KUANZIA sasa Shirikisho la soka Tanzania (TFF) litawajibika
kulipa kiasi cha shilingi milioni 10 kwa uharibifu wa idadi yoyote ya viti
utakofanywa kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar
es Salaam .
Hatua hiyo inafuatia kukithiri kwa uharibifu wa viti hivyo
ambao umekuwa ukifanywa na mashabiki wa soka hapa nchini na hasa wa Vilabu vya
Simba na Yanga.
Akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Habari, Vijana,
Utamaduni na Michezo, mkurugenzi wa Idara ya Michezo nchini Leonard Thadeo
alisema kwamba lengo la kufanya hivyo ni kudhibiti vitendo vya uharibifu wa
viti katika Uwanja huo.
Thadeo aliongeza kuwa uharibifu huo umekuwa ukifanyika mara
kwa mara na serikali imekuwa ikilazimika kufanya matengenezo bila kuwahusisha
wadau wengine lakini inaonekana kujengeka kuwa tabia miongoni mwa baadhi ya
mashabiki hatua ambayo haiwezi kuvumilika.
“Inasikitisha kuona hata baadhi ya viongozi wa vilabu vyetu
hawatambui kuwa wanawajibu wa msingi kama
viongozi kuwaelimisha wanachama na
wapenzi wa vilabu vyao kuacha uharibifu badala yake wanadai kuwa viti vingi
viliharibika,kaharibu nani? alihoji Thadeo.
Alisema sasa hivi dunia ni sawa na kijiji na wakati mataifa
mengine yalikuwa yameanza kuisifia Tanzania kwa kujenda Uwanja wa kisasa na wa
kimataifa, kudumisha amani na kutekeleza mambo kistaarabu, lakini vurugu hizo
zinaweza kutia doa sifa zote hizo.
“Viongozi tutambue
wajibu wetu kwa tunaowaongoza na wizara haitasita kufunga uwanja endapo tabia
hiyo itaendelea...ili tusifikie hatua hiyo, tunawaomba wapendamichezo na
Watanzania wote tushirikiane, tuhamasishane na kuelimishana kushangilia timu
zetu kwa amani na utulivu,”Aliongeza Thadeo.
Hivi karibuni Serikali ilitaka TFF kulipa jumla ya shilingi
milioni kumi kufuatia mashabiki kuahribu viti katika mechi ilizozihusisha timu
za Simba na Yanga kwa nyakati tofauti ambapo kulitokea uharibifu wa viti
ulioafanywa na mashabiki wa timu hizo.
Kufuatia hali hiyo TFF iliamua kuikata Simba shilingi
milioni tano kwa madai kuwa mashabiki wake walifanya uharibifu huo katika mechi
yao dhidi ya Kiyovu ya Rwanda kabla ya kuikata Yanga kiasi kama hicho
kutokana na uharibifu uliofanywa katika mechi yao ya ligi kuu dhidi ya Azam.
0 comments:
Post a Comment