Wachezaji wa Azam FC, timu ambayo inaongoza mechi zake za Ligi Kuu kuvurugika |
KWA mara ya tatu katika kipindi cha miezi miwili, juzi refa
aliyechezesha mechi ya Azam FC katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara,
alikuwa chanzo cha matatizo mchezoni.
Mtibwa waligomea mechi na kuondoka uwanjani wakiwa
wamefungana 1-1 na Azam FC, Uwanja wa Azam, Chamazi.
Msimu uliopita Mtibwa Sugar walifungwa nyumbani na Azam
mabao manne, hawakuleta tatizo, lakini juzi wakiwa wapo 1-1 wakaamua kugoma.
Waligoma baada ya kuchoshwa na maamuzi mabovu ya refa,
ikiwemo kuwapa penalti ambayo si halali wenyeji.
Hii ni mara ya tatu ndani ya miezi miwili, marefa
wanaochezesha mechi za Azam wanakuwa sababu ya kuvurugika kwa mchezo.
Wiki mbili zilizopita tu, refa aliyechezesha mechi kati ya Azam
FC na wenyeji Polisi Dodoma, Uwanja wa Jamhuri alipigwa na mashabiki baada ya
mechi.
Azam ilishinda 1-0, beo pekee la beki wake wa kati wa kimataifa
wa Tanzania, Aggrey Morris Ambroce dakika ya 83 katika mchezo wa Ligi Kuu ya
Vodacom Tanzania Bara dhidi ya wenyeji Polisi Dodoma.
Katika mchezo huo, Polisi Dodoma, ilipata pigo baada ya beki
wake, Bakari Omari kutolewa nje kwa kadi nyekundu, dakika ya 57 baada ya
kuonyeshwa kadi ya pili ya njano.
Refa wa mchezo huo
alipigwa na mashabiki kwa madai ya kuwapendelea Azam, baada ya mpambano
kukamilika, lakini askari walifanikiwa kumuokoa asipokee kipondo zaidi.
Awali, mwezi uliopita, refa aliyechezesha mechi kati ya
Yanga na Azam, Israel Nkongo alipigwa na Stefano Mwasyika na angeweza kupigwa
pia na mashabiki wa Yanga.
Kwa nini apigwe? Kisa kutuhumiwa kuipendelea Azam. Mechi
zinazochezwa kwenye Uwanja wao, timu nyingi zimekuwa zikilalamika Azam inabebwa.
Kwa muda mrefu wapenzi wa soka Tanzania wamekuwa
wakilalamikia desturi ya klabu kongwe nchini Simba na Yanga kutamba nyumbani,
kudaiwa kushinda kwa kununua mechi.
Hii inasababisha timu zetu zinakuwa dhaifu kwenye michuano
mikubwa na ndiyo maana zinashindwa japo kucheza hatua ya makundi tu ya michuano
ya Afrika.
Watu wanataka timu ishinde kwa uwezo, ili idhihirishe ubora
ambao utakwenda kuifanya ishiriki vyema michuano ya Afrika.
Kwa sababu hiyo, ujio wa Azam FC timu inayomilikiwa na
Milionea Said Salim Bakhresa ulipokewa kwa furaha na wadau wa soka nchini,
wakijua amepatikana mkombozi wa kweli.
Azam imewekeza fedha nyingi kuanzia kwenye usajili, ajira za
makocha, Uwanja wake kule Chamazi- na kwa ujumla ni timu ambayo ukiangalia
inapoelekea unajenga matumaini.
Azam haina wanachama wa kuleta mizengwe ya kuvuruga timu,
wanaweza kujivuruga wao kwa wao tu.
Mchezaji wa Azam hachezi kwa presha ya kutukanwa na
mashabiki akikosea kama mchezaji wa Yanga au Simba. Azam imesajili wachezaji
nyota kuanzia ndani na nje ya nchi.
Azam inaongoza kutumia fedha nyingi na kusajili wachezaji
bora nchini. Hivyo timu hii inastahili kuwa bingwa wa nchi kulingana na jinsi
ilivyowekeza.
Lakini wasiwasi ni kwamba, mechi zao zinatiliwa shaka sasa
nao kama wanatumia mbinu chafu ikiwemo kuhonga marefa ili kushinda.
Kama kweli watakuwa wanafanya hivyo, ina maana watakuwa
wanaiga Simba na Yanga, ambazo kimsingi zinanyooshewa kidole kwa kudumaza
maendeleo ya soka ya nchi hii.
Kama Azam wanaiga Simba na Yanga kununua mechi, wanaweza
wakafanikiwa kuwa mabingwa, lakini swali la kujiuliza soka ya Tanzania itakuwa
kweli imepata mkombozi?
