Solomon Mukubwa |
KATIKA matamasha ya Pasaka mwaka 2010 na 2011, yaliyopambwa
kwa muziki wa Injili kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee, Dar es Salaam,
kusherehekea Sikukuu ya Pasaka, nyoyo za mashabiki zilikongwa na waimbaji
kochokocho waliotumbuiza.
Lakini kivutio kikubwa walikuwa ni mwimbaji wa Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Congo (DRC) anayeishi Kenya, Solomon Siaka Mukubwa na Rose
Muhando, ambao mara kwa mara kelele za mashabiki zilisikika wakitaka kila mmoja
aendelee kuwapa burudani.
Mbali ya Rose Muhando ambaye wimbo wake wa Nibebe uliteuliwa
kuwa Wimbo Bora wa Mwaka 2009 kupitia televisheni ya Taifa, TBC1 na Mukubwa,
wasanii wengine walioshiriki na kufanya vizuri ni Flora Mbasha na Upendo Nkone.
Waimbaji wengine ni Bahati Bukuku, Jennifer Mgendi, Geraldine
Oduor, Enock Jonas, na kundi la muziki wa Injili la Upendo la Kijitonyama, Dar
es Salaam.
Lakini Mukubwa na Rose ndio waliokuwa kivutio zaidi kutokana
na kushangiliwa kwa nguvu. Mukubwa anasema hamasa aliyoipata mwaka juzi na
mwaka jana ndiyo inampa msukumo zaidi wa kuendelea kukonga nyoyo za mashabiki
katika tamasha la mwaka huu.
Tamasha la mwaka huu litafanyika kwenye Uwanja wa Taifa, Dar
es Salaam, Aprili 8, kisha litarindima kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma
Aprili 9, ambayo itakuwa Jumatatu ya Pasaka.
Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya tamasha hilo, Alex
Msama anasema kwa vile tamasha la mwaka jana lilikuwa la mafanikio makubwa,
anaamini mwaka huu watavuka malengo ya kukusanya fedha kwa ajili ya watoto
yatima na kuwasaidia mitaji ya biashara wajane wasiojiweza.
Wasifu wa Mukubwa
Mukubwa ni mlemavu wa mkono mmoja wa kushoto anaodai umekuwa
katika hali hiyo kutokana na kudhuriwa kwa uchawi na mama yake wa kambo
alipokuwa na umri mdogo.
Anasema akiwa na miaka 12, alipata matatizo hayo kwa kutokea
uvimbe wa ajabu na hakuna aliyejua tatizo lilikuwa nini, lakini walibaini kuwa
ni mama yake wa kambo ndiye alimroga kutokana na wivu.
Mukubwa aliyetamba na wimbo wa 'Mfalme wa Amani', anabainisha
kwamba aliugua kwa miaka mitatu na alihaha huku na huko hospitalini hadi kwa
waganga wa kienyeji kusaka tiba, lakini hakufanikiwa.
Kwa mantiki hiyo, alifikia uamuzi wa kukatwa mkono kwa vile
ulikuwa umeharibika.
Mukubwa anasema mama yake huyo wa kambo alikiri kumroga baada
ya kuokoka, hivyo alimsamehe. Hata hivyo, anasema mkono huo aliokatwa haumzuii
kumuimbia Mungu.
Mukubwa anasema alihamia Kenya kutokana na msaada wa mwimbaji
wa nyimbo za Injili, marehemu Angela Chibalonza, aliyekuwa mshauri wake.
Mukubwa amezaliwa kwenye familia ya watoto tisa, wanaume saba
na wanawake wawili, yeye akiwa wa kwanza, ameoa kwa alifunga ndoa na Betty
Japhet, Machi mwaka 2010.
Mwimbaji huyo wa nyimbo za kumsifu Mungu mwenye ulemavu wa
mkono mmoja, hivi sasa anatamba na albamu yake mpya ya Usikate Tamaa, ambayo
anaamini itamng'arisha katika tamasha hilo.
Nyimbo zilizomo kwenye albamu hiyo ya Usikate Tamaa ni
Usikate Tamaa, Mungu Wangu Nitetee, Niko na Yesu, Mke Si Nguo, Moyo Tukuza
Bwana, Chunga Ahadi Yako na Yesu Jina Zuri.
Mukubwa anayeishi Kenya, amewahi kutoa albamu mbili ambazo ni
Sijaona Rafiki na Mungu Mwenye Nguvu.
Sijaona Rafiki Kama Yesu ambayo ni albamu yake ya kwanza ina
nyimbo za Uwe Nami Bwana, Sijaona Rafiki Kama Yesu, Nitayainua Macho, Matendo
ya Mungu, Bwana Wastahili na Yesu Kimbilio.
Albamu yake ya pili ya Mungu Mwenye Nguvu ina nyimbo za Mungu
Mwenye Nguvu, Mkono wa Bwana, Mfalme wa Amani, Siku Moja, Tabia Ina Dawa na
Roho Yangu Ikuimbie.
Wengine watakaoshiriki
Mbali na Mukubwa, wengine waliothibitisha kushiriki tamasha
hilo litakalofanyika Sikukuu ya Pasaka ni Rose Muhando, Anastazia Mukabwa,
Upendo Nkone, Upendo Kilahiro, Christina Shusho, Atosha Kissava, Mwinjilisti
Faraja Ntaboba kutoka DRC na kundi la Glorious Celebration.
Pia kwaya mahiri ya Kinondoni Revival inayotamba na albamu
yao mpya ya Mtu wa Nne, inatarajia kutumbuiza katika tamasha la Pasaka. Mgeni
rasmi atakuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard
Membe.
Nyimbo zilizomo kwenye albamu ya Kinondoni Revival ni Mtu wa
Nne, Imekwisha, Chukua Hatua, Mtafuteni Bwana, New Season, Hakikisha,
Ninakushukuru na Dini Iliyo Safi.
Pia kwaya hiyo ya Kinondoni Revival imewahi kutamba na albamu
yao ya Kilio cha Mcha Mungu yenye nyimbo nane za Kilio cha Mcha Mungu, Kwanini
Unataka Kujiua, Ayubu II, Vumilia Kidogo, Nafsi Yangu, Natamani Kwenda
Mbinguni, Ndugu Yetu Twakutafuta na Twalilia Tanzania ambazo pia wameahidi
wataziimba.
Msama anasema baada ya waimbaji hao kutikisa Uwanja wa Taifa,
mashambulizi mengine yatahamia kwenye Uwanja wa Jamhuri, Dodoma Aprili 9 mwaka
huu.
Kiingilio katika tamasha hilo kimetengwa katika kategoria
tatu na kitakuwa sh. 2,000 kwa watoto, sh. 5,000 kwa viti vya kawaida na viti
maalumu sh. 10,000.
Tamasha la Pasaka la mwaka huu pia litashirikisha waimbaji wa
nyimbo za Injili kutoka nchi za Uganda, Rwanda, Afrika Kusini na Zambia. Pia
kutakuwa na kwaya na vikundi vya burudani.
0 comments:
Post a Comment