Stramaccioni akimkumbatia Milito aliyepiga matatu |
KOCHA mpya wa Inter Milan, Andrea Stramaccioni ameanza kazi
vizuri baada ya kuiongoza timu hiyo kupata ushindi mnono wa mabao 5-4 dhidi ya
Genoa leo, Diego Milito akipiga mabao matatu peke yake katika mechi ambayo timu
zote zilimaliza pungufu ya mchezaji ya mmoja mmoja.
Kocha kijana wa umri wa miaka 36, Stramaccioni alitambulishwa
Jumatatu baada ya kutupiwa virago Claudio Ranieri kwa matokeo mabaya, Inter
ikishinda mechi moja tu katika mechi 10.
Wiki moja iliyopita, Stramaccioni aliiongoza timu ya vijana
ya Inter kuifunga Ajax katika fainali ya michuano ya NextGen Series, ambayo ni
sawa na Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa vijana chini ya umri wa miaka 19.
Kwa ushindi huo, Inter inaipindua Catania katika nafasi ya
saba, sasa ikizidiwa pointi 20 na vinara wa Serie A, AC Milan, ambayo jana
ilitoka sare ya 1-1 na Catania.
Milan inazidi pointi tano Juventus, ambayo baadaye leo
inavaana na Napoli katika fainali ya Kombe la Italia.
Mapema Roma iliitandika Novara 5-2 na kuweka hai matumaini
ya kushika nafasi ya tatu kuwania kucheza Ligi ya Mabingwa.
Roma ipo nafasi ya sita, ikizidiwa pointi tatu na Lazio
wanaoshika nafasi ya tatu, ambao walifungwa 3-1 na Parma jana.
Katika mechi nyingine, leo Bologna ilifungwa 3-1 na Palermo,
Cagliari iliifunga 2-0 Atalanta, Fiorentina ilifungwa 2-1 na Chievo Verona,
Lecce ilitoka 0-0 na Cesena na Siena ilishinda 1-0 dhidi ya Udinese.
0 comments:
Post a Comment