Kikosi cha Simba msimu huu |
JIONI hii Simba SC imeifunga Moro United mabao 2-0 katika
mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, na sasa inahita pointi moja tu katika
mechi zake tatu zilizobaki ili kutawazwa rasmi kuwa mabingwa.
Simba wanawavua ubingwa wapinzani wao wa jadi, Yanga SC
ambao msimu huu ‘wamefulia’ kiasi cha kukosa hata nafasi ya pili, ambayo
ingewawezesha kucheza michuano yua Afrika mwakani.
Ni ukweli usiopingika kwamba chachandu ya soka ya Tanzania
ni klabu mbili kongwe, Simba na Yanga, ambazo kwa sababu hiyo, zina mashabiki
lukuki nchini.
Maelfu ya Watanzania wanaweza kuziunga mkono timu za
majimboni mwao, wilayani mwao, mikoani mwao, lakini mwisho wa siku wanabakia
kuwa na timu ambazo zipo kwenye damu zao, Simba au Yanga.
Ni kwamba, Tanzania ina wapenzi wawili tu wa soka, mmoja ni
wa klabu ya Simba na mwingine wa Yanga. Hata wale ambao wamejijengea umaarufu
kama mashabiki wa timu fulani, mfano Yamungu aliyekuwa Reli Morogoro na
Mang'ombe aliyekuwa Pamba FC ya Mwanza, nao pia inadaiwa kuna timu waipendayo
miongoni mwa hizo.
Hakuna ubishi, Simba na Yanga ndiyo maana halisi ya soka
Tanzania.
Je, waijua vyema Simba SC?
Jezi za rangi nyekundu na nyeupe ndio utambulisho wao
dimbani, rangi ambayo inatumiwa na klabu nyingi kubwa za Ulaya, hususan
England, kama Liverpool, Manchester United na Arsenal.
Unapoizungumzia Simba, unamaanisha klabu kubwa Tanzania na
Afrika kwa ujumla, ambayo ilianzishwa mwaka 1936, enzi hizo ikijulikana kwa
jina la Queens, yaani Watoto wa Malkia.
Baadaye Simba ilibadilisha jina na kuwa Eagles, yaani ndege
aina ya Tai, kabla ya kuanza kutumia jina jingine, Sunderland, ambalo lilidumu
hadi mwaka 1971 lilipobadilishwa na kuwa Simba.
Wakati huo Sunderland ilikuwa ina matawi yake, ambayo
yalikuwa ni timu za Morning Stars, Canada Dry, Liverpool na Ilala Stuff, ambako
huko mchezaji aliyeonekana kukomaa alipelekwa kukipiga Sunderland.
Sababu ya kuachana na jina la Sunderland ni aliyekuwa Rais
wa Kwanza wa Zanzibar, Abeid Amaan Karume (sasa marehemu), ambaye wakati
anaweka jiwe la msingi kwa ajili ya ujenzi wa jengo la klabu hiyo, lililopo
Mtaa wa Msimbazi, mwaka huo 1971, alikemea tabia ya kupenda kuiga mambo ya
Waingereza, akiamini kufanya hivyo ni kuendelea kuutukuza ukoloni.
Rais Karume, aliwaambia Simba waachane na majina ya kizungu
na watumie jina la asili ya Afrika na ndipo jina la Mnyama tishio zaidi porini,
Mfalme wa Nyika, Simba, lilipowavutia hata ukawa mwanzo wa Simba SC.
Simba ikiwa inaitwa Sunderland, iliweza kutwaa ubingwa wa
Tanzania mara mbili tu, ikiweka rekodi ya kuwa klabu ya kwanza kutwaa taji hilo
mwaka 1965 na kuutetea mwaka 1966 na baada ya hapo haikuutia tena mikononi hadi
ilipobadilishwa jina na kuwa Simba, ndipo ilipourejesha mwaka 1973.
Simba ilishindwa kutetea taji lake mwaka 1974, baada ya
kuporwa na watani wao wa jadi, Yanga mwaka uliofuata, kwa kipigo cha mabao 2-1
katika fainali ya kihistoria iliyopigwa kwenye Uwanja wa Nyamagana, mjini
Mwanza.
Adamu Sabu (marehemu) aliyeingia uwanjani kuchukua nafasi ya
Saad Ali, aliifungia Simba bao la kuongoza, kabla ya Sunday Manara
kuisawazishia Yanga na Gibson Sembuli (marehemu pia) kufunga la ushindi kwa
Watoto wa Jangwani.
