Waziri Membe |
WAZIRI wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard
Membe, ndiye atakuwa mgeni rasmi katika tamasha la Pasaka litakalofanyika
Sikukuu ya Pasaka Aprili 8 mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana,
Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya Tamasha la Pasaka ambaye ni Mkurugenzi
Mtendaji wa Kampuni ya Msama Promotions, waandaaji wa tamasha hilo, Alex Msama
alisema Waziri Membe amethibitisha kuwa mgeni rasmi katika kilele cha tamasha
hilo.
"Napenda kuwaambia kwamba Waziri Membe amethibitisha
kuwa mgeni rasmi katika tamasha la Pasaka la mwaka huu.
"Amekubali kushirikiana na Wakristo wote kusherehekea
Sikukuu ya Pasaka kwenye Uwanja wa Taifa," alisema Msama.
Msama kwa niaba ya Kamati alimshukuru Waziri Membe kwa
kukubali mwaliko wa kuhudhuria tamasha hilo la Pasaka kwa kusema: "Hii ni
furaha si kwa waandaaji wa tamasha la Pasaka tu bali ni kwa Wakristo wote,
maana siku hiyo ni siku ya kusherehekea Sikukuu ya Pasaka.
"Itakuwa ni siku ya furaha, nderemo na shangwe ambapo
tutafurahi pamoja na Waziri Membe katika tamasha la Pasaka ambalo hufanyika kwa
mwaka mara moja," alisema Msama.
Kwa mujibu wa Msama, tamasha hilo limelenga kuchangia watoto
yatima na kusaidia wajane wasiojiweza.
Mbali na Dar es Salaam, tamasha la Pasaka pia litafanyika
mjini Dodoma Aprili 9 mwaka huu kwenye Uwanja wa Jamhuri ambayo ni Jumatatu ya
Pasaka.
Baadhi ya viongozi waliowahi kuwa wageni rasmi katika
matamasha yaliyopita ya Pasaka ni Rais mstaafu, Alhaj Ali Hassan Mwinyi (2000),
Mchungaji, Dk. Getrude Rwakatare (2001), Profesa Jumanne Maghembe (2005)
aliyemwakilisha Rais Jakaya Kikwete.
Wengine ni Mwenyekiti wa Kampuni za IPP, Reginald Mengi
(2006), Mama Salma Kikwete (2007), Philip Marmo (2008), aliyekuwa Spika wa
Bunge la Tisa, Samuel Sitta (2009) na Rais Kikwete (2011). Mwaka 2010 tamasha
halikufanyika.
0 comments:
Post a Comment