Papic |
Papic: Kibali kilinizuia kwenda Arusha | Send to a friend |
Thursday, 26 April 2012 20:35 |
KOCHA wa Yanga, Kostadin Papic amesema alishindwa kwenda jijini Arusha wakati timu yake ilipokuwa ikiikabili JKT Oljoro kwa sababu kibali chake cha kufanya kazi nchini kilikuwa kimeisha muda wake. Papic hakuonekana katika benchi la Yanga wakati timu hiyo ilipoifunga JKT Oljoro mabao 4-1, ambapo majukumu yake yalichukuliwa na msaidizi wake Fredy Minziro. Akizungumza na Mwananchi jana, Papic alisema kibali chake cha kufanya kazi nchini kilimalizika muda wake Aprili 24 hivyo kama angeendelea kuifundisha Yanga baada ya tarehe hiyo ingekuwa kinyume na taratibu za nchi. "Unaniuliza kwa nini sikusafiri na Yanga? ok sawa, kibali changu cha kufanya kazi kimemalizika tangu Aprili 24. "Hili jambo hata viongozi wangu wanalifahamu na ndio maana nilisema mwisho wa kuifundisha Yanga ni Aprili 24,"alisema Papic. Awali msemaji wa Yanga, Louis Sendeu alisema wanashangazwa na Papic kutosafiri na timu hiyo na wanahisi hajui majukumu yake wala mkataba wake. "Wenyewe tunamshangaa Papic, sisi tunavyojua mkataba wake unamalizika mwishoni mwa Ligi inawezekana hajui mkataba wake unavyosema, tuna mashaka kuwa hajausoma mkataba wake vizuri," alisema Sendeu mara baada ya mchezo huo. Kuhusu hatma yake ya kuinoa timu hiyo baada ya kibali chake cha sasa kuwa kimeisha muda wake, Papic alitarajiwa kukutana na mwenyekiti wa Yanga, Lloyd Nchunga ili kujadili suala hilo. "Nitakutana na mwenyekiti (Lloyd Nchunga) jioni hii (jana) ili kujadiliana juu ya suala hilo pamoja na mkataba mpya. "Nadhani baada ya hapo nitajua nini kinachoendelea na ukinitafuta nitakuambia,"alisema Papic. Awali Papic alitangaza angeondoka nchini jana. |
0 comments:
Post a Comment