Azim Dewji |
BAADA ya timu ya soka ya Simba
kuing’oa ES Setif ya Algeria katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika,
mfanyabiashara maarufu na mfadhili wa zamani wa klabu hiyo yenye makao yake
makuu Mtaa wa Msimbazi, Dar es Salaam, Azim Dewji ametangaza kuwamwagia
wachezaji kitita cha sh milioni 15.
Simba, `wataalamu’ wa michuano
ya kimataifa wa Tanzania, wameingia raundi ya tatu ya michuano ya mwaka huu,
licha ya usiku wa juzi kufungwa 3-1 ugenini Algeria, kwani tayari
ilishatengeneza akiba nzuri ya mabao kutokana na ushindi wa 2-0 jijini Dar es
Salaam wiki mbili zilizopita.
Dewji, akiwa mwenye furaha
alitamka jana kuwa, anawazawadia wachezaji hao kutokana na ushujaa wa kupigana
kiume hadi kufanikiwa kuing’oa timu hiyo ngumu kutoka Kaskazini mwa Afrika.
Alisema kuwa, alitoa hiyo katika
mchezo wa kwanza uliofanyika Dar es Salaam na kwamba anachokifanya sasa ni
kutimiza ahadi.
“Kwanza niwashukuru wachezaji
kwa kuwapa raha WanaSimba na Watanzania kwa ujumla, name nakamilisha furaha
yangu kwa kuwapa sh milioni 15 nilizoahidi.
“Nitakabidhi mara mashujaa hawa
watakaporejea nchini kutoka Algeria. Hakika wametupa heshima kubwa sana,”
alisema.
Mwanamichezo huyo aliyeiongoza
Simba kufika fainali za Kombe la CAF mwaka 1993, pia kuiwezesha Tanzania Bara
kutwaa ubingwa wa Chalenji huko Kenya akiwa Mwenyekiti wa Kamati ya Kuisaidia
Taifa Stars mwaka 1994, alisema atazidi kusaidia kadri timu itakavyoendelea
kufanya vizuri.
Aidha, alitumia fursa hiyo
kuwataka viongozi, wachezaji na wanachama kuongeza mshikamano ili kila timu
itakayokumbana na Simba katika michuano ya mwaka huu iishie kuangua kilio.
“Siri ya mafanikio ni
mshikamano. Baada ya Setif tujipange kwa vita iliyopo mbele, naamini kwa nguvu
za pamoja tutafika,” alisisitiza mfanyabiashara huyo ambaye hivi karibuni
aliwajaza pesa wachezaji wa timu ya Taifa ya Zambia `Chipolopolo’ baada ya
kutwaa ubingwa wa Afrika usiku wa Februari 12 huko Libreville, Gabon
ilikoizamisha Ivory Coast kwa mabao 8-7.
0 comments:
Post a Comment