Ubingwa wa Tanzania mwaka 1975 kwa mara ya kwanza ulikwenda
nje ya Dar es Salaam, ukichukuliwa na Mseto ya Morogoro, iliyokuwa ikinolewa na
kocha maarufu, Mohamed Msomali.
Simba iliurejesha ubingwa wake mwaka 1976 na kuutetea kwa
miaka minne mfululizo, 1977, 1978, 1979 na 1980. Baada ya hapo, Simba iliyumba
na kupoteza makali, kabla ya kuibuka mwaka 1984 na kutwaa taji hilo.
Ililipoteza tena na kulazimika kulisubiri hadi mwaka 1990, kabla ya kulipoteza
na kulitwaa tena mfululizo mwaka 1994 na 1995. Simba ilitwaa tena taji hilo
katika miaka ya 2001, 2003, 2004, 2007 katika Ligi Ndogo, ikiifunga Yanga
kwenye fainali na msimu uliopita.
Ukiachana na utawala wa Simba katika soka ya Tanzania,
kwenye medani ya kimataifa klabu hiyo ndiyo inayoongoza kwa kuipeperusha vyema
bendera ya Tanzania.
Simba ndiyo klabu pekee iliyoweza kufika Nusu Fainali ya
Klabu Bingwa Afrika, mwaka 1974 ikiitoa timu ngumu ya Ghana katika Robo
Fainali, Hearts Of Oak kwa jumla ya mabao 2-0.
Yalikuwa ni mabao ya Sabu na Abdallah 'King' Kibadeni,
Wakenya wakimuita Ndululu kutokana na ufupi wake, mjini Accra, yaliyoipa timu
hiyo ushindi wa 2-0, kabla ya kuja kulazimisha sare ya bila kufungana mjini Dar
es Salaam.
Hata hivyo, baada ya kushinda 1-0 mjini Dar es Salaam dhidi
ya Mehala El Kubra, Simba ilikwenda kufungwa pia 1-0 na Waarabu hao mjini
Cairo, hivyo mchezo kuhamia kwenye mikwaju ya penalti, ambako Wekundu wa
Msimbazi waling'olewa.
Nyota wengine wa Simba walikuwa ni kipa Athumani Mambosasa,
mabeki Shaaban Baraza, Mohamed Kajole, Athur Mwambeta, Omari Chogo, viungo
Khalid Abeid, Willy Mwaijibe, Haidari Abeid, Abbas Dilunga na washambuliaji
Adam Sabu na Abdallah Kibadeni.
Nyota hao ndio waliowafunga watani wao wa jadi, Yanga mwaka
1973, baada ya Watoto hao wa Jangwani kutawala soka ya Tanzania kwa miaka
mitano mfululizo, wakichukua ubingwa wa nchi tangu mwaka 1968 hadi 1972. Hao
pia ndio waliotwaa ubingwa wa Afrika Mashariki na Kati kwa mara ya kwanza mwaka
1974 mjini Dar es Salaam.
Simba pia ni klabu pekee ya Tanzania, iliyoweza kucheza fainali
ya michuano ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF). Hiyo ilikuwa ni mwaka 1993,
ilipofanikiwa kutinga fainali ya Kombe la CAF, (sasa limeunganishwa na Kombe la
Washindi na kuwa Kombe la Shirikisho) na kufungwa na Stella ya mjini Abidjan,
Ivory Coast.
Bahati haikuwa yao Wekundu wa Msimbazi, kwani baada ya
kulazimisha sare ya bila kufungana ugenini, wengi waliamini kwenye mechi ya
marudiano, Stella hawatapona Dar es Salaam, lakini matokeo yake, wenyeji
walilala 2-0 kwa mabao ya Boli Zozo.
Klabu hiyo pia ilifanikiwa kuwa ya pili Tanzania kucheza
Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 2003, baada ya Yanga kuwa ya kwanza mwaka 1998.
Lakini Simba ilitinga hatua hiyo kiume zaidi, ikiwatoa waliokuwa mabingwa
watetezi, Zamalek ya Misri, kwa mikwaju ya penalti.
Hiyo ilifuatia ushindi wa 1-0 mjini Dar es Salaam, kabla ya
kwenda kufungwa 1-0 na yenyewe pia Cairo, lakini mchezo ulipohamia kwenye
mikwaju ya penalti, Juma Kaseja, mtaalamu wa kuokoa michomo hiyo, aliibeba
Simba baada ya kucheza penalti mbili.
