Jose Mourinho haoni sababu ya kuondoka Real Madrid
KOCHA Jose Mourinho amesema kwamba hajapanga kuondoka Real Madrid mwishoni mwa msimu akiwa amekaribia kutwaa taji la nne la Ligi Kuu katika nchi tofauti.
Real inaongoza kwa pointi saba La Liga ya Hispania, lakini Mourinho amekuwa akihusishwa na mipango ya kuhamia Chelsea na Manchester City za England.
"Kwa sasa mustakabali wangu si muhimu, lakini nafikiri nitakuwa hapa msimu ujao," alisema kocha huyo wa Real.
"Nina mkataba na klabu na hakuna sababu ya kuondoka. ni vizuri kubaki katika klabu kwa miaka minne au mitano."
Mreno huyo aliuteuliwa Mei mwaka 2010, akisaini mkataba wa miaka minne, lakini taarifa za mapema mwaka huu zilidai anataka kurejea England mwishoni mwa msimu.
Mourinho alisema: "Mwishoni mwa msimu nitakuwa na muda wa kuzungumza na wachezaji na Wakurugenzi na tutaamua jambo zuri kwangu, kwa klabu na kwa timu."
Baada ya ushindi wa 2-1 Jumamosi dhidi ya wapinzani wao wa jadi, Barcelona, Mourinho anakaribia kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu kwa mara ya nne katika nchi tofauti, baada ya awali kuziongoza FC Porto, Chelsea na Inter Milan kutwaa ubingwa wa ligi za nchi zao, Ureno, England na Italia.
Usiku huu ameshindwa kutimiza ndoto za kutwaa taji la tatu la Ligi ya Mabingwa Ulaya, baada ya Real Madrid kutolewa na Bayern Munich.
0 comments:
Post a Comment