Muuwaji Cisse |
MABAO mawili ya mshambuliaji wa kimataifa wa Senegal, Papiss
Demba Cisse yalitosha kuipa Newcastle ushindi wa 2-0 dhidi ya Liverpool jioni
hii, ambayo ilimaliza na wachezaji 10, hivyo kuzidi kujiimarisha katika kuwania
kwake nafasi ya kucheza michuano ya Ulaya msimu ujao.
Msenegali aliyejiunga na Newcastle Januari mwaka huu akitokea
Freiburg ya Ujerumani, sasa ametimiza mabao saba katika mechi saba alizocheza
kwa mabao yake hayo ya dakika za 19 na 59 kwenye Uwanja wa St. James’ Park.
Ushindi wa Newcastle unawafanya walingane kwa pointi na Chelsea
inayoshika nafasi ya tano na kupunguza idadi ya pointi wanazozidiwa na Arsenal inayoshika
nafasi ya tatu hadi kubaki tano zikiwa zimebaki mechi saba za kumalizia msimu.
Katika mchezo huo, Liverpool ilimpoteza kipa wake Jose Reina
dakika za mwishoni aliyelimwa kadi nyekundu baada ya kumpiga kichwa beki wa Newcastle,
James Perch.
Kipa huyo wa kimataifa wa Hispania, sasa atakosa mechi tatu
ikiwemo Nusu Fainali ya Kombe la FA dhidi ya wapinzani wao wa Merseyside,
Everton kwenye Uwanja wa Wembley, Aprili 14.
0 comments:
Post a Comment