KLABU ya Yanga imekata rufani Shirikisho la Soka Tanzania
(TFF), ikipinga hatua ya Kamati ya Ligi ya shirikisho hilo kuwafungia wachezaji
wake watano wakiwemo Stephano Mwasika na Nadir Haroub ‘Cannavaro’.
Juzi Kamati ya Ligi ya TFF iliyokutana Dar es Salaam ilitoa
adhabu kwa wachezaji watano wa Yanga kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo
kudaiwa walimpiga mwamuzi wakati wa
mchezo wa timu hiyo na Azam Jumamosi kwenye Ligi Kuu
Tanzania Bara uliomalizika kwa Yanga kufungwa mabao 3-1.
Wachezaji hao ni Stephano Mwasika, Nadir Haroub ‘Cannavaro’,
Jerry Tegete, Omega Seme na Nurdin Bakari, wanaodaiwa kumpiga mwamuzi Israel
Nkongo kwenye mechi hiyo.
Ofisa Habari wa Yanga, Luios Sendei alisema jana kuwa adhabu
walizopewa wachezaji hao ni kubwa na zinaua vipaji vyao, hivyo wataomba kwa
Kamati ya Nidhamu ya TFF kuwapunguzia
adhabu hizo.
Kulingana na Ofisa Habari wa TFF, Boniface Wambura,
Cannavaro, amefungiwa mechi sita za Ligi Kuu na kupigwa faini ya Sh 500,000,
baada ya kuoneshwa kadi nyekundu kwa kosa la
kumshambulia mwamuzi Israel Nkongo kwenye mechi hiyo ya
Yanga na Azam.
“Wachezaji wengine wa Yanga walioadhibiwa kutokana na mechi
hiyo ni Nurdin Bakari amefungiwa mechi tatu na faini ya Sh 500,000, Omega Seme
amefungiwa mechi tatu na faini ya Sh 500,000, Jerryson Tegete amefungiwa miezi
sita na faini ya Sh 500,000.
“Stephano Mwasika amefungiwa mwaka mmoja na faini ya Sh
milioni moja kwa kumpiga mwamuzi Nkongo. Adhabu zote zimetolewa kwa mujibu wa
Kanuni za Ligi Kuu.
“Kamati ya Ligi imempongeza Nahodha wa Yanga, Shadrack
Nsajigwa na mshambuliaji wa timu hiyo Hamis Kiiza kwa kuwa mstari wa mbele
kuzuia wenzao kumshambulia mwamuzi. Pia
imempongeza kocha Kostadin Papic wa Yanga kwa kukemea vurugu
zilizofanywa na wachezaji wake,” alisema.
Hata hivyo akizungumzia hilo, Sendeu alisema wameomba radhi
kwa tukio lililofanywa na wachezaji, hivyo TFF iwasaidie kwa kuwapunguzia
adhabu.
“Mwasika kwa muda mrefu alikuwa majeruhi, ndiyo ameanza
kucheza, lakini Nurdin pia alikuwa majeruhi, tunaamini TFF itafikiria angalau
kuwapunguzia adhabu. Ni kubwa sana na inaua vipaji vyao,” alisema.
Kwa upande wake Wambura alikiri Yanga kuwasilisha barua TFF,
ikidai wachezaji wake wameonewa katika mchezo huo.
Wakati huohuo, Wambura alisema Kamati hiyo ya Ligi pia
imetoa adhabu kwa Villa Squad ambayo imetozwa faini ya Sh 500,000 baada ya
mashabiki wake kufanya vurugu kwenye mechi dhidi ya Azam iliyochezwa Februari
15 mwaka huu Uwanja wa Chamazi.
“Pia klabu hiyo imepigwa faini ya Sh 300,000 kwa kuchelewa
uwanjani kwenye mechi namba 129 dhidi ya Mtibwa Sugar iliyochezwa Februari 19
mwaka huu Uwanja wa Manungu.
Nayo Yanga imepigwa faini ya Sh 500,000 kutokana na mashabiki
wake kufanya vurugu kwenye mechi dhidi ya Azam,” alisema Wambura na kuongeza
kuwa Yanga imepigwa faini ya Sh 500,000 baada ya wachezaji wake kuoneshwa kadi
kuanzia tano kwenye mechi dhidi ya Azam.
“Mchezaji Juma
Mohamed wa Polisi Dodoma amefungiwa mechi tatu na kupigwa faini ya Sh 500,000
baada ya kuwashambulia watazamaji kwa chupa ya maji katika mchezo kati ya timu
yake na Villa Squad uliochezwa Februari 11 mwaka huu,”
alisema
0 comments:
Post a Comment