SIMBA na Yanga zitakutana katika mechi ya mwisho ya kufunga msimu huu wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, mapema mwezi ujao.
Mchezo wa kwanza, Yanga iliifunga Simba 1-0, bao pekee la Mzambia Davies Mwape mwishoni mwa mwaka jana.
Watangazaji wa Televisheni ya kulipia ya
kimataifa SuperSport ya Afrika Kusini, waliwahi kuiingiza mechi ya Simba na
Yanga katika orodha ya mechi tatu kali za wapinzani wa jadi Afrika - nyingine
zikiwa ni kati ya Orlando Pirates na Kaizer Chiefs za Afrika Kusini na Al Ahly
dhidi ya Zamalek za Misri.
Hakuna ubishi upinzani wa Ahly na Zamalek huo
ni dunia nzima - ni zaidi ya upinzani, lakini kwa Afrika fuatilia ligi nyingi,
utagundua Simba na Yanga ni mechi yenye mvuto wa kipekee na ndiyo maana hivi
sasa SuperSport wamekuwa wakionyesha mfululizo mechi za watani hao, ingawa
hawana mkataba na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) wa kuonyesha mechi za Ligi
Kuu.
Unaweza kutilia shaka kiwango cha soka cha
timu hizo, lakini si upinzani wao kwa maana ya upinzani. Upinzani wao ni sehemu
ya burudani na kama iko siku zitakuwa imara na kucheza soka ya kuvutia, basi
burudani itakuwa mara mbili.
Hata hivyo kuna mambo mawili au matatu ambayo
kwa kiasi fulani yamekuwa yakipunguza ladha ya mechi za watani hao wa jadi.
Awali tatizo kubwa lilikuwa Uwanja mdogo wa
Uhuru, lakini tangu kukamilika kwa Uwanja wa Taifa ambao tumeshuhudia mechi
zote zilizochezwa hapo, haijatokea mechi hata moja mashabiki wakajaza viti,
mambo yamekuwa mazuri.
Matatizo mawili yaliyobakia ni viwango vya
timu kuboreshwa, ili ifike wakati pamoja na upinzani, kukamiana lakini
watazamaji washuhudie soka safi.
Tatizo la pili ni marefa, kweli ilipofikia na
kama kweli lengo ni kuiongezea msisimko zaidi mechi ya watani, waamuzi wa
Tanzania wawekwe kando na watumike waamuzi kutoka nje ya nchi, tena ikibidi nje
kabisa ya nchi tatu za Jumuiya yetu ya Afrika Mashariki.
Rejea mchezo wa Machi 5, mwaka 2011 Uwanja wa
Taifa, refa Orden Mbaga aliivuruga mno mechi hiyo, kutokana tu na pengine
mchecheto ama kutaka kufanya kile ambacho kinaitwa ‘kubalansi’ mchezo au
kukwepa lawama, matokeo yake anafanya madudu.
Dakika ya 58 Juma Said Nyosso alimkwatua
Davies Robby Mwape kwenye eneo la hatari akawapa penalti Yanga na kilichofuatia
wengi walijua beki huyo wa Simba atatolewa nje kwa kadi nyekundu, badala yake
akampa kadi ya njano.
Ngumu kuamini Mbaga, refa mwenye beji ya
Shrikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) hajui alipaswa kufanya nini kwa Nyosso,
lakini kwa sababu ni refa wa nyumbani na aliongoza wapinzani wa jadi katika
mechi ya nyumbani, alihofia kumtoa mchezaji kwa kadi nyekundu angeshushiwa
lawama nzito. Marefa hufanyiwa fujo na kupigwa na mashabiki, labda alihofia
hali hiyo pia.
Dakika ya 73 Simba walipata bao safi la
kusawazisha lililofungwa kwa kichwa na Mussa Hassan Mgosi, aliyeuwahi mpira
uliotemwa na kipa Yaw Berko kufuatia
shuti la mpira wa adhabu, lililogonga mwamba wa juu na kudondokea nyavuni kabla
ya kuokolewa na mabeki wa Yanga.
Halikuwa bao lenye shaka yoyote, hakukuwa na
kuotea wala dosari yoyote, lakini haieleweki kwa nini Mbaga alilikataa bao hilo
awali.
Ilikuwa offside au mpira haukutinga nyavuni
hadi akalikataa kwanza? Haijulikani, lakini alilikubali baada ya wachezaji wa
Simba kumuambia aangalie kwenye TV iliyokuwapo uwanjani marudio ya tukio lile
na baada ya hapo akaenda kujadiliana na msaidizi wake, ndipo akalikubali.
Mbaga alichemsha- lakini si Mbaga tu, marefa
wengi wa Tanzania waliwahi kutokota kabla yake na nitakumbushia baadhi ya
mechi.
