Simba SC, mabingwa watarajiwa |
MEI 5, mwaka huu nyasi za Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam zitawaka moto
kwa mpambano mkali wa watani wa jadi, Simba na Yanga katika Ligi Kuu ya Vodacom
Tanzania Bara.
Ingawa mchezo huo unachukuliwa kama wa kukamilisha ratiba tu, kwa kuwa
Simba ilikwishajisogeza jirani na ubingwa na Yanga imekwishatoka kwenye
matumaini ya kupata hata nafasi ya pili, baadhi wana dhana tofauti- tena
inayowadanganya.
Hiyo inafuatia kuvunjika kwa mechi kati ya Azam FC na Mtibwa Sugar,
Uwanja wa Azam, Chamazi, Mbagala, Dar es Salaam wiki iliyopita, wanadhani mambo
yamebadilika.
Mtibwa ndiyo walikuwa sababu ya kuvunjika mechi hiyo, baada ya kugomea
penalti, na matokeo yake Kamati ya Ligi Kuu imewapa ushindi Azam.
Lakini katika kutoa adhabu, Kamati ya Ligi Kuu imeonyesha mapungufu
kulingana na kanuni inavyosema; kwamba timu inayosababisha mechi kuvunjika
inashushwa daraja. Wao hawajatoa adhabu kwa ukamilifu kulingana na maelekezo ya
kanuni.
Nini kinachofuata Mtibwa ikishushwa daraja? Matokeo yake yatafutwa, ina
maana timu zilizonufaika kwa kubeba pointi nyingi dhidi ya Mtibwa, yenye
maskani yake Uwanja wa Manungu, Turiani ambayo tangu ipande Ligi Kuu mwaka
1996, haijawahi kushuka zitaathirika.
Simba ni timu pekee iliyovuna pointi zote sita kwa Mtibwa, kwanza
ikiifunga 1-0 Septemba 25, mwaka jana mjini Morogoro na baadaye 2-1 katika
mchezo wa marudiano Machi 18, mwaka huu.
Azam ilivuna pointi tatu tena za mezani, kwani mechi ya kwanza Oktoba
25, mwaka ilifungwa 1-0 kabla ya mechi ya marudiano iliyovunjika na Yanga
ilivuna pointi nne, kutokana sare ya bila kufungana katika mechi ya kwanza
Septemba 11, mwaka jana kabla ya kushinda 3-1 katika mchezo wa marudiano Februari
8, mwaka huu.
Iwapo adhabu ya Mtibwa ingetokana na maelekezo ya kanuni, Azam
ingenufaika zaidi- kwa sababu ingekatwa pointi tatu, wakati Simba ingekatwa
pointi sita na Yanga pointi nne.
Kwa sasa Simba ina pointi 59 na ikishinda mechi ya mwisho itatawazwa
rasmi kuwa bingwa, kwa kufikisha pointi 62, lakini kama Mtibwa itashushwa daraja,
Wekundu wa Msimbazi watamaliza na pointi hizo hizo 59 iwapo wakiifunga Yanga
katika mechi ya mwisho.
Azam wana pointi 53 na wakishinda mechi zao mbili za mwisho dhidi ya
Kagera na Toto, watafikisha pointi 59- lakini Mtibwa ikishushwa watamaliza na
pointi 56. Ina maana hata kama Simba ikifungwa na Yanga na Mtibwa ikashushwa, bingwa ataamuliwa kwa wastani wa mabao.
Kama Mtibwa ikishushwa, katika hesabu zake za sasa Yanga itajiongezea
pointi moja tu, je wataipiku Azam? Jua la mwakani.
Nataka niwaambie tu wadau wenye kudhani Mtibwa ikishushwa Top 3 ya Ligi
Kuu ya Bara itabadilika, wanajidanganya. Itabaki vile vile.
MECHI ZA MTIBWA DHIDI
YA TOP 3 LIGI KUU BARA
J’tano 07/09/11 Mtibwa 0 – 0 Yanga
J’nnee 25/10/11 Mtibwa 1
– 0 Azam
J’pili 25/09/11 Simba 1 – 0 Mtibwa
Sugar
J’tano 08/02/12 Yanga 3 – 1 Mtibwa
Sugar
J’pili 18/03/12 Simba 2
– 1 Mtibwa Sugar
J’tatu 23/04/12 Azam 1 – 1 Mtibwa
Sugar
(Mechi ilivunjika, Azam ikapewa pointi tatu)
(Mechi ilivunjika, Azam ikapewa pointi tatu)
0 comments:
Post a Comment