KWA muda mrefu miaka ya karibuni mabeki wa pembeni imekuwa
ni tatizo nchini, na ndio maana Nsajigwa Shadrack amekosa upinzani kwenye beki
ya kulia tangu mwaka 2006.
Haruna Shamte alijaribu kutaka kupora namba ya
Nsajigwa,lakini akachemsha ila sasa Shomari Salum Kapombe kwa kasi anayokuja
nayo anaelekea kuleta mapinduzi ya kweli.
Huyu ni beki chipukizi wa timu ya taifa ya Tanzania na
Simba, anayemudu kucheza pia na nafasi za kiungo ambaye,anainukia vizuri
kisoka.
“Ninamudu kucheza nafasi zote pale kocha atakaponipanga
kwani mpira upo kwenye damu yangu,” anasema Kapombe katika mahojiano maalum na
DIMBA yaliyofanyika hivi karibuni jijini Dar es Salaam.
Ni mchezaji chipukizi ambaye anacheza beki kulia na kiungo,
kutokana na uhodari wake uwanjani, jina hili limekuwa maarufu sana, kwani
katika kikosi cha timu ya vijana chini ya miaka 23 na hata ile ya wakutwa, mchezaji huyo hakosekani,
na ndio maana amejizolea umaarufu mkubwa sana.Nyota ya Kapombe ilianza kung’ara
pale alipoitwa kwa mara ya kwanza
katika kikosi cha U-23 kilichokuwa kikiwania kufuzu michuano ya Olimpiki
na Mataifa ya Afrika, na kwenye mechi kadhaa za mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu
Bara iliyomalizika Novemba 3, akiwa na vinara wa ligi hiyo, Simba, hali
iliyomfanya kocha wa timu ya Taifa ‘Taifa Stars’ Jan Borge Poulsen avutiwe
naye.
Baada ya kuvutiwa na soka ya mchezaji huyo, Poulsen alimwita
katika kikosi chake kilichokuwa kikiwania kupangwa kwenye makundi ya kufuzu
Fainali za Kombe la Dunia, dhidi ya
Chad, mechi hiyo ilichezwa jijini
Nd’jamena, Novemba 11 na kurudiana siku nne baadaye jijini Dar es Salaam,
ambapo Stars walifanikiwa kuwaondoa Chad.
Kutokana na nahodha wa timu ya taifa, Taifa Stars, Nsajigwa
Shedrack kuwa majeruhi, kinda huyo alikuwa akicheza nafasi ya mkongwe huyo,
beki ya kulia.
Alicheza mechi zote dhidi ya Chad na michuano ya Kombe la
Tusker Challenge iliyomalizika mwezi huu, ambapo timu yake ya Tanzania Bara
ilishika nafasi ya nne.
Katika mahojiano maalumu na DIMBA Kapombe mwenye historia
ndefu katika medani ya soka, licha ya kuwa na umri mdogo, baada ya kutua Simba
msimu huu, amefanikiwa kupigana vilivyo na kula sahani moja na nyota kadhaa
wakongwe na wa kimataifa na kufanikiwa kucheza mechi karibu zote za mzunguko wa
kwanza.
Kapombe alizaliwa Januari 28 mwaka 1992, alihitimu elimu
yake ya msingi mwaka 2006 katika shule ya msingi Morogoro kabla ya kumaliza
elimu yake ya sekondari mwaka 2010 katika shule ya Lupamba mjini Morogoro.
Ni mtoto pekee ya kiume katika familia yam zee Salum yenye
watoto watatu, wakike wawili, yeye akiwa kitinda mimba.
“Mpira upo kwenye damu yangu, kwani nilianza kuupenda tangu
utotoni, na hivyo nikaanza kucheza mechi mbalimbali za mitaani ambako pia nilikuwa navuma sana,”
anasema Kapombe
.Anasema alianza kujitambua kama mwanasoka tangu akiwa
darasa la tatu, kipindi hicho alikuwa kwenye kituo cha Morogoro Youth Academy,
ambapo pia alikuwa akishiriki michuano mbalimbali ambayo ilikuwa ikiandaliwa na
kituo hichoKapombe anasema pia aliwahi kucheza na timu ya watoto wanaookota
miopira kwenye Uwanja wa Jamhuri Morogoro ambayo ilikuwa ikiitwa Jamhuri Ball Boys.
“Mimi nilikuwa ni muokota mipira pale Uwanjawa Jamhuri mjini
Morogoro, hapo ndipo utakapogundua kwamba mpira upo kwenye damu yangu, hapo
ndipo ikaundwa timu yetu sisi watoto waokota mipira ambayo iliitwa Jamhuri Ball
Boys.
“Timu nyingine ambazo nilichezea ni Mafiga Kids, Santos Fc, Jamhuri Ball Boys
mpaka nilipokuja kuonekana na kituo cha Moro Youth Academy, nilikuwa najituma
sana nikijua fika ipo siku nitakuja kufika mbali sana katika soka,” anasema.