Nyota waliokuwa wakiunda kikosi cha Simba mwaka 2003 ni Juma
Kaseja, Amri Said, Said Sued, Boniface Pawasa, Ramadhan Wasso, Victor Costa,
Yusuf Macho, Athumani Machuppa, Jumanne 'Shengo' Tondola, Emmanuel Gabriel,
Steven Mapunda, Madaraka Selemani, Ulimboka Mwakingwe, Patrick Betwel, Selemani
Matola, Amani Mbarouk, Farouk Ramadhan, Yahaya Akilimali, Primus Kasongo, Abu
Amrani, Kevin Mhagama, Majuto Komu, Lubigisa Edward Lubigisa, Christopher Alex,
William John, Emmanuel Kingu, Edibilly Lunyamila na Clement Kahabuka.
Aidha, Simba pia ndiyo klabu iliyoweza kutwaa mara nyingi
zaidi Kombe la Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, lijulikanalo kama Kombe
la Kagame katika miaka ya 1974, 1991, 1992, 1995, 1996 na 2002.
Katika michuano mingine midogo ya Afrika Mashariki, Kombe la
Tusker, Simba tena ndiyo timu iliyotwaa mara nyingi zaidi taji hilo, mara nne
kati ya michuano saba ya Kombe hilo, katika miaka ya 2001, 2002, 2003 na 2005.
Ililikosa mwaka 2006, lilipochukuliwa na Kagera Sugar, mwaka 2007
lilipochukuliwa na Yanga, mwaka 2008 lilipochukuliwa na Mtibwa Sugar na mwaka
2009, lilipiochukuliwa na Yanga tena.
Asili ya Simba SC tangu enzi na enzi ni kucheza soka ya
utulivu yenye kuburudisha mashabiki wake, wakitandaza pasi kwa wingi kabla ya
kulifikia lango. Imekuwa bahati iliyoje makocha wote wameendelea kuuenzi
utamaduni huo hadi kesho.
Japokuwa imepita mikononi mwa makocha wengi tangu kuanzishwa
kwake, lakini makocha wa kihistoria na wa kukumbukwa kwenye klabu hiyo ni
watano tu, kwanza Paul West Gwivaha (sasa marehemu), pili Nabby Camara, tatu
Abdallah Kibadeni, nne Msomali Enteneh Esheteh na wa mwisho ni Mkenya, James
Siang'a.
Kwa nini hao ndio makocha wa kihistoria Simba SC?
Wakati Simba inafika Nusu fainali ya Klabu Bingwa Afrika
mwaka 1974, ilikuwa inanolewa na Gwivaha na wakati inafika fainali ya Kombe la
CAF mwaka 1993, ilikuwa chini ya Kibadeni na Esheteh na mwaka 2003 ilipoitoa
Zamalek katika Raundi ya Pili ya Ligi ya Mabingwa, ilikuwa inanolewa na
Siang'a.
Camara, aliyekuwa raia wa Guinea, atakumbukwa kwa kuvumbua
vipaji vya nyota waliowika Simba baadaye, kama Abbas Kuka, Filbert Rubibira,
Nico Njohole na George 'Best' Kulagwa, kupitia timu ya vijana aliyounda mwaka
1975, baada ya kutua Simba.
Kwa sasa Simba iko chini ya Mserbia Profesa Milovan Cirkovic, ambaye ameiwezesha kurejesha makali yake, huku
mashabiki wa Wekundu hao wa Msimbazi, wakiwa wana matumaini ya kula raha zaidi
chini ya babu huyo aliyerejea mwaka mwishoni.
Simba SC ipo chini ya Mwenyekiti Ismail Aden Rage, Makamu
Mwenyekiti, Geoffrey Nyange ‘Kaburu’, Wajumbe sita wa Kamati ya Utendaji, ambao
ni Joseph Kinesi, Suedi Mkwabi, Saidi Pamba, Daniel Manembe, Francis Waya na
Ibrahim Masoud. Simba ina watendajiwa wa kuajiriwa, ambao ni Ofisa Utawala,
Evodius Mtawala na Ofisa Habari, Clifford Ndimbo- wakati meneja wa timu ni
Innocent Njovu na daktari ni Cosmass Kapinga.
Rasilimali kubwa za Simba ni majengo yake mawili pacha
yaliyopo Mtaa wa Msimbazi, Dar es Salaam. Jengo la kwanza la Simba lilijengwa
kwa mchango wa Karume na wanachama wa klabu hiyo wakaongezea fedha na
wakashiriki ujenzi, wakibeba, zege, mchanga, kokoto- yaani vifaa vya ujenzi kwa
ujumla na hata kufyatua tofali. Jengo la Simba lilijengwa chini ya uongozi wa
Mwenyekiti Dumelezi na Katibu Mkuu Said Mpolaki.
