Del Piero |
MKONGWE Alessandro Del Piero alitokea benchi na kuisaidia Juventus
kushinda 2-0 dhidi ya Inter Milan katika Serie A jana, kikosi hicho cha Antonio
Conte kikiwatia presha vinara wa ligi hiyo Kuu Italia, AC Milan.
Inter walimuachia mwanya wa kutosha Martin Caceres kuuchupia
mpira na kupiga kmichwa kuifungia Juventus bao la kwanza dakika ya 57 na Del
Piero—ambaye pia alifunga katikati ya wiki dhidi ya AC Milan kwenye Kombe la
Ligi, alifunga la kuhitimisha ushindi dakika ya 70.Kipa wa Juventus, Gianluigi Buffon aliokoa michomo mingi ya hatari.
Milan, ambayo iliifunga Roma 2-1 juzi, inaongoza ligi ikiwazidi Juventus kwa pointi nne, lakini Del Piero, akiwa katika msimu wake wa mwisho Juve baada ya kuichezea kwa miaka 19, amewataka wachezaji wenzake kutokata tamaa.
Inter imeporomoka hadi nafasi ya nane, ikiwa imeshinda mechi moja tu kati ya mechi zake 10 zilizopita za ligi.
Katika mechi nyingine, Catania ilitoka nyuma na kupata sare ya 2-2 na Napoli kwa mabao ya dakika lala salama ya Nicolas Spolli na Davide Lanzafame aliyetokea benchi.
Mabao ya Napoli yalifungwa na Blerim Dzemaili na Edinson Cavani kipindi cha pili.
Sare hii ni pigo kwa Napoli inayowania nafasi ya tatu, hususan baada ya bao la dakika za lala salama la Modibo Diakite kuipa ushindi wa 1-0 Lazio dhidi ya Cagliari.
Lazio sasa ni ya tatu, ikiwazidi pointi tatu Udinese na Napoli.
Novara ililazimishwa sare ya bila kufungana na Lecce, ambayo inapigana kuepuka kushuka daraja|.
Cesena ilitoka 2-2 na Parma na Genoa pia ilitoka 2-2 na Fiorentina, Chievo Verona ilitoka 1-1 na Siena wakati Atalanta iliipiga Bologna 2-0.
0 comments:
Post a Comment