Bin Kleb akimkabidhi Haruna Niyonzima jezi baada ya kumsajili |
WAJUMBE wawili wa Kamati ya Utendaji ya Yanga, Seif Ahmad ‘Magari’
na Abdallah Bin Kleb wamewasilisha barua za kujiuzulu wadhifa wao huo wa
kuteuliwa, imeelezwa.
Mwenyekiti wa Yanga, Wakili Lloyd Baharagu Nchunga ameiambia
bongostaz.blogspot.com mchana huu kwamba, ameambiwa juu ya Wajumbe hao wa
Kamati ya Mashindano, kuwasilisha barua za kujiuzulu.
Alipoulizwa sababu zilizoainishwa na watu hao kwenye barua
zao, Nchunga alisema kwamba ni kutokuwana imani na uongozi.
“Alipokuwa akizungumza na Radio One jana, alisema ni kwa sababu
za kifamilia, lakini katika barua niliyosomewa na Katibu (wa Yanga, Celestine
Mwesigwa), Seif amesema haridhishwi na mambo yanavyokwenda kwenye uongozi,”alisemsa Nchunga akiinukuu barua ya
Seif.
“Anasema hapati taarifa za fedha kutoka kwa Katibu. Anasema fedha
nyingi zinaingia Yanga, lakini yeye hajulishwi, wakati wao wanatumia fedha
nyingi kugharamia klabu,”alisema Nchunga.
Nchunga alisema yeye alikuwa safarini Afrika Kusini na
amerejea jana, lakini hajaziona rasmi hizo barua bali amesomewa na Katibu Mkuu.
Lakini alipoulizwa maoni yake juu ya madai ya Seif, kwanza Nchunga
alisema; “Kwanza nataka niseme, huu haukuwa wakati mwafaka kuleta haya mambo,
tuna wiki mbili kabla ya kucheza na Simba. Hizi ni dalili mbaya,”alisema.
Kuhusu madai ya Seif kutojulishwa taarifa za fedha, Nchunga
alisema kwamba taarifa za fedha zinatolewa katika vikao vya Kamati ya Utendaji.
“Na sisi tunakutana sana, na kama mtu anataka kuhoji jambo,
hakatazwi, sasa sielewei hii inatoka wapi,”alisema.
Lakini Nchunga alisema inawezekana matokeo mabaya msimu huu
yamechafua hali ya hewa ndani ya Yanga kiasi kwamba viongozi hao wameshindwa
kuimudu.
“Kuna mengi katika wakati huu timu ikiwa vibaya, kuna
kuzongwa na wanachama na nini, ni mambo ambayo viongozi wanatakiwa kuvumilia na
tujipange upya kwa ajili ya mashindano yajayo, lakini si kujiuzulu,”alisema
Nchunga.
Pamoja na hayo, Nchunga alisema kwamba anawatafuta kwanza
viongozi hao azungumze nao na kujaribu kuwashawishi warudi katika uongozi.
“Nina wajibu wa kufanya jitihada za haraka ili kunusuru
mmomonyoko huu usitokee, huu ni wakati ambao wana Yanga tunapaswa kushikamana
sana ili kuinusuru klabu yetu, hapa ninatoka kuanza kuhangaikia hilo,”alisema Nchunga.
Yanga ipo katika wakati mgumu hivi sasa, baada ya kukosa
nafasi ya kucheza ya michuano ya Afrika mwakani, ikizidiwa kete na Azam FC.
Yanga ilipoteza nafasi hiyo, baada ya kupoteza pointi tisa
mfulilizo katika mechi dhidi ya Coastal Union, Toto African na Kagera Sugar.
Pamoja na kuifunga Coastal bao 1-0, lakini Yanga ilipokonywa
pointi kwa kosa la kumtumia beki Nadir Haroub ‘Cannavaro’ akiwa anatumikia
adhabu kabla ya kwenda kufungwa 3-2 na Toto na 1-0 na Kagera.
Seif na Bin Kleb ni watu muhimu mno ndani ya Yanga kwa sasa,
ambao wazi kama wataachia ngazi klabu itayumba na kuna hatari ya kupoteza
malengo ya msimu ujao.
Achilia mbali ujanja wao wa mjini unaowawezesha kupambana na
fitina za wapinzani wao katika Ligi Kuu, lakini wamekuwa wakihudumia timu
kuanzia usajili na uendeshaji.
0 comments:
Post a Comment