KWA nini Redondo? Ni soka
yake maridadi tangu akiwa kinda, akicheza chandimu kwenye vichochoro vya mitaa
ya Keko Magurumbasi, wilayani Temeke, Dar es Salaam ilimfanya afananishwe na
kiungo wa zamani wa kimataifa wa Argentina, Fernando Carlos Redondo Neri.
Leo anacheza Ligi Kuu ya
Vodacom Tanzania Bara, lakini ni kinyume kabisa cha ndoto