Ndugu wa Kanumba akizungumza na Waandishi |
MVUA inanyesha, lakini mamia ya
watu wamejazana mchana huu nje ya nyumba aliyokuwa anaishi marehemu Steven Charles
Kanumba, aliyefariki usiku wa kuamkia leo.
Nyumba hiyo ipo eneo la Sinza,
mkabala kabisa na hoteli maarufu ya Vatican. Pande zote mbili za barabara
inayotokea Sinza Kijiweni kuelekea Tandale Uzuri watu wamejazana.
Misururu ya watu imeanzia kwenye
hoteli ya Deluxe, Sinza na wengine ambao wameamua kujiweka kwenye baa zilizo
jirani na eneo hilo ili mradi washiriki kwa namna yoyote.
Nyumba zilizo jirani na nyumba aliyokuwa
akiishi The Great Kanumba watu wamepanda juu ya kuta kuchungulia ndani ya
nyumba ya staa huyo, nini kinaendelea.
Yote haya yanaashiria ni kiasi
gani Steven Kanumba alikuwa kipenzi cha wapenzi wa filamu nchini. Kipenzi cha
Watanzania.
Vilio, manung’uniko, sura za
majonzi na simanzi, vyote vimetawala eneo la tukio. Hakika ni majonzi makubwa-
na hata baadhi ya wanaume wanashindwa kujizuia. Wanalia. “Kanumba, Kanumba, why
Lulu?” alisikika dada mmoja akisema huku analia, karibu kabisa na geti la
nyumba aliyokuwa akiishi marehemu.
Ndani ya nyumba hiyo, watu
hawaingii tena. Kumejaa. Getini kuna ulinzi mkali na idadi ya watu waliojazana
getini ni sawa ile misururu ya kuingia kwenye mechi kubwa Uwanja wa Taifa.
Maoni ya watu ni kwamba, eneo ambalo
watu wamekusanyika kwa sasa ili kuomboleza msiba huo halitoshi na wanapendekeza
msiba huo upewe hadhi ya kitaifa kwa kupelekwa kwenye maeneo ya wazi.
KIFO CHAKE:
Kanumba |
Kanumba alifariki dunia ghafla usiku
wa kuamkia leo na chanzo cha kifo chake inaelezwa ni kugombana na mpenzi wake,
mwigizaji mwenzake, Lulu.
“Alikuwa anagombana na Lulu.
Lulu akamsukuma Kanumba, akaangukia kichwa, ndio akafa, ilikuwa saa tisa
usiku,” kilisema chanzo.
Habari zaidi zinasema, wivu ndio
chanzo cha ugomvi wao.
Inaelezwa Lulu alikuwa anazungumza
na simu na Kanumba akataka kujua anaongea na nani.
Lulu hakutaka kumpa simu Kanumba
na ndipo wakaanza kuvutana na mwenzake akadondoka chini.
Inaelezwa alidondokea kisogo
katika eneo gumu na ndipo hali ikawa mbaya kabla ya kifo chake.
MWILI WA KANUMBA:
Waombolezaji |
Kwa sasa mwili wa mwigizaji huyo
wa picha la Big Daddy upo katika vyumba vya kuhifadhia maiti, Hospitali ya
Taifa ya Muhimbili, Dar es Salaam.
Mwili huo ulichukuliwa mara tu
baada ya tukio lililosababisha kifo chake.
Kanumba ambaye filamu yake ya
mwisho kuingia sokoni ni Tambua Haki, inayoendelea kuuzwa hivi sasa, imeelezwa kwamba
Lulu ndio chanzo cha kifo chake.
Ndugu wa Kanumba ambaye alikuwa akiishi naye
Sinza, jijini Dar es Salaam na wakati mauti yanamkuta- na aliyekuwapo nyumbani
amethibitisha hayo alipohojiwa na waandishi wa habari.
Ndugu huyo amekaririwa akisema Lulu
ambaye jina lake halisi ni Elizabeth Michael, alikuja nyumbani kwa Kanumba na
kumkuta yeye (ndugu) amekaa na marehemu usiku.
Ndugu huyo anasema aliwaachia faragha
wawili hao wazungumze, lakini baada ya muda akasikia malumbano na yalipozidi
wakahamia chumbani, ambako waliendelea kugombana.
Anasema baada ya muda, Lulu alitoka
chumbani akipiga kelele huku akimuita yeye (ndugu).
Anasema alipotokea, Lulu akasema
Kanumba ameanguka chumbani na povu linamtoka mdomoni.
Ndugu huyo anasema alipokwenda
chumbani, kweli alikuta hali hiyo, akaenda kumuita daktari.
Anasema aliporejea na daktari, katika
hali ya kushangaza, akakuta Lulu amekwishatoweka, ndipo wakachukua mwili wa
marehemu na kuupeleka Muhimbili.
