Samatta anafunga hapo mpira ushatimkia nyavuni, lango halionekani. |
MBWANA Ally Samatta, maarufu kama Sama Goal, jana aliibuka
shujaa kwenye Uwanja wa Kibassa Maliba, baada ya kufunga bao moja katika
ushindi wa 2-0 kwa timu yake kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika.
Tout Puissant Mazembe imeanza vizuri hatua ya 16 Bora ya
Ligi ya Mabingwa Afrika, baada ya kushinda 2-0 dhidi ya El Merreikh ya Sudan
mjini Lubumbashi.
Wageni wanaonolewa na RICARDO waliuanza mchezo huo vizuri na
mapema tu shuti lao kali la mpira wa adhabu liliokolewa na kipa KIDIABA na
shambulizi la kwanza dakika ya 39 lilipaa juu ya lango.
Kama ilivyokuwa dhidi ya Power Dynamos, safu ya ushambuliaji
ya Mazembe inayoundwa na wakali kama MPUTU, Singuluma, Kalaba na SAMATA ilikuwa
mwiba mkali.
Mazembe ilipata kona sita wakati wapinzani wao hawakupata
hata moja na katika kona hizo ni moja tu iliyozaa matunda kwa SAMA GOAL kufunga dakika ya 22
kwa kichwa akiunganisha kona iliyochongwa na MPUTU.
Hadi dakika 45 za kwanza zinamalizika Mazembe inayofundishwa
na Lamine Ndiaye ilikwenda kupumzika ikiwa inaongoza kwa bao hilo moja tu.
Nahodha Tressor Mputu aliifungia Mazembe bao la pili dakika ya
70, akipiga shuti zuri nje ya eneo la penalti na mpira kutinga nyavuni upande
wa kulia wa lango.
Hakuna kilichobadilika katika dakika 20 za mwisho, licha ya
nafasi kadhaa zilizoshindikana kutumiwa vema.
Mazembe sasa inatakiwa kwenda kupigana kiume ugenini kulinda
ushindi wake huu, kwani ni mwembamba.
Samatta, Mtanzania aliyetokea Simba SC kujiunga na Mazembe
katikati ya msimu uliopita, sasa ana mabao mawili katika Ligi ya Mabingwa ndani
ya mechi mbili.
Awali alifunga katika sare ya 1-1 na Power
Dymanos ya Zambia, mchezo wa kwanza hatua ya 32 Bora, lakini sikku hiyo aliumia
bega na akakosa mechi ya marudiano.
0 comments:
Post a Comment