Waombolezaji |
BARABARA ya Mtaa aliokuwa
anaishi msanii maarufu wa kiume Tanzania, Steven Charles Kanumba aliyefariki
dunia usiku wa kuamkia leo imefungwa rasmi.
Barabara hiyo inayotokea Sinza
Kijiweni na kwenda Magomeni, ikipitia Tandale Uzuri- pia hutumiwa na watu
wanaokwenda Kijitonyoma, Kinondoni wakati mwingine huwa njia nzuri ya mkato kwa
madereva wengi wakati wa foleni hususana siku kama leo Jumamosi.
Nyumba anayoishi Kanumba imepakana
na hoteli maarufu ya Vatican, Sinza, Dar es Salaam.
Watu wanaoruhusiwa kuingia ndani
ni wasanii na wanamuziki tu na wadau kama Waandishi wa Habari na wafanyabishara
zinazohusiana na sanaa.
Bado umati ni mkubwa ndani na
nje ya nyumba na hilo ndilo limesababisha barabara hiyo kufungwa.
HALI YA USALAMA
Wakati usiku unaingia, tishio kubwa
ni usalama wa watu na mali zao na Kamati ya Mazishi chini ya Mwenyekiti wake,
Gabriel Mtitu imeanza kuhaha kuhakikisha ulinzi unaongezwa kwenye eneo hilo.
Kwa sasa walinzi waliopo ni
askari wawili wa usalama barabarani na Polisi wasiozidi wanne- zaidi ya hapo
kuna walinzi wa kampuni binafsi, Maninja ambao ni maarufu kusimama milangoni
kwenye kumbi za dansi.
Wakati dalili za vurugu kutoka
kwa ‘Masela wa Sinza’ zikijitokeza, Mjumbe wa Kamati ya Mazishi, Ruge Mutahaba
alionekana akijadiliana na Ofisa wa Jeshi la Polisi, Koba Kimanga juu ya
kuongeza ulinzi.
Koba, ambaye ni bondia mstaafu
wa ngumi za Ridhaa uzito wa juu nchini, alimshauri Ruge aagize askari wa kikosi
cha mbwa na kuongezewa askari ambao ameshauri waje na gari la doria.
UIGIZAJI UNAENDELEA
Penye wengi hapakosi wengi, kuna
vituko vya hapa na pale kwenye eneo la msiba.
Kikubwa ni waigizaji, watu wa
fani moja na marehemu Kanumba kuendeleza uigizaji wao eneo la tukio.
Kwa mfano mtu anatoka alipotoka
akiwa anafuraha anacheka na kurukaruka, lakini akiingia getini anajifanya ana
majonzi sana na hajiwezi, anaangua kilio au kujiangusaha haswa kwa waigizaji wa
kike.
Baadhi kwenye eneo hilo wameonekana
kuanza kuishitukia hali hiyo na akitokea ‘mtu kituko’ wa aina hiyo nao
wanaichukulia hiyo kama burudani na kuanza kucheka.
BADO WANAZIMIA
Lakini bado wapo wenye hisia za
kweli za majonzi ambao hakika wameshindwa kujimudu na kufikia hadi kuzimia.
Dada mmoja ambaye jina lake
halikupatikana, aliyeingia analia, alipofika karibu na eneo ambalo kuna picha
ya marehemu kwenye meza ya rambirambi, alianguka chini na kupoteza fahamu.
Zilipita dakika tano watu
hawajui cha kufanya juu yake, lakini baadaye ukatolewa ushauri amwagiwe maji
ndipo akafanikiwa kuzinduka.
WASANII NA KITU KIZITO
Ruge ambaye ni Mkurugenzi wa
Clouds Media Group, amefanya kikao na wasanii mbalimbali kuwashauri wafanye
kitu kizito kwa ajili ya kumuenzi msanii mwenzao huyo.
Ruge amewataka wasanii wenyewe
kuketi chini na kufikiria cha kufanya kama kazi ya pamoja au kila mmoja kazi
yake binafsi, lakini Jumanne siku ya kuuaga mwili wa marehemu kiwasilishwe
mbele ya umma kwenye viwanja vya Leaders.
Prodyuza Lamar amejitolea studuo
wasanii wakarekodi nyimno mbili na Diamond ameiambia bongostaz, yeye yupo
tayari kutia sauti kwa ajili ya Kanumba.
EAST COAST TEAM IMERUDI?
Majira ya saa 10 jioni, kwa
pamoja wasanii waliokuwa wakiunda kundi la East Coast Team lililokuwa na
maskani yake Upanga, Dar es Salaam waliingia kwa pamoja nyumbani kwa marehemu
na kusisimua watu.
Wakiongozwa na King Crazy GK,
wengine walikuwa ni Mwana FA, AY, Snare na Benja ambao maana yake wimbo wa Hii
Leo umekamilika na Ama Zao unaimbika.
Lakini ECT wote walionekana kutekwa
zaidi na msiba- hivyo hawakuwa tayari kuzungumzia mustakabali wao zaidi ya
kuiambia bongostaz wataingiza sauti kwenye wimbo kwa Lamar.
CHOKI BOSI WA DANSI BONGO:
Kwa moyo mkunjufu, Mkurugenzi wa
Kampuni ya African Stars Entertainment (ASET) Asha Ramadhani Baraka amemteua
Ally Choky, mwanamuziki wake wa zamani kwenye bendi ya Twanga Pepeta kuwa ‘bosi
wa wasanii wa dansi nchini’ katika suala la msiba wa Kanumba.
Asha ameiambia bongostaz kwamba
katika juu ya kitu gani watafanya wasanii wa dansi kwa ajili ya Kanumba, Choky
atashughulikia suala hilo na kitu kitakuwa tayari Jumanne wakati wa kuuaga
mwili wa marehemu.
KAMATI YA MAZISHI
Kamati ya Mazishi inaundwa na Mwenyekiti Gabriel Mtitu, Makamu
Mwenyekiti, Jacob Steven ‘JB’, Katibu, William Mtitu na Wajumbe Issa Mussa ‘Cloud’,
Kimosa, Vincent Kigosi ‘Ray’, Single Mtambalike ‘Richie’, Dilesh Solanki, Adele
Kanumba (dada wa marehemu), Hartman Mblinyi, Ruge, Ally Choky, Simon
Mwakifamba, Eric Shigongo, Steve Nyerere, Mahsein Awadh ‘Dk Cheni’ na Mama Nassor,
mmiliki wa nyumba aliyokuwa akiishi Kanumba.
Kamati hiyo Wajumbe wake
wanaonekana kufanya kazi nzuri, kuhakikisha wanamsitiri kwa hadhi yake ‘The Great
Steve Kanumba’.
0 comments:
Post a Comment