Jengo la pili lilijengwa kwa mpango maalumu wa mkataba na
mtu aliyeamua kuwekeza kwenye kiwanja cha wazi cha klabu hiyo. Mwekezaji
aliruhusiwa kujenga na kutumia jengo kwa biashara zake hadi mwaka 2012
alikabidhi kwa klabu.
Mpango kamili wa ujenzi wa jengo hilo ulioanzishwa na
aliyekuwa Katibu Mkuu wa Simba, Kassim Mohamed Dewji, ni kuwa na ghorofa nane
katika mtindo huo wa makubaliano na watu wenye nia ya kuwekeza kwenye jengo
hilo.
Mwekezaji wa sasa angeweza kuendelea na ujenzi wa jengo
hilo, kama wanachama wa klabu hiyo wasingefungua kesi mahakamani kupinga zoezi
hilo.
Simba SC pia ina mpango wa kujenga Uwanja wake wa kisasa
hivi sasa na tayari Rage amekwishakaririwa mara kadhaa akizungumzia ujenzi huo-
kwamba mipango inaendelea vizuri ingawa haujaanza.
Pamoja na mafanikio hayo, Simba imepitia vipindi tofauti,
vikiwemo vigumu, wakati ilipokutwa na misiba ya viongozi na wachezaji wake.
Migogoro pia, imekuwa sehemu ya matatizo ndani ya klabu ya Simba, ingawa kwa
upande mwingine hiyo ni demokrasia.
Mbali na majengo yake, Simba inajivunia udhamini wa kampuni
ya Bia Tanzania, kupitia bia ya Kilimanjaro.
Kilimanjaro imeleta ukombozi Simba, ambayo ilikuwa inahaha
tangu kumpoteza mdhamini wake wa mwisho, Mohamed Enterprises Limited (MeTL),
kampuni inayomilikiwa na mpenzi mkubwa wa klabu hiyo, Mohamed Gullam Dewji.
Wafadhili wengine wa Simba, tangu enzi za Sunderland ni
mmiliki wa Salama Travel Agency, Saleh Ruwey ambaye aliwanunulia basi la kwanza,
Colt Rosa (sasa halipo tena), Ramesh Patel, Fakhrudin Amijee, Ally Mwinyi
Tambwe na Abdulrahman Muchacho, ambaye alikuwa akiilisha Simba.
Miaka ya 1990, ndipo walipoibuka wafadhili wengine kama Azim
Dewji, ambaye baadaye aliitema timu hiyo kutokana na migogoro, japo amebaki
mwanachama na anahudhuria mikutano wakati mwingine.
Mkataba wa awali wa Kilimanjaro uliokuwa na thamani ya Sh
bilioni 3, kila mwaka Simba ilikuwa inapata
Sh bilioni 1, kwa ajili ya shughuli za uendeshaji wa timu.
Mkataba huo, ulisainiwa Agosti 18, mwaka 2008, katika hoteli
ya Movenpick, mjini Dar es Salaam.
Kilimanjaro Premium Lager, ambayo imetoa pia udhamini kama
huo kwa Yanga, imekuwa ikiipa Simba Sh milioni 16, kila mwezi kwa ajili ya
mishahara ya wachezaji, hiyo ikiwa ni mbali na kupatiwa mabasi mawili madogo.
Mabasi hayo, moja aina ya Hiace na jingine Coaster, tayari yamekwisha
kukabidhiwa kwa klabu hiyo na yameanza kutumika.
Aidha, Kili pia imeweka utaratibu wa kuipa Simba zawadi,
iwapo itafanikiwa kushika moja ya nafasi mbili za juu kwenye msimamo wa Ligi
Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, ikiwa bingwa itapata Sh milioni 25 na ikishika
nafasi ya pili, itapewa Sh milioni 15.
Agosti mwaka jana, TBL kupitia bia yake ya Kilimanjalo ilisaini
mkataba mpya na Simba katika hoteli ya Double Tree.
Mkataba huo ulioanza rasmi Agosti 1, mwaka jana utaisha
Julai 31, mwaka 2016.
Katika mkataba huo, Simba watakuwa wanapewa fedha za mishahara
kwa mwezi Sh. Milioni 25 kwa mwezi, watapewa basi jipya la abiria 54, fedha za
kuendeshea Mkutano Mkuu wa mwaka, Shilingi Milioni 20 kwa kwa ajili ya tamasha
la kila mwaka, Simba Day, vifaa vya mechi na mazoezi vyenye thamani ya Sh. Milioni
35 kila msimu, wakiwa mabingwa watapewa Sh Milioni 25, wakiwa washindi pili Sh.
Milioni 15.
