// Disable text selection (not fully reliable) function disableSelection(element) { element.setAttribute('unselectable', 'on'); element.style.userSelect = 'none'; element.style.MozUserSelect = 'none'; element.style.webkitUserSelect = 'none'; } // Apply to the entire document body document.addEventListener('DOMContentLoaded', function() { disableSelection(document.body); }); LULU TAABANI POLISI, MAMIA WAFURIKA NYUMBANI KWA KANUMBA - BIN ZUBEIRY SPORTS - ONLINE LULU TAABANI POLISI, MAMIA WAFURIKA NYUMBANI KWA KANUMBA - BIN ZUBEIRY SPORTS - ONLINE
  • HABARI MPYA

    Saturday, April 07, 2012

    LULU TAABANI POLISI, MAMIA WAFURIKA NYUMBANI KWA KANUMBA

    Ndugu wa Kanumba akizungumza na Waandishi
    MVUA inanyesha, lakini mamia ya watu wamejazana mchana huu nje ya nyumba aliyokuwa anaishi marehemu Steven Charles Kanumba, aliyefariki usiku wa kuamkia leo.
    Nyumba hiyo ipo eneo la Sinza, mkabala kabisa na hoteli maarufu ya Vatican. Pande zote mbili za barabara inayotokea Sinza Kijiweni kuelekea Tandale Uzuri watu wamejazana.
    Misururu ya watu imeanzia kwenye hoteli ya Deluxe, Sinza na wengine ambao wameamua kujiweka kwenye baa zilizo jirani na eneo hilo ili mradi washiriki kwa namna yoyote.
    Nyumba zilizo jirani na nyumba aliyokuwa akiishi The Great Kanumba watu wamepanda juu ya kuta kuchungulia ndani ya nyumba ya staa huyo, nini kinaendelea.
    Yote haya yanaashiria ni kiasi gani Steven Kanumba alikuwa kipenzi cha wapenzi wa filamu nchini. Kipenzi cha Watanzania.
    Vilio, manung’uniko, sura za majonzi na simanzi, vyote vimetawala eneo la tukio. Hakika ni majonzi makubwa- na hata baadhi ya wanaume wanashindwa kujizuia. Wanalia. “Kanumba, Kanumba, why Lulu?” alisikika dada mmoja akisema huku analia, karibu kabisa na geti la nyumba aliyokuwa akiishi marehemu.
    Ndani ya nyumba hiyo, watu hawaingii tena. Kumejaa. Getini kuna ulinzi mkali na idadi ya watu waliojazana getini ni sawa ile misururu ya kuingia kwenye mechi kubwa Uwanja wa Taifa.
    Maoni ya watu ni kwamba, eneo ambalo watu wamekusanyika kwa sasa ili kuomboleza msiba huo halitoshi na wanapendekeza msiba huo upewe hadhi ya kitaifa kwa kupelekwa kwenye maeneo ya wazi.

    KIFO CHAKE:
    Kanumba
    Kanumba alifariki dunia ghafla usiku wa kuamkia leo na chanzo cha kifo chake inaelezwa ni kugombana na mpenzi wake, mwigizaji mwenzake, Lulu.
    “Alikuwa anagombana na Lulu. Lulu akamsukuma Kanumba, akaangukia kichwa, ndio akafa, ilikuwa saa tisa usiku,” kilisema chanzo.
    Habari zaidi zinasema, wivu ndio chanzo cha ugomvi wao.
    Inaelezwa Lulu alikuwa anazungumza na simu na Kanumba akataka kujua anaongea na nani.
    Lulu hakutaka kumpa simu Kanumba na ndipo wakaanza kuvutana na mwenzake akadondoka chini.
    Inaelezwa alidondokea kisogo katika eneo gumu na ndipo hali ikawa mbaya kabla ya kifo chake.  

    MWILI WA KANUMBA:
    Waombolezaji
    Kwa sasa mwili wa mwigizaji huyo wa picha la Big Daddy upo katika vyumba vya kuhifadhia maiti, Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Dar es Salaam.
    Mwili huo ulichukuliwa mara tu baada ya tukio lililosababisha kifo chake.
    Kanumba ambaye filamu yake ya mwisho kuingia sokoni ni Tambua Haki, inayoendelea kuuzwa hivi sasa, imeelezwa kwamba Lulu ndio chanzo cha kifo chake.
     Ndugu wa Kanumba ambaye alikuwa akiishi naye Sinza, jijini Dar es Salaam na wakati mauti yanamkuta- na aliyekuwapo nyumbani amethibitisha hayo alipohojiwa na waandishi wa habari.
    Ndugu huyo amekaririwa akisema Lulu ambaye jina lake halisi ni Elizabeth Michael, alikuja nyumbani kwa Kanumba na kumkuta yeye (ndugu) amekaa na marehemu usiku.
    Ndugu huyo anasema aliwaachia faragha wawili hao wazungumze, lakini baada ya muda akasikia malumbano na yalipozidi wakahamia chumbani, ambako waliendelea kugombana.
    Anasema baada ya muda, Lulu alitoka chumbani akipiga kelele huku akimuita yeye (ndugu).
    Anasema alipotokea, Lulu akasema Kanumba ameanguka chumbani na povu linamtoka mdomoni.
    Ndugu huyo anasema alipokwenda chumbani, kweli alikuta hali hiyo, akaenda kumuita daktari.
    Anasema aliporejea na daktari, katika hali ya kushangaza, akakuta Lulu amekwishatoweka, ndipo wakachukua mwili wa marehemu na kuupeleka Muhimbili.

