Rebecca |
MALKIA wa muziki wa Injili nchini Afrika Kusini, Rebecca
Malope, naye atakuwa miongoni mwa waimbaji watakaopamba tamasha la nyimbo za
Injili litakalofanyika Aprili 8 mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es
Salaam.
Mwenyekiti wa Kamati inayoratibu tamasha hilo chini ya
Kampuni ya Msama Promotions ya Dar es Salaam, Alex Msama, alisema Rebecca
amethibitisha kushiriki tamasha hilo.
Msama alisema Rebecca ataungana na waimbaji wa muziki wa
Injili kutoka nchi jirani za Zambia, Kenya, Jamhuri ya Kidemokrasia na Congo
(DRC), Rwanda na Uganda.
Malope atakuwa mmoja kati waimbaji siku hiyo wakiwemo Rose
Muhando, Christina Shusho, Upendo Nkone, Upendo Kilahiro, Solomon Mukubwa,
Ephraim Sekeleti, Anastazia Mukabwa, Atosha Kissava na kundi la Glorious
Celebration.
Pia kwaya mahiri ya Kinondoni Revival inayotamba na albamu
yao mpya ya Mtu wa Nne, inatarajia kutumbuiza katika tamasha la Pasaka na
Mwinjilisti Faraja Ntaboba kutoka DRC.
Mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe. Baada ya kutikisa Uwanja wa Taifa,
mashambulizi mengine yatahamia kwenye Uwanja wa Jamhuri, Dodoma Aprili 9 mwaka
huu.
"Katika tamasha la Pasaka mwaka huu, Rebecca Malope
atapata fursa ya kuimba nyimbo mbalimbali zilizomo kwenye albamu zake,"
alisema Msama.
Rebecca amewahi kutamba na albamu za Saturday Nite (aliyoitoa
Januari 1, 2009), Hlala Nami (Novemba 11, 2003), Siyabonga (Desemba 21, 2000),
Free at Last (Novemba 18, 1997), African Classics (Mei 5, 2009) na Greatest
Hits (Januari 10, 2006).
"Bado tunaendelea na mazungumzo na waimbaji wengine
mahiri wa muziki wa Injili, lakini Rebecca atakuwepo akishirikiana na wengine
mahiri kama Rose Muhando, Solomon Mukubwa na wengineo," alisema Msama.
Tamasha la mwaka huu malengo yake makubwa ni kuchangisha
fedha kwa ajili ya kuwasomesha watoto yatima na kuwasaidia mitaji wanawake
wajane.
Kiingilio katika tamasha hilo kimetengwa katika kategoria
tatu na kitakuwa sh. 2,000 kwa watoto, sh. 5,000 kwa viti vya kawaida na viti
maalumu sh. 10,000.
Rebecca Malope ni mwimbaji nguli wa Afrika Kusini aliyetamba
zaidi kimataifa mwishoni mwa miaka ya 90.
Malope alizaliwa katika shamba la tumbaku Afrika Kusini.
Akiwa mtoto, yeye na dada zake walikuwa wakiimba kwaya kanisani.
Alijiunga na kundi la muziki wa injili akiwa binti mwenye
umri mdogo, jijini Johannesburg, chini ya mtozi, Zizwe Zakho.
Alianza kutoa albamu yake ya kwanza aliyoipeleka Marekani
mwaka 1996 na mwaka uliofuata alisaini mkataba na EMI kisha akatoa albamu ya
Free At Last.
0 comments:
Post a Comment