Simba, inayojulikana pia kwa majina ya utani kama Wekundu wa
Msimbazi, Mnyama na Taifa Kubwa, imekuwa ikipewa vifaa vya thamani na vya
kisasa vya michezo, lengo likiwa ni kuifanya iwe bora na mfano wa kuigwa katika
ligi hiyo.
Lakini Simba ina kundi la wapenzi wa klabu hiyo, waliounda
umoja wao chini ya Kassim Dewji, uitwao Friends Of Simba, ambalo linasaidia mno
klabu hiyo. Kundi hilo lililoibuka mwaka 2001, likiwa na watu kama Crescentius
Magori, Evans Aveva, Mulamu Nghambi, Mohamed Nassor, Musley Ruwey, Harrison
Mutembey, Jerry Yambi na wengine, limekuwa likisaidia huduma za timu, usajili
na kadhalika.
Bado kuna watu wengine mashuhuri nchini, wakiwemo
wafanyabiashara na viongozi wa serikali, ambao kwa mapenzi yao wamekuwa
wakiisaidia mno Simba.
Timu hii yenye mashabiki hadi nchi jirani za Kenya, Uganda,
Rwanda, Burundi, ina sura ya kitaifa na ina matawi hadi mikoani, bara na
visiwani.
Ingawa tathmini inaonyesha Yanga ndiyo yenye mashabiki wengi
zaidi ya Simba, lakini siku za karibuni ni kama mambo yanaanza kubadilika,
kwani kwa vigezo vile vile vilivyotumika kubaini kuwa Yanga ndiyo yenye
mashabiki wengi, Simba nayo inaonekana kuongeza idadi ya mashabiki wake.
Kigezo kikubwa kinachotumika ni idadi ya mapato yatokanayo
na viingilio vya milangoni, Simba nayo siku hizi inavutia watu wengi na
kutengeneza mapato makubwa, wakati mwingine kuliko Yanga.
Yote kwa yote, linapokuja swali nani zaidi baina ya watani
wa jadi, ukiachilia mbali mechi baina ya wababe hao, Simba inaweza kujinasibu
ndiyo mbabe, kutokana na rekodi nzuri katika medani ya kimataifa.
Naam, hao ndio Simba SC, Wekundu wa Msimbazi, wapeperusha
vyema bendera ya nchi kwenye michuano ya kimataifa.
REKODI ZA SIMBA:
UBINGWA WA LIGI KUU:
1965, 1966, 1973, 1976, 1977, 1978, 1979, 1980, 1984, 1990,
1994, 1995, 2001, 2003, 2004 na 2007
(Ligi Ndogo), 2010 na 2012.
LILILOKUWA KOMBE LA NYERERE:
1984, 1995 na 2000
LILILOKUWA KOMBE LA MUUNGANO:
1993, 1994, 1995, 2001, na 2002
KOMBE LA TUSKER:
2001, 2002, 2003 na 2005
KOMBE LA CAF:
Ilifika fainali mwaka 1993
KOMBE LA KAGAME:
1974, 1991, 1992, 1995, 1996 na 2002
LIGI YA MABINGWA AFRIKA:
Kucheza hatua ya makundi 2003
KLABU BINGWA AFRIKA:
Kucheza Nusu Fainali 1974
MABINGWA WA JUMLA LIGI KUU:
1965 : Sunderland (Dar es Salaam)
1966 : Sunderland (Dar es Salaam)
1967 : Cosmopolitans (Dar es Salaam)
1968 : Yanga
1969 : Yanga
1970 : Yanga
1971 : Yanga
1972 : Simba
1973 : Simba
1974 : Yanga
1975 : Mseto SC (Morogoro)
1976 : Simba
1977 : Simba
1978 : Simba
1979 : Simba
1980 : Simba
1981 : Yanga
1982 : Pan African
1983 : Yanga
1984 : Simba
1985 : Yanga
1986 : Tukuyu Stars (Mbeya)
1987 : Yanga
1988 : Coastal Union (Dar es Salaam)
1989 : Yanga
1990 : Simba
1991 : Yanga
1992 : Yanga
1993 : Yanga
1994 : Simba
1995 : Simba
1996 : Yanga
1997 : Yanga
1998 : Yanga
1999 : Mtibwa Sugar (Morogoro)
2000 : Mtibwa Sugar (Morogoro)
2001 : Simba
2002 : Yanga
2003 : Simba
2004 : Simba
2005 : Yanga
2006 : Yanga
2007 : Simba (Ligi Ndogo)
2008 : Yanga
2009: Yanga
2010: Simba SC
2011: Yanga SC
2012: Simba SC?
0 comments:
Post a Comment