Anasema katika timu ya
Jamhuri Ball Boys, U-14,alikuwa ni nahodha wa timu hiyo katika michuano
ya Winome Cup na michuano ya Serve Access Games ambapo
aling’ara sana.
Kapombe anasema mtu ambaye hata kuja kumsahau katika maisha
yake ya soka ni kocha wake Yahya Belin,
aliyekuwa akikinoa kikosi cha Jamhuri
Ball Boys, kwani ndiye aliyemsaidia kuinua kipaji chake.
Anasema kocha Belin,
alikuwa akimsihi acheze namba tofauti tofati uwanjani, ili siku ikitokea mmoja
wa wachezaji akiumia basi acheze yeye nafasi hiyo kuliko kumtegemea mchezaji
mmoja katika nafasi Fulani hivyo yeye akiwa kiraka.
Akiwa katika kituo hicho cha Moro Youth, baadaye alipanda
hadi kikosi cha U-17 cha kituo hicho, ambako aliweza kuchaguliwa kuwa nahodha
wa timu ya mkoa wa Morogoro iliyoshiriki michuano ya Copa Coca-Cola 2008,
wakati huo akiwa na miaka 16.
Anasema katika mashindano hayo walitolewa hatua ya robo
fainali na Kigoma ambayo ilikuja kuwa mabingwa.
Kapombe anasema uhodari mkubwa aliokuwa akiuonyesha katika
michuano hiyo faida yake alikuja kuiona baadaye baada kuchaguliwa wachezaji
nyota wakati huo ilikuwa ni mwaka 2008, na walitakiwa kwenda nchini Brazil,
katika mkoa wa Morogoro walichaguliwa wawili yeye pamoja na Zahoro Zeiran.
Baada ya kumalizika kwa michuano hiyo, Kapombe anasema
alirudi katika kituo chake cha Morogoro ambako alijiunga na kikosi cha timu B
cha Polisi Dodoma mwaka 2007, ambapo 2009 alipandishwa timu ya wakubwa.
Kapombe anasema baada ya timu ya Polisi Moro kushuka daraja
alikuwa akiitumikia timu hiyo katika mashindano ya Ligi Daraja la Kwanza.
“Nakumbuka siku hiyo tulikuwa tunacheza na Arusha, katika
mchezo huo kocha Jamhuri Kikwelu ‘Julio’ alikuwepo, hivyo alivutiwa na uwezo
wangu na kunichagua katika timu ya taifa ya Vijana wenye umri chini ya miaka
23.
Anaongeza kuwa akiwa katika kikosi cha timu ya vijana
alikuwa akiongeza bidii kila kukicha, na alijituma zaidi katika michuano ya
kimataifa ya All African Games na Olimpiki ambapo aliweza kucheza mechi zote,
nyumbani na ugenini, ikiwemo na timu za Cameroon, Nigeria na Uganda, hali
ambayo ilizidi kumuongezeav uwezo zaidi na kujiamini.
“Nashukuru Mungu Simba walivutiwa na uwezo wangu, hivyo
msimu huu walinisajili katika kikosi chao, ambapo nimezidi kung’ara zaidi na
hivyo kuwavutia makocha wangu wa Simba na wale wa timu za taifa.
Anasema, baada ya kujiunga na Wekundu hao, furaha yake
ilizidi pale alipokabidhiwa jezi namba 15 na kuwa miongoni mwa wachezaji 18 wa
kikosi cha kwanza cha kutumainiwa cha aliyekuwa Kocha Mganda, Moses Basena.
Kapombe anasema anafuraha zaidi kwani kocha wa Simba wakati
huo, Mganda Moses Basena alivutiwa naye na hivyo akamchagua katika kikosi cha
kwanza, hali ambayo anasema imempa changamoto kubwa katika maisha yake ya soka.
“Kwanza nimecheza mechi zote 13 za mzunguko wa kwanza za
Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, hivyo inaonyesha kabisa uwezo wangu upo juu
sana,” anasema.
Jambo ambalo Kapombe anasema hata kuja kusahau katika maisha
yake, ni mwaka 2002 alipofiwa na mama yake mzazi, Bi.Ester Shomari.
“Kwakweli kila nikikumbuka huwa nalia sana, kwani alikuwa ni
kipenzi change, ikizingatiwa mimi nilikuwa ni kitinda mimba wake,” anasema.
Kapombe analishauri Shirikisho la SokaTanzania (TFF), kuwa
na shule za michezo nyingi ili kukuza vipaji vya watoto.
“Shule za michezo zinasaidia sana kwani kuna watoto wengi
sana ambao wanavipaji, lakini hawana pa kuvionyesha,” anasema.
WASIFU WAKE:
JINA KAMILI: Shomari Salum Kapombe.
KUZALIWA: Januari 28, 1992 (Miaka 19)
ALIPOZALIWA: Morogoro.
KLABU YAKE: Simba
Mwaka Klabu
2007-2009 Polisi
Dodoma
0 comments:
Post a Comment