barca walitoka sare ya 0-0 mjini Milan katika
mechi ya kwanza wiki iliyopita na kikosi cha Pep Guardiola bado kinapewa nafasi
kubwa ya kusonga mbelena wapinzani wao kutoka Serie A kwa sare ya nyumbani,
kidogo wanaonekana kutokuwa na nafasi wakicheza ugenini.Vigogo wengine Ulaya, Bayern watakuwa wenye kujiamini mno wakiingia kwenye mchezo wa marudiani Jumanne dhidi ya Olympique Marseille baada ya kushinda 2-0 Ufaransa wiki iliyopita, wakati timu wanayoweza kukutana nayo kwenye Nusu Fainali, Real wataikaribisha Apoel Nicosia ya Cyprus Jumatano wakitoka kushinda 3-0 ugenini.
Chelsea walishinda 1-0 ugenini na Jumatano watakuwa wenyeji wa Benfica na timu hiyo ya London, chini ya kocha mpya wa muda Roberto Di Matteo, imeonekana kuimarika huku Fernando Torres akifufua makali kwa kutengeneza mabao na kufunga pia.
Lakini macho ya wengi yatakuwa Nou Camp ambako Barca – inayosifiwa na wachambuzi wengi wa soka duniani kama timu bora daima – itachuana na mabingwa mara saba Ulaya, Milan yenye mshambuliaji wao wa zamani, Zlatan Ibrahimovic.
Milan ilionekana kama inacheza ugenini katika mechi ya wiki iliyopita kwenye Uwanja wa San Siro, lakini waliwamudu Barca Mwanasoka Bora wa Dunia, Lionel Messi wakati Ibrahimovic na Mbrazil Robinho walikuwa mwiba.
“Ni mechi muhimu ya mwaka na wakati huo huo ni mechi moja nzuri sana,” Guardiola aliwaambia Waandishi baada ya ushindi wa 2-0 nyumbani dhidi ya Athletic Bilbao katika La Liga mwishoni mwa wiki.
“Bilbao hawapaki basi, wanakufuata. Ni tofauti kabisa na Milan,ni kama usiku na mchana.”
Kocha wa Milan, Massimiliano Allegri alihofia kuwashambulia Barca wiki iliyopita lakini haikuwa kama ilivyozoeleka kwa mfumo wa zamani wa kujihami wa Italia.
Alisema watakwenda kushambulia kusaka mabao katika mchezo wa pili kwa heshima kubwa dhidi ya Barca waliotwaa mataji mawili mfululizo ya Ulaya.
Allegri alisema kama vijana wake watamsikiliza kwa makini na kufuata maelekezo yake, kama wakishindwa kupata bao, watoe sare ya 0-0 ili penalti ziamue mshindi.
Mshambuliaji wa Sweden, Ibrahimovic dhahiri atapenda kufunga bao kwenye Uwanja wa Nou Camp na kuitoa timu yake ya zamani, Barca aliyoiacha miezi 18 iliyopita baada ya kutofautiana na Guardiola.
Torres alionekana kufilisika kisoka baada ya kucheza ovyo kwa muda mrefu, lakini pasi yake kwa Salomon Kalou aliyefunga bao la ushindi dhidi ya Benfica na bao alilofunga mwishoni mwa wiki katika Ligi Kuu dhidi ya Aston Villa, vinaleta sura tofauti kwa sasa.
Nyota huyo wa Hispania, anatumai atapata nafasi Jumatano wakati Didier Drogba akisumbuliwa na maumivu ya goti.
Beki wa zamani wa Benfica, David Luiz pia yuko kwenye hatihati.
Benfica wanaweza kuwa na imani ya kubadilisha matokeo London, lakini Marseille na vibonde kutoka Cyprus, Apoel, wanapaswa kujivunia japo kufika hatua hii na safari yao ya kuaga imewadia.
Marseille inayofundishwa na Didier Deschamps ilifika hatua hii kimiujiza, ikiifunga 3-2 Borussia Dortmund ya Ujerumani, huo ukiwa ushindi wao wa pili katika kundin lao dhidi ya mabingwa hao wa Bundesliga.
Pamoja na hayo, wakawatoa na mabingwa wa mwaka 2010, Inter Milan katika hatua ya 16 bora na sasa mbele ya timu nyingine ya Ujerumani, wanatakiwa kushinda 3-0 kwa Bayern ambao wapo kwenye kiwango kizuri na mechi ya kwanza mabao yake yalifungwa na Mario Gomez na Arjen Robben.
Kikosi cha Jupp Heynckes, pia kimepania kucheza fainali ya michuano hiyo mei, mwaka huu kwenye Uwanja wao wenyewe.
0 comments:
Post a Comment