Soka | Ligi Kuu England
| |
Rooney-Welbeck ni Yorke-Cole wapya
KOCHA wa Manchester United, Sir Alex Ferguson anaamini washambuliaji wake wawili Wayne Rooney na Danny Welbeck wanaweza kufanya kazi nzuri ya kufunga mabao Old Trafford kama Dwight Yorke na Andy Cole enzi zao.
Welbeck alifunga bao lake la 12 msimu huu katika mechi iliyopita ya sare ya 4-4 na Everton, wakati Wayne Rooney alifunga mawili na kufikisha 33.
Kiwango hicho kinakumbusha mabao 53 ambayo Yorke na Cole waliifungia United mwaka 1999 ikitwaa mataji matatu msimu huo.
"Wiki iliyopita tuliona kitu fulani maalumu sana,"alisema Ferguson, kuelekea mechi ya Jumatatu ya Ligi Kuu na Manchester City.
"Nafahamu hapa kuna kumbukumbu lukuki za Yorke na Cole enzi zao. Kulikuwa kuna dalili za kufanana hilo. Mwenendo wa Danny ulikuwa babu kubwa. Sasa yuko fiti tena na anacheza mfululizo, anaendelea vizuri.
"Wayne ana miaka 26 sasa. Danny mikaka ya 21. Kwa miaka michache ijayo watakuwa vema tu. Tunatumaini mno hivyo."
Ferguson anaamini kuwekeza kwenye maendeleo ya soka ya vijana kunalipa na ataendelea kufanya hivyo hata kama itatoa nafasi kwa wapinzani wake kama Man City, Liverpool na Chelsea kubomoa akaunti zao kwa manunuzi ya wachezaji nyota.
"Ni vigumu kubadilisha njia yetu ya kufanya mambo," alisema Ferguson.
"Baada ya kutawala, wakati tuliposhinda mataji matatu na kilichofuatia hapo tulipitia vipindi tofauti, kulikuwa kuna kipindi cha mpito.
"Tulijaribu kujenga upya timu na wachezaji wadogo, kama Rooney na (Cristiano) Ronaldo na mmoja kati ya wachezaji wetu tuliowapika wenyewe kwenye chuo chetu aliibuka pia."Nafikiri tutaendelea kufanya kama tunavyofanya."
0 comments:
Post a Comment