Barca wakifuatia taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu uliopita Uwanja wa Wembley, chini ya kocha Guardiola |
UNADHANI nini kimemwondoa Pep Guardiola
Barcelona? Je, aliona kutosheka baada ya kutumia vizuri muda wake alipokuwa
Catalan? Je, ni sahihi kwa kipindi hiki alichoondoka na kuiacha timu mikono
mitupu?
Jibu la waliowengi watasema kwamba kukosa
nafasi ya kunyakua taji lolote kwa msimu huu – ndicho chanzo kikubwa
kilichofungua njia kwa kocha huyo kuamua kufungasha virago vyake.
Guardiola alishuhudia kikosi chake
kikipoteza nafasi ya kutetea ubingwa wa La Liga mbele ya Real Madrid baada ya
kunyukwa kwenye mechi ya El Clasico.
Na mbaya zaidi, siku chache baadaye, wababe
hao wa Nou Camp walijikuta wakilitema taji jingine la Ligi ya Mabingwa barani
Ulaya baada ya kutupwa nje ya michuano hiyo katika hatua ya nusu fainali na
Chelsea.
Lakini, kuna jambo ambalo mashabiki wa soka
watakuwa hawalifahamu lililomfanya Guardiola kuamua kusahau mafanikio yake
aliyopata kwenye kikosi hicho katika misimu yake minne aliyodumu na kuamua
kuondoka.
Pep ameamua kung’atuka Barca mwishoni mwa
msimu huu kwasababu ya tofauti zake zilizoibuka dhidi ya rais wa klabu na
presha inayowakabili wachezaji wake.
Oktoba mwaka jana – mchambuzi wa masuala ya
michezo, Antony Kastrinakis – anayeandika kolamu yake ya Kastro kwenye gazeti
la The Sun, aliwaeleza wasomaji wake kwamba Guardiola atang’atuka Barca
mwishoni mwa msimu.
Na hilo
kwa kiasi kikubwa lilichangiwa na hasira zilizopo baina ya rais Sandro Rosell
dhidi ya mtangulizi wake, Joan Laporta.
Na hilo
lilithibitishwa kama alivyozungumza Guardiola
mwenyewe kwamba: “Nilimweleza rais mwisho mwa Septemba au mwanzoni mwa Oktoba
kwamba huu ni msimu wangu wa mwisho.”
Kwa kauli hiyo ni wazi kabisa kilichomtoa
Guardiola kwenye dimba la Nou Camp si Barca kushindwa kunyakua taji msimu huu,
ni kitu kingine kabisa kinachoanzia kwenye uongozi.
Vita ya Rosell dhidi ya Laporta — mtu
ambaye alimteua Guardiola — inaonekana kuhusika kwa namna fulani katika jambo hilo la Pep kuamua
kutimka.
Heshima ya Guardiola kwa Laporta haina
kifani, lakini hiyo si sababu pekee iliyochangia kocha huyo kuamua kuondoka
mwenyewe kabla ya Rosell kumwonyesha njia.
Guardiola anafanya kazi saa 24 kwa wiki
nzima na hivyo kukosa nafasi na muda wa kutosha wa kupumzika na familia yake.
Licha ya kwamba hilo ni jambo la lazima, mazingira mengine
katika Nou Camp yanaweka bayana kwamba hali si shwari kwa Guardiola kwamba
hayupo kwenye mahusiano mazuri na baadhi ya wachezaji wake nyota, jambo ambalo
si zuri.
Lilikuwa ni suala la kawaida tu kwa
Guardiola – ambaye alihitaji wachezaji wake kuwa na nidhamu ya kutosha na hivyo
kuifikisha timu kwenye mafanikio inayostahili.
Urafiki kwenye kikosi hicho ungemfanya
Guardiola kuwa kwenye wakati mgumu wa kuwaonyesha baadhi ya wachezaji wake njia
ya kutokea mwishoni mwa msimu huu.
Baadhi ya wataalamu wa masuala ya soka
wanaamini suala la kukichekecha kikosi hicho halikuwa la kupitwa na kwamba
Barca inahitaji kuboresha kikosi chake mwishoni wa msimu huu kama
kinahitaji kuwa na nguvu itakayowafanya kuendelea kupambana na kuonyesha
kandanda la kishindani.