LULU YUKO WAPI?
Kimwana Lulu |
Tayari Lulu amekwishakamatwa na
Polisi na amehifadhiwa Kituo cha Oysterbay, Dar es Salaam.
Chanzo cha habari kinasema Lulu
amechanganyikiwa na tangu ahakikishiwe kwamba Kanumba amefariki dunia,
hajitambui.
Bado ni kizungumkuti juu ya
hatima ya Lulu na kifo cha Kanumba na ni taarifa ya Polisi pekee itakayoondoa
utata kuhusu tukio zima hilo.
Ingawa siri ya mapenzi yao inafichuka
baada ya kifo cha mwenzake, lakini Lulu katika mahojiano mbalimbali ambayo
amekuwa akifanyiwa amekuwa akikakana kuwepo uhusiano wa aina yoyote kati yake
na marehemu Steve.
MSIBA, MAZISHI:
Ndani kwa Kanumba |
Bado pamoja na mvua kunyesha,
eneo dogo, lakini bado watu wanakusanyika Sinza.
Ndani ya nyumba waliobahatika
kuingia kwa wingi ni wasanii mastaa haswa, na watu wa karibu, lakini wengine
wamekwama nje.
Kulingana na umaarufu wa Kanumba
katika jamii, familia ya marehemu italazimika kushirikiana na serikali kupitia
vitengo husika kama BASATA katika kuratibu mazishi ya nyota huyo aliyekuwa na
kipaji kikubwa cha uigizaji.
Ni moja kati ya mawili, Kanumba
atasafirishwa Shinyanga au atazikwa hapa hapa Dar es Salaam. bongostaz inaendelea
kufuatilia kwa karibu na itaendelea kukupasha kila kitakachojiri.
HISTORIA YAKE:
Steven Charles Kanumba alizaliwa
Januari 8, mwaka 1984, mkoani Shinyanga, kabla ya umauti kumfika Aprili 6,
mwaka 2012.
Elimu ya msingi alipata katika
shule ya Bugoyi, Shinyanga na baadaye akajiunga na sekondari ya Mwadui, kabla
ya kuhamia Dar Christian Seminary.
Baada ya kumaliza Kidato cha Nne
Dar Christian, Kanumba alijiunga na sekondari ya Jitegemee, Dar es Salaam pia
kwa elimu ya Kidato cha Tano na Sita.
Ni wakati huo akiwa Jitegemee,
Kanumba alianza shughuli za sanaa katika Kundi la Kaole Sanaa Group la
Magomeni, Dar es Salaam.
Baada ya kukomaa Kaole, Kanumba
aliamua kuanzisha kampuni yake mwenyewe ya filamu na hadi anakutwa na umauti
alikuwa mwigizaji anayefahamika Afrika nzima.
Ameshirikiana na wasanii wakubwa
duniani kama Ramsey Nouah wa Nigeria na amefanya kazi na mastaa wengine kadhaa
wa Nigeria.
Miongoni mwa filamu ambazo
alifanya ni Dar To Lagos, She is My Sister, Ancle JJ, Oprah, Tufani, Johari,
Gharika, Baragumu, Sikitiko Langu, Dangerous Desire, Cross My Sin, Village
Pastor, Family Tears na kadhalika.
Hivi karibuni, alikaririwa
akisema atagombea Ubunge katika uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2015.
Kanumba atakumbukwa na wengi
sana kwa ucheshi wake- upole na ushirikiano mzuri na wenzake katika kazi.
Kifo cha Kanumba ni pigo katika
tasniya ya filamu Tanzania. Taifa limempoteza mtu ambaye alikwishaanza
kuitangaza vema nchi kupitia sanaa hiyo na ambaye angetarajiwa kuitangaza zaidi
katika anga za kimataifa zaidi kupitia sanaa hii.
Nigeria sasa wanajua Tanzania kuna
filamu. Nchi nyingi za Afrika zinajua sasa na hii sehemu ya kazi nzuri ya
Kanumba.
Mwenyewe aliwahi kukaririwa
alifika hadi Hollywood, Marekani, ambayo ni ‘makka’ ya wacheza filamu. Kwa sasa
mwili wa marehemu upo katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Dar es Salaam.
Mungu aiweke pema peponi roho ya
marehemu. Amin.
1 comments:
Kwa level ya Kanumba angetakiwa kuwa na manager wake wa kumshauri katika tyaaluma yake na hata mahusiano. Wenzetu walioendelea wanaamini kuwa ni hatari sana kuwa na mahusianoi na watu ambao una act nao. Yaliyomkuta kanumba sio mageni sana bali ni ugumu wa kuelewa kuwa taaluma yako na mapenzi na wale wale unaoigiza mao ni HATARI SANA..... MUNGU AMLAZE MAHALI PEMA PEPONI!
Post a Comment