Machi
31, mwaka 2002 katika fainali ya Kombe la Tusker, Simba ikishinda 4-1, refa
Abdulkadir Omar ‘Msomali’ aliivuruga mechi na kuvuruga amani uwanjani pia kwa
madudu yake.
Kwa
nini? Katika mechi hiyo ya fainali iliyohudhuriwa na
rais mstaafu wa awamu ya pili ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ali Hassan
Mwinyi, chupuchupu ivunjike dakika ya 32, baada ya Madaraka Suleiman kufunga
bao ambalo kabla ya kufumua shuti lililomshinda kipa Manyika Peter, aliushika
mpira kwa makusudi, ili kuuweka sawa.
Rais wa Yanga wakati huo, Tarimba Abbas
aliinuka na kuwaonyesha ishara wachezaji wake watoke uwanjani na hapo ndipo
meza kuu aliyokuwa ameketi mzee Mwinyi, ilipoanza kushambuliwa kwa chupa za
maji na mashabiki wa Yanga. Abdulkadir Omar alisubiri hadi vurugu zilipotulizwa
na FFU ndipo akaendeleza mchezo. Tarimba alitoka nje na hakutaka kuendelea
kushuhudia mchezo huo. Baada ya hapo, alifungiwa na Chama cha Soka Tanzania,
(FAT), sasa TFF kabla ya kujiuzulu uongozi wa klabu hiyo baadaye.
Agosti 18, mwaka 2002 Simba na Yanga zikitoka
sare ya 1-1 katika mechi ya Ligi Kuu, refa Victor Mwandike aliwaacha mashabiki
wa Simba midomo wazi kwa kuwapa Yanga penalti dakika ya 89 na ushehe, ambayo
Sekilojo Chambua aliitumia vema kuisawazishia bao timu yake, baada ya Simba
kutangulia kufunga kupitia kwa Madaraka Suleiman dakika ya 65.
Oktoba 24, mwaka 2007, refa Osman Kazi
alikataa mabao matatu yaliyofungwa na Yanga, yote akidai kipa Juma Kaseja
alisukumwa na wachezaji wa Yanga, lakini kwa yeyote atakayerudia kuangalia DVD
ya mchezo ule, hawezi kuona ukweli wa madai ya Kazi.
Awali ya hapo, Kazi aliwahi kupuliza filimbi
ya kumaliza dakika 45 za kipindi cha kwanza katika Nusu Fainali ya Kombe la
Tusker mwaka 2005 mjini Mwanza, wakati mchezaji wa Yanga, Said Maulid ‘SMG’
amekwishawatoka mabeki wa Simba na anakwenda na mpira mbele yake amebaki Juma
Kaseja tu.
Refa ni mwamuzi wa mwisho- lakini kwa wana
Yanga walijutia mno tukio lile kwenye mchezo ambao mwishowe walifungwa 2-0, kwa
mabao ya kipindi cha pili ya Emmanuel Gabriel na Mussa Mgosi.
Aprili
19, mwaka 2009, Jerry Tegete aliifungia Yanga bao la kusawazisha kwa
mkono na kutengeneza sare ya 2-2, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Refa makini
asingeweza kukubali bao lile, hivyo kwa haya yote lazima tukubali marefa wa Tanzania
hawawezi tena kuchezesha mechi za watani wa jadi.
Sababu nyingine za marefa wetu kuzishindwa
mechi hizo ni mapenzi yao kwa moja ya timu hizo, kitu ambacho Misri wamekiepuka
na mechi ya Zamalek na Ahly inachezeshwa na marefa kutoka nje ya nchi yao.
Nakumbuka refa kutoka Uganda, Dennis Bate
aliyechezesha Nusu Fainali ya Kombe la Tusker mwaka 2009 kati ya Simba na
Yanga, aliiongoza vizuri mechi hiyo na akadhibiti ujanja wote wa wachezaji
kutaka kumdanganya na hatimaye aboronge.
Kuna wachezaji wanaitwa wazoefu wa mechi za
Simba na Yanga na hawa wamekuwa wakiwapoteza sana marefa kwa uzoefu wa kucheza
mechi hizo, lakini kama marefa watatoka nje ya Tanzania, tena wa kiwango cha
beji za FIFA, uhondo wa mechi za watani utaongezeka maradufu. Ila kwa sasa, marefa
wetu hawaziwezi tena mechi hizi. Wakati sasa umefika, TFF ifikirie kuleta marefa wa kigeni, wenye beji za FIFA na rekodi ya kuongoza mechi kubwa zenye upinzani wa aina ya upinzani wa Simba na Yanga, kuchezesha Derby la Tanzania.
0 comments:
Post a Comment