Zamoyoni Mogella |
ZAMOYONI Mogella amewahi, hajawahi kuifunga
Yanga?
Mpachika mabao mashuhuri wa zamani nchini,
Mogella aliyezaliwa miaka 58 iliyopita mjini Morogoro, amekuwa gumzo kubwa hata
baada ya kustaafu kwake soka.
Kumekuwa na ubishi kuhusu nyota huyo kwamba
aliwahi au hajawahi kuifunga Yanga. Ukweli ni kwamba, Mogella aliifunga Yanga,
tena lilikuwa bao ambalo lilielekea kuipa ushindi wa jumla wa mchezo huo Simba.
Ilikuwa ni Julai 14, mwaka 1984 kwenye Uwanja
wa Taifa, sasa Uhuru mjini Dar es Salaam, wakati Golden Boy alipotangulia
kuifungia Simba kwenye mchezo wa Ligi Daraja la Kwanza Tanzania Bara, sasa Ligi
Kuu katika dakika ya 17.
Hata hivyo, mchawi wa vichwa enzi hizo, Abeid
Mziba aliisawazishia Yanga bao hilo katika dakika ya 39.
Kabla ya kujiunga na Simba, Mogella alichezea
timu za Jogoo, Reli, Tumbaku zote za Morogoro tangu mwaka 1974, hadi mwaka
1981, alipotua Mtaa wa Msimbazi.
Alijiunga na Simba baada ya soka yake
kuwavutia viongozi wa Simba alipokuwa akichezea timu ya taifa ya vijana chini
ya umri wa miaka 20. Mogella aling'ara zaidi alipokwenda na timu hiyo kwenye
michuano maalumu ya vijana iliyofanyika nchini Norway.
Alitua Simba kwa dau la Sh 50,000 tu, ambayo
tena alilipwa kwa awamu, kwanza 25,000 na nyingine akamaliziwa baadaye.
Tangu anajiunga na Simba, Mogella pia alianza
kuichezea timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars.
Mwaka 1986, Mogella alikwenda kucheza soka ya
kulipwa nchini Kenya katika klabu ya Volcano na baada ya miezi sita alikwenda
Oman ambako alicheza hadi mwaka 1989.
Alirejea Simba mwaka 1990 na aliichezea hadi
mwaka 1992, alipohamia Yanga ambako alicheza kwa msimu mmoja tu.
Ingawa wengi wanajua Athumani Juma Chama
'Jogoo' ndiye pekee aliyekuwa akimpa wakati mgumu Mogella uwanjani, lakini
mwenyewe anawataja pia Yussuf Ismail Bana, Allan Shomari na Isihaka Hassan
kwamba nao walikuwa wakimuumiza kichwa
Hivi sasa Mogella ni baba wa watoto wanne,
akiwemo Farshed, anayefuata nyayo za baba yake kwenye soka.
Farshed, aliyezaliwa miaka 17 iliyopita, mbali
na kucheza soka shuleni kwao, pia anachezea timu ya mtaani, Buibui nafasi ya
ushambuliaji kama baba yake. Farshed ana pacha wake, Fuhal, aliyehitimu kidato
cha Nne mwaka jana katika Shule ya Sekondari Green Acres.
0 comments:
Post a Comment