BAO la dakika ya 89 lililofungwa na Hamisi Kiiza jioni hii
wakati Yanga ilipocheza na Villa Squad Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam katika mfululizo wa mechi za
Ligi Kuu Tanzania Bara, liliiwezesha Yanga kutoka kifua mbele kwa kujipatia
pointi tatu muhimu katika ligi hiyo.
Yanga sasa inapanda hadi nafasi ya pili, kwa kutimiza pointi
43 baada ya kucheza mechi 20, sawa na vinara Simba SC wenye pointi 44, ambao
leo wanacheza mechi ya 21 na Mtibwa Sugar. Azam yenye pointi 41, inashuka hadi
nafasi ya tatu na kuwaachia ‘wanaume’ anga zao.
Kiiza aliipatia timu yake bao hilo pekee baada ya kumalizia
kazi nzuri iliyoanzishwa na Haruna Niyonzima kisha Godfrey Taita kuachia shuti
kali la mbali lililomkuta mfungaji aliyekwamisha wavuni na kuwainua mashabiki wao katika dakika hizo
za lala salama ambao walikuwa vichwa chini wakitarajia mechi hiyo ingekwisha
kwa suluhu.
Hasa baada ya Davies Mwape kuwakatisha tamaa kwa kukosa
nafasi nyingi za kufunga hasa ile ya dakika 69 baada ya Pius Kisambale
kumtengenezea mpira mzuri hivyo kuwakera mno mashabiki wao.
Mbali ya Mwape, Kenneth Asamoah naye alikosa bao la wazi
akiwa yeye na kipa wa Villa Squad, Daudi Mwasongwe dakika ya 57 aliposhindwa
kuitendea haki krosi ya Haruna Niyonzima.
Villa itabidi ijilaumu kuruhusu nyavu zao kutikiswa dakika
za lala salama kwani walikuwa wameishawabana Yanga kwa kuonyesha kandanda safi
na kuufanya mchezo huo kuwa mgumu kwa pande zote lakini wakishindwa kuhimili
vishindo.
Katika nafasi ambazo Villa itazijutia, ni dakika ya 22 baada
ya mchezaji wao, Martin Rupert kupiga mpira nje ya lango la Yanga akiwa peke yake na kushindwa kucheka
na nyavu huku mchezaji huyo akiendelea kufanya makosa ya kushindwa kucheka na
nyavu dakika 71 baada ya kumpoka mpira Oscar Joshua.
Hata hivyo pambano hilo ambalo matokeo yake yalikuwa
yakisubiriwa kwa hamu na mashabiki wa soka, lilikuwa zuri na kuwa kivutio kwa
mashabiki waliojitokeza uwanjani.
Katika mchezo mwingine leo, Coastal Union imefanikiwa
kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya maafande ya JKT Orjolo huo pia ukiwa ni
mchezo wa Ligi Kuu.
Bao la Coastal Union lilifungwa dakika ya 18 na Salum Sued
kwa penati baada ya mchezaji mwenzake,
Daniel Lyanga kukwatuliwa katika eneo la hatari na mchezaji wa JKT Orjolo,
Omary Mswaki.
Ligi hiyo itaendelea leo katika viwanja viwili ambapo katika
Uwanja wa Jamhuri Morogoro, Simba itatoana jasho na Mtibwa Sugar huku katika
dimba la Chamazi, wenyeji Azam FC ikiwakaribisha maafande wa Ruvu Shooting.
0 comments:
Post a Comment