Diamond |
MWANZONI mwa miaka ya 1990, Hamis Thobias Gaga Gagarino angeingia katika Ukumbi wa DDC Kariakoo jijini Dar es Salaam akiyumba.
Katika mfuko wake wa jeans wa nyuma kulikuwa kuna chupa ya kilaji. Nywele zake hajachana. Na kila mtu ana furaha kumuona Hamis.
Jukwaani, Shaaban Dede wakati huo anaimba nyimbo zake. Kando yake yupo Hassan Rehani Bitchuka. Gaga anazungukwa na umati wa watu kwa sababu ni kivutio. Akiwa ameitibua akili yake kwa kilaji, Gaga anayumba huku akicheza kwa maringo.
Unajua kwa nini anavutia watu? Kwa sababu jioni yake, Gaga alikuwepo Uwanja wa Taifa akiyumba. Muda huo alikuwa hayumbi kwa kinywaji kichwani. Alikuwa anayumba kwa soka maridadi.
Utasema nini kuhusu Gaga? Katika jezi ya Wekundu wa Msimbazi alikuwa hakamatiki. Alikuwa na ubongo wenye akili, chenga maridadi, mashuti makali, pasi za mwisho na mabao ya kusisimua.
Jioni hiyo wakati Gaga akisisimua watu, Dede na Bitchuka wanakuwa wapo jukwaani wakimtazama Gaga.
Wanamuziki hawa wawili ni Simba wa kutupwa na hapana shaka Gaga alikuwa anakonga mioyo yao. Mwishowe kabisa walikuwa wanabadilishana starehe na umaarufu. Baada ya Gaga kuwaburudisha pale Taifa, usiku wao wangemburudisha Gaga pale DDC Kariakoo.
Kwa sasa Gaga ni marehemu. Amepumzika katika makaburi ya Kola yaliyopo nje kidogo ya Mji wa Morogoro. Mungu amlaze mahali pema Hamis Gaga. wengine tulimuita Hamis Maringo.
Miaka mingi sasa imepita na mambo yamebadilika. Hamis, Dede na Bitchuka si matajiri. Wakati huo walipokuwa wanabadilishana starehe, kijana anayeitwa Nassib Abdul maarufu kama Diamond the Platinum alikuwa mdogo sana wa miaka miwili tu.
Wiki chache zilizopita, Diamond alifanya onyesho lake binafsi katika Ukumbi wa Mlimani City. Kiingilio kilikuwa shilingi 50,000 kwa kila kichwa kilichoingia.
Ukumbi ulijaza watu zaidi ya 500. Alisimama jukwaani peke yake kwa muda wa saa tatu na ushee na kuweka historia.
Ukipiga hesabu ya jumla makusanyo yataonyesha pesa nyingi. Jaribu kuweka kando kila makato inasemekana Diamond aliweka mfukoni shilingi milioni tano za Kitanzania. Jina lake liko juu.
Lakini si yeye tu. Wanamuziki wengi wa kizazi kipya mifuko yao imetuna. Unajua kwa nini? Muziki wao umewekwa katika mzunguko mwingine wa maisha. Kilichonikumbusha maisha ya Gaga na Dede ni ukweli kwamba walikuwa wanazunguka katika njia moja ya maisha.
Jioni Dede angeweza kumtazama Gaga. usiku Gaga angeweza kumtazama Dede. Umaarufu wao ulilingana. Kama jioni Gaga angefunga bao la kisigino kama alivyofanya siku ile dhidi ya Pamba ya Mwanza, basi jioni Dede angeachia kibao kipya kwa ustadi.
Uzuri wake ni kwamba, hata maisha yao yalishabihiana. Kipato chao kilikuwa sawa. Gaga angetuzwa na mashabiki wa Simba, na Dede angetuzwa na mashabiki wa muziki wa DDC Mlimani Park.
Lakini leo, inachekesha kidogo. Baada ya wenzetu wa kizazi kipya kuufanya muziki wao upendwe, baada ya redio kuufanya muziki wao upendwe, baada ya magazeti kuufanya muziki wao upendwe, akina Diamond wanachezea pesa ya kutosha.
Hata hivyo, bado Diamond hawezi kubadilishana burudani na Juma Kaseja wala Jerry Tegete. Unajua kwa nini? Kwa sababu wakati watu wa muziki wameingia zama mpya, sisi wa soka tumezubaa.
Diamond anategemea zaidi redio, magazeti na televisheni. Tegete au Kaseja wanategemea zaidi klabu zao ziwe za kisasa ili wapate fedha nyingi katika mauzo ya jezi, skafu, na mapato mengine.
Kama klabu zao Simba na Yanga zingekuwa na usasa huu, ina maana leo wachezaji wake wangekuwa wanalipwa hadi shilingi milioni tano kwa mwezi. Nilikuwa Afrika Kusini mwezi mmoja uliopita na ukipita tu katika maduka yaliyopo Johannesburg, Pretoria, Durban na kwingineko kuona jinsi jezi za Kaizer Chiefs na Orlando Pirates zinavyouzwa kama njugu utagundua kwa nini akina Siphiwe Tshabalala ni matajiri.
Kasi ya watu wa muziki imetutoa kapa sisi watu wa soka. Kutoka Shaaban Dede mpaka Diamond wamefanikiwa kubadilika. Na wala si kwa muziki wa kizazi kipya tu. Leo hawa akina Nyoshi El Saadat, Charlz Baba, Ally Choki na wengineo wameufikisha muziki katika mapato.
Huku katika soka kuna soga kubwa la wanasiasa.
Hawajaendana na kasi hii. Ingawa wapo wanasoka walioambulia visenti katika miaka ya karibuni kama akina Kaseja, lakini bado hawako katika viwango vya akina Diamond. Hakuna anayeweza kuingiza shilingi milioni tano kwa saa tatu tu.
Mara kadhaa huwa nasafiri na wachezaji wa timu zetu. Huwa wanatembea na simu za kisasa zenye nyimbo kibao za akina Joe Makini, Diamond, FM Academia, Twanga na wengineo. Utasikia akina Kaseja wakiwasifia akina Diamond �Dah aisee huyu dogo anapiga pesa mbaya�. Kuna pengo kubwa wanaliona.
Sawa, mtu mmoja ana uwezo mkubwa wa kuingiza pesa kuliko kundi la watu. Na ndiyo maana Michael Jackson ni tajiri kuliko David Beckham. Lakini pengo lililopo baina ya wachezaji wetu ni kubwa sana mbele ya hawa akina Diamond.
Tasnia ya muziki Tanzania inakua kwa kasi wakati soka letu linadorora kwa kasi hiyo hiyo. Hata hivi vichwa vya habari tunavyovisoma kila siku kuhusu uhusiano wa Diamond na wapenzi wake vinatokana na jeuri yake ya pesa tu.
Bado naamini, kama kweli Yanga ina mashabiki milioni 10 nchini kote na ambao wangeweza kufikishiwa bidhaa za Yanga, au kuhusiana moja kwa moja na pato la Yanga kwa mwaka, leo Nsajigwa Shadrack angeweza kula sahani moja na Diamond katika suala la fedha na staili ya maisha anayoishi.
Watu wa muziki wametuzidi ujanja sisi watu wa soka. Na ndiyo maana mzunguko wa kubadilishana starehe na umaarufu kati ya Gaga na Dede umetoweka. Ni mchezaji gani anaweza kula sahani moja na Diamond kwa umaarufu na pesa?
GAZETI LA MWANASPOTI:
0 comments:
Post a Comment