MJUMBE wa Kamati ya Ufundi ya Yanga, Dk Maneno Tamba (pichani kushoto) amewaomba wapenzi na wanachama wa Yanga kushikamana katika wakati huu mgumu,
wamalize Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara salama.
Akizungumza na bongostaz.blogspot.com, Dk Tamba alielezea
kusikitishwa kwake na kujiuzulu kwa Wajumbe wawili wa Kamati ya Mashindano ya
klabu hiyo, Seif Ahmad ‘Magari’ na Abdallah Ahmed Bin Kleb mwanzoni mwa wiki.
Tamba alisema viongozi hao wanaondoka katika uongozi katika
kipindi kigumu ambacho, timu imekosa nafasi ya kucheza michuano ya Afrika
mwakani na inakabiliwa na mechi ngumu ya mwisho ya Ligi Kuu dhidi ya watani wa
jadi, Simba SC.
“Nawaomba wanachama, wapenzi, wachezaji na viongozi, kushikamana
na kuwa kitu kimoja haswa katika wakati huu wa kujiandaa na kucheza mechi ya
mwisho na Simba.
Na viongozi waliojiuzulu, au kutangaza kujitoa, nao huu si
wakati mwafaka kufanya hivyo, na kama wapo wengine wanaotaka kufanya hivyo,
nawaomba wasifanye kwa kipindi hiki,”alisema Dk Tamba.
Tamba aliongeza; “Wao wana dhamana kubwa waliyopewa na
wanachama wa Yanga, wakiwa wanataka kutoka, basi wasubiri tumalize ligi ndio
watoke, mbele ya wanachama wa Yanga, mkutanoni, waseme yote mabaya na maovu,”aliasa
Dk Tamba.
Seif na Bin Kleb wamejiuzulu kwa sababu za kutoridhishwa na
uongozi wa klabu hiyo chini ya Mwenyekiti wake, Wakili Lloyd Baharagu Nchunga.
Wameelezea matatizo mengi katika kujiuzulu kwao, kubwa ni
kutokuwa na imani na Mwenyekiti wao. Tayari Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Davis
Mosha alijiuzulu Machi mwaka jana kwa sababu ya kutokuwa na imani na Mwenyekiti
wake huyo.
Yanga imekosa nafasi ya kuwakilisha nchi kwenye michuano ya
Afrika mwakani, baada ya kuzidiwa kete na Azam FC.
Walikuwa wana mwendo mzuri na mwelekeo wa ubingwa kabla ya
kupoteza pointi tisa mfululizo, dhidi ya Coastal Union ya Tanga, Toto African
ya Mwanza na Kagera Sugar ya Bukoba.
Licha ya kuifunga Coastal 1-0 Uwanja wa Mkwakwani, Tanga-
Yanga ilipokonywa pointi tatu kwa kosa la kumtumia beki Nadir Haroub ‘Cannavaro’
akiwa hajamaliza kutumikia adhabu yake ya kadi nyekundu kabla ya kwenda
kufungwa na Toto mabao 3-2 na Kagera 1-0.
Lakini baada ya hapo, Yanga imeshinda mechi zake mbili mfululizo
kabla ya kumenyana na Simba, 3-1 dhidi ya Polisi Dodoma na 4-1 dhidi ya JKT
Oljoro mjini Arusha.
0 comments:
Post a Comment