Napata shaka sana juu ya mustakabali wa soka ya nchi hii,
ikiwa Azam nayo inakuja kwa staili hii- dhahiri
bado tuna kazi ngumu na safari ndefu kufikia japo karibu na mafanikio.
Kwa sababu mchezaji akishajua kwamba kuna unafuu katika
mchezo kutokana na mabosi wao kuhonga, hawezi kujituma tena kwa sababu anajua
ushindi upo tu.
Mwaka 2007, baada ya Yanga kutolewa katika Ligi ya Mabingwa
Afrika na Esperance ya Tunisia, aliyekuwa kipa wa timu hiyo, Ivo Mapunda
aliwashauri viongozi wa klabu yake wakati huo, wawe wanafanya mipango na marefa
kurahisisisha mechi.
Tayari mchezaji kujenga dhana hiyo- inamaanisha amefikia
mwisho wa uwezo wake, wakati suluhisho ni kufanyia kazi mapungufu ili wakati
mwingine ufanye vizuri.
Mwaka juzi, Simba ilifungwa 5-0 na Haras El Hodood nchini
Misri katika mchezo wa Kombe la Shirikisho,
mwaka jana ilifungwa 3-0 na Wydad Cassablanca, mara zote ikitolewa
katika michuano ya Afrika.
Mwaka huu, imefungwa 3-1 ikitoka kushinda 2-0 nyumbani na ES
Setif moja ya timu tishio tu Afrika na kuingia hatua ya 16 Bora ya Kombe la
Shirikisho.
Hii nini maana yake? Simba imefanyia kazi mapungufu kutoka
kufungwa 5-0, 3-0 na 3-1 sambamba na kusonga mbele.
Lakini desturi ya kutaka kurahisisisha kazi kwa kununua
mechi- maana yake hatuwezi kufanyia kazi mapungufu.
Kweli wapenzi wa soka Tanzania wanaitegemea Azam iijengee
heshima nchi hii katika michuano ya Afrika, lakini kwa staili ambayo wanataka
kwenda nayo. Hakuna hakika kama watafanikiwa.
Yapo maneno tayari yanasemwa semwa kuhusu Azam na harakati
zao za ubingwa na mbinu wanazodaiwa kutumia hadi watu wanaodaiwa kutumiwa
kutoka kwenye mamlaka husika- japo kwa sasa tunayachukuliwa kama maneno ya
mtaani tu, lakini ipo haja ya kuiangalia Azam kwa jicho la tatu.
Haina maana Yanga kukosekana michuano ya Afrika mwakani,
wakati ilipigana kwa uwezo wake na kuzidiwa na timu ambayo ushindi wake
ulitokana na mbeleko za marefa.
Namna hii hata mtu huwezi kustaajabu kwa nini John Bocco
mabao yake anafunga Azam tu na timu ya taifa anabaki yeye na kipa mara kibao
anashindwa. Akizomewa eti anasusa.
Watu hawataki kujadili ukweli wa kiini cha tatizo, kwa
sababu tayari kuna kosa lilitendeka- lakini hawajui kwamba hata kosa lina sababu.
Jasiri yoyote hakubali kudhulumiwa haki yake bana-
tusidanganyane na wala watu wasitake kujiona wao miungu watu katika dunia hii-
misingi ya haki ni ile ile.
Kila jina zuri lina jina mbadala la uasi- watu wakikupenda
kwa ujasiri wako wa kutopenda kuonewa kiasi cha kuwa tayari kupambana na yeyote
kutetea haki, watakuita jasiri, shujaa, shupavu.
Lakini kwa sababu hizo hizo, wakiwa hawakupendi watakuita
mkorofi- mgomvi, huelewani na watu- hiyo ndio dunia yetu ya leo- dunia tofauti
na ile waliyoishi akina Mtemi Mirambo, Chifu Mkwawa na Adolph Hitler.
Mtibwa walikuwa wastaarabu wakaondoka uwanjani- hawajui
mbali na kupoteza pointi tatu, watatozwa faini na sijui kanuni zinasemaje
zaidi, ili kuna hatari ya kufungiwa pia kucheza ligi.
Wachezaji wa Yanga waliona bora kumtandika Nkongo- hawakujua
mbele yake kuna kufungiwa kucheza na kuigharimu zaidi klabu yao.
Lakini chanzo cha yote haya ni nini? Azam hao. Wanafanya
nini, sijui na sina ushahidi kama wanahonga marefa na siwezi kusema wanahonga
marefa, ila naweza kujiuliza kwa nini wawe wao tu? Mara moja bahati mbaya-
lakini sasa mara ya tatu jamani, timu hiyo hiyo moja! Hapana bwana!
0 comments:
Post a Comment