DORIS MALIYAGA (gazeti
la mwanaspoti)
TIBA ya tatizo la pumzi kwa Simba imepatikana baada ya timu
hiyo kufunga mabao yake katika dakika 19 za mwisho za mechi yao ya Kombe la
Shirikisho dhidi ya Entente Setif ya Algeria juzi Jumapili.Simba iliibuka na ushindi wa 2-0 katika mchezo huo uliochezwa Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam na kujiweka pazuri kabla ya mechi ya marudiano itakayochezwa huko Algeria.
Katika siku za karibuni, Simba ilikuwa na tatizo la stamina na lilidhihirika ilipotoa sare ya 1-1 na Kiyovu ya Rwanda kwenye mechi ya mtoano ya Kombe la Shirikisho hivi karibuni mjini Kigali, Rwanda.
Kiyovu walisawazisha bao hilo katika dakika ya 87 kupitia kwa Yusuph Ndayishimiye, lakini pia mechi ya marudiano jijini Dar es Salaam, Simba ilikuwa ikiongoza kwa 2-0, lakini Nelly Mayanja alipata nafasi dakika ya 77 na kufanya matokeo kuwa 2-1 na pia timu hiyo iliipa presha kubwa Simba.
Pia imekuwa na tatizo hilo kwenye mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara lakini hali ilikuwa tofauti kwenye mechi yao na Entente Setif.
Huku mashabiki wa timu hiyo wakiwa wameingiwa na hofu baada ya kushindwa kufungana katika kipindi cha kwanza, Simba ilifunga mabao yake katika kipindi cha pili.
Ilipata bao la kwanza katika dakika ya 71, likifungwa na Emmanuel Okwi na lile la pili likizamishwa na Haruna Moshi 'Boban' katika dakika ya 79.
Simba ilicheza vizuri katika kipindi cha pili tofauti na kipindi cha kwanza dhidi ya wapinzani wao Entente Setif, ambao wamewahi kuwa mabingwa wa Afrika mwaka 1988.
Hata hivyo, Simba walipoteza nafasi nyingi za wazi katika mchezo huo mkali.
Kocha Milovan Cirkovic alisema: "Tuligundua upungufu huo wa pumzi katika mechi zetu za awali, tukafanya marekebisho katika maandalizi yetu."
0 comments:
Post a Comment