    LULU YUKO WAPI? 
    Kimwana Lulu
    Tayari Lulu amekwishakamatwa na Polisi na amehifadhiwa Kituo cha Oysterbay, Dar es Salaam.
    Chanzo cha habari kinasema Lulu amechanganyikiwa na tangu ahakikishiwe kwamba Kanumba amefariki dunia, hajitambui.
    Bado ni kizungumkuti juu ya hatima ya Lulu na kifo cha Kanumba na ni taarifa ya Polisi pekee itakayoondoa utata kuhusu tukio zima hilo.
    Ingawa siri ya mapenzi yao inafichuka baada ya kifo cha mwenzake, lakini Lulu katika mahojiano mbalimbali ambayo amekuwa akifanyiwa amekuwa akikakana kuwepo uhusiano wa aina yoyote kati yake na marehemu Steve.

    MSIBA, MAZISHI:
    Ndani kwa Kanumba
    Bado pamoja na mvua kunyesha, eneo dogo, lakini bado watu wanakusanyika Sinza.
    Ndani ya nyumba waliobahatika kuingia kwa wingi ni wasanii mastaa haswa, na watu wa karibu, lakini wengine wamekwama nje.
    Kulingana na umaarufu wa Kanumba katika jamii, familia ya marehemu italazimika kushirikiana na serikali kupitia vitengo husika kama BASATA katika kuratibu mazishi ya nyota huyo aliyekuwa na kipaji kikubwa cha uigizaji.
    Ni moja kati ya mawili, Kanumba atasafirishwa Shinyanga au atazikwa hapa hapa Dar es Salaam. bongostaz inaendelea kufuatilia kwa karibu na itaendelea kukupasha kila kitakachojiri.  

    HISTORIA YAKE:
    Steven Charles Kanumba alizaliwa Januari 8, mwaka 1984, mkoani Shinyanga, kabla ya umauti kumfika Aprili 6, mwaka 2012.
    Elimu ya msingi alipata katika shule ya Bugoyi, Shinyanga na baadaye akajiunga na sekondari ya Mwadui, kabla ya kuhamia Dar Christian Seminary.
    Baada ya kumaliza Kidato cha Nne Dar Christian, Kanumba alijiunga na sekondari ya Jitegemee, Dar es Salaam pia kwa elimu ya Kidato cha Tano na Sita.
    Ni wakati huo akiwa Jitegemee, Kanumba alianza shughuli za sanaa katika Kundi la Kaole Sanaa Group la Magomeni, Dar es Salaam.
    Baada ya kukomaa Kaole, Kanumba aliamua kuanzisha kampuni yake mwenyewe ya filamu na hadi anakutwa na umauti alikuwa mwigizaji anayefahamika Afrika nzima.
    Ameshirikiana na wasanii wakubwa duniani kama Ramsey Nouah wa Nigeria na amefanya kazi na mastaa wengine kadhaa wa Nigeria.
    Miongoni mwa filamu ambazo alifanya ni Dar To Lagos, She is My Sister, Ancle JJ, Oprah, Tufani, Johari, Gharika, Baragumu, Sikitiko Langu, Dangerous Desire, Cross My Sin, Village Pastor, Family Tears na kadhalika.
    Hivi karibuni, alikaririwa akisema atagombea Ubunge katika uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2015.
    Kanumba atakumbukwa na wengi sana kwa ucheshi wake- upole na ushirikiano mzuri na wenzake katika kazi.
    Kifo cha Kanumba ni pigo katika tasniya ya filamu Tanzania. Taifa limempoteza mtu ambaye alikwishaanza kuitangaza vema nchi kupitia sanaa hiyo na ambaye angetarajiwa kuitangaza zaidi katika anga za kimataifa zaidi kupitia sanaa hii.
    Nigeria sasa wanajua Tanzania kuna filamu. Nchi nyingi za Afrika zinajua sasa na hii sehemu ya kazi nzuri ya Kanumba.
    Mwenyewe aliwahi kukaririwa alifika hadi Hollywood, Marekani, ambayo ni ‘makka’ ya wacheza filamu. Kwa sasa mwili wa marehemu upo katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Dar es Salaam.
    Mungu aiweke pema peponi roho ya marehemu. Amin.
    • Blogger Comments
    • Facebook Comments

    1 comments:

    Mzungu said... April 7, 2012 at 11:35 PM

    Kwa level ya Kanumba angetakiwa kuwa na manager wake wa kumshauri katika tyaaluma yake na hata mahusiano. Wenzetu walioendelea wanaamini kuwa ni hatari sana kuwa na mahusianoi na watu ambao una act nao. Yaliyomkuta kanumba sio mageni sana bali ni ugumu wa kuelewa kuwa taaluma yako na mapenzi na wale wale unaoigiza mao ni HATARI SANA..... MUNGU AMLAZE MAHALI PEMA PEPONI!

    Item Reviewed: LULU TAABANI POLISI, MAMIA WAFURIKA NYUMBANI KWA KANUMBA Rating: 5 Reviewed By: Mahmoud Bin Zubeiry
    Scroll to Top