Lulu akitoka mahakamni na kurudishwa mahabusu gereza la Segerea |
MWIGIZAJI nyota wa filamu Tanzania, Elizabeth Michael ‘Lulu’
leo amewatoa machozi baadhi ya watu waliohudhuria kesi yake katika Mahakama ya Hakimu
Mkazi, Kisutu, Dar es Salaam.
Lulu mwenye umri wa miaka 17, anayekabiliwa na kesi ya
mauaji ya mwigizaji mwenzake, Steven Charles Kanumba, aliwasikitisha watu na
baadhi kumwaga machozi, kutokana na jinsi alivyowasili Mahakamani hapo akiwa chini
ya ulinzi mkali wa askari Magereza.
“Masikini biti anapata matatizo sasa, inatia huruma,
nawaonea huruma wazazi wake, wanakosa raha sasa,”alisikika mtu mmoja akisema mahakamani
hapo.
Pamoja na kufikishwa mahakamani hapo,
Hakimu Mkazi wa Mahakama Kisutu, Ritha Tarimo aliahirisha
kesi hiyo hadi Mei 7, mwaka kwa sababu upelelezi bado unaendelea.
Lulu anayekabiliwa na tuhuma za kumuua The Great Kanumba
aliyefariki dunia, Aprili 7, mwaka huu nyumbani kwake Vatican, Sinza Dar es
Salaam, hii ni mara ya pili kufikishwa mahakamani hapo.
Lulu aliyecheza filamu kadhaa na marehemu Kanumba waliyeibuka
naye katika kundi la Kaole, Magomeni, hakutakiwa kutoa maelezo yoyote
Mahakamani, kwa kuwa Mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi za mauaji.
Wakati kesi hiyo ikiwa katika hatua za mwanzoni, Polisi bado
inaendelea na uchunguzi wake na baadhi ya watu wakiwemo wasanii wamekuwa
wakihojiwa kulisaidia jeshi hilo upelelezi.
Taarifa za awali baada ya kifo cha Kanumba, zilisema kwamba
mwigizaji huyo alifariki baada ya kusukumwa na Lulu nyumbani kwake Sinza Vatican,
ambaye inadaiwa alikuwa mpenzi wake.
Inaelezwa baada ya tukio hilo, Lulu alikimbia nyumbani kwa
Kanumba na mdogo wa Ther Great, Sethi Bosco akaenda kuchukua gari kumpeleka
kaka yake hospitali ya Muhimbili, ambako alipofika iligundulika amekwishafariki
dunia.
Sethi alikaririwa akisema kwamba siku ya tukio, Lulu alikwenda
kwao usiku wa manane na alipofika yeye (Sethi) alimuacha aongee na kaka yake. Sethi
alidai aliwaacha sebuleni akaingia chumbani kwake na baadaye akasikia wameingia
chumbani (kwa Kanumba).
Sethi alisema baada ya muda alisikia kelele za dalili ya
ugomvi na baada ya muda Lulu alitoka kumwambia (Sethi) juu ya hali ya Kanumba
kubadilika na kuwa mbaya.
Sethi alidai aliposikia hivyo akashituka na kwenda chumbani ambako
alimkuta kaka yake katika hali mbaya, povu likimtoka mdomoni hivyo kuchukua
hatua ya kumuita daktari wake, kabla ya kumkimbiza Muhimbili.
Lulu alikamatwa asubuhi ya kuamkia siku ya tukio hilo, linalodaiwa
kutokea usiku wa manane na kuwekwa kizuizini katika kituo cha Polisi Oysterbay,
Kinondoni, Dar es Salaam.
Tayari baadhi ya wanaharakati wa haki za wanawake
wamekwishatangaza azma yao ya kumsaidia Lulu katika kesi hii.
Miongoni mwao ni Mbunge wa Jimbo la Kawe, (CHADEMA), Halima
Mdee.
Bado watu wanajiuliza maswali mengi kuhusu kifo cha Kanumba,
mojawapo kama kweli Lulu anayedaiwa kumuuwa wakati wakigombana ‘ana ubavu’ huo.
Lakini pia, siku ya kifo cha Kanumba, inadaiwa alionekana
katika ukumbi wa starehe, Club Maisha akinywa pombe.
Uchunguzi wa madaktari katika hospitali ya Rufaa ya Muhimbili
ulisema pombe kali aina ya Jackie Daniels ilisababisha kifo cha mwigizaji huyo.
Lakini baadhi ya vielelezo vilipelekwa kwa mkemia mkuu wa
serikali, ili kutaka kujua kama msanii huyo aliwekewa sumu.
Kifo cha Kanumba kimewaumiza wengi, kwani msanii huyo
alikuwa mahiri na kipenzi cha wapenzi wa filamu nchini.
Wapembuzi wa mambo wanasema huu ni msiba wa kwanza kuteka
hisia za watu wengi zaidi, tangu kifo cha baba wa taifa, Mwalimu Julius
Kambarage Nyerere Oktoba mwaka 1999.
0 comments:
Post a Comment