Guardiola alitua kwenye kiti hicho
akimbadili Frank Rijkaard mwaka 2008 na moja kwa moja akawaondoa wachezaji
waliokuwa na ‘mapembe’ wake ule, Ronaldinho na Deco.
Alifanya hivyo si kwamba nyota hao
walishuka kiwango, hapana ni kwasababu hawakuwa wachezaji wake.
Kwa wakati huu, Guardiola hakutaka kuuza
wachezaji ambao alishirikiana nao muda wote na kufanikiwa kutwaa mataji yote
yaliyopita mbele yao .
Gerard Pique, mchezaji wa kwanza
aliyesajiliwa na Guardiola, hakumchezesha kwenye mechi ya El Clasico iliyofanyika
siku kadha zilizopita.
Cesc Fabregas aliwekwa benchi kwenye mechi
dhidi ya AC Milan kwenye dimba la San Siro na dhidi ya Bilbao na kwenye El Clasico.
Kijamii, yote yalionekana kawaida – lakini
kiwango cha Pique kipo kwenye mushkeli mkubwa na hilo linahitaji kuwapo ndani ya klabu hiyo
kutambua kinachoweza kutokea siku za usoni.
Hayo ni baadhi ya matukio ambayo, Guardiola
angelazimika kumpiga bei Pique mwishoni mwa msimu, jambo lingekuwa gumu kwa
kocha huyo.
Nahodha wa zamani wa Arsenal, Cesc alipoteza
nafasi mbili muhimu kabisa za mabao kwenye mchezo wao dhidi ya Stamford
Bridge na alionyesha kiwango kibovu sana
kwenye mechi ya marudiano dhidi ya Chelsea — licha ya kwamba alipata penalti,
ambapo Lionel Messi akashindwa kufunga.
Mwingine ni Dani Alves, moja ya mabeki bora
kabisa pembeni dunia. Huyu alitokea benchi kwenye mechi dhidi ya Chelsea.
Kiwango cha Mbrazil huyo kimeshuka kwa
asilimia kubwa na mazungumzo ya kutaka kuhamia Anzhi Makhachkala yamekuwa
bayana kwa sasa.
Fabregas ataendelea kubaki Nou Camp, hilo halina ubishi.
Lakini, je, Pique na Alves watabaki? Pep hakutaka kuhusika kwenye kufanya
uamuzi huo.
Kingine, kuna suala la Rosell kutaka
kumnunua Mbrazil, Neymar na Guardiola hataki. Kumsajili Neymar itakuwa ushindi
mkubwa dhidi ya mahasimu wao Real Madrid.
Lakini, Guardiola amekijenga kikosi chake
kupitia Messi na hivyo hakutaka kuingiza mchezaji mwingine ambaye atasababisha
mtikisiko kwenye vyumba vya kubadilishia nguo Nou Camp.
Hayo ndio baadhi ya mambo yaliyomfanya
Guardiola kuamua kumaliza nyakati zake katika kikosi hicho cha Barca.
Kwa sasa ameshatangaza kuondoka na mengi
yameanza kuhusishwa naye kuhusu hatima yake.
Maneno kutoka Hispania yanabainisha kwamba Pep
Guardiola anapenda kwenda kufanya kazi England .
Si kufanya kazi England ,
si kufanya kazi Manchester United – bali England inayotajwa hapa ni timu ya
taifa, Three Lions.
Imebainika kwamba kocha huyo anaweza
kushawishika kuchukua kibarua kingine kuliko maelezo yake ya awali ya kutaka
mapumziko ya mwaka mmoja nje ya soka.
Kuinoa timu ya taifa kumtafanya kuwa na
muda wa kutosha wa kupumzika na familia yake kwasababu mechi ni chache na
safari ni chache pia.
Lakini, tatizo kubwa lililopo England
ni kwamba Chama cha soka nchini humo (FA) kutaka kocha mzawa na juzi usiku
walimbainisha Roy Hodgson kwamba ni chaguo lao namba moja.
Lakini, kwa sasa kocha bora kabisa duniani yupo
huru na hivyo FA wanatambua nafasi ipo wazi kwenye timu yao
ya taifa, haitakuwa makosa kama wataweka
pembeni suala la uzawa na kumchukua bosi huyo.
0 comments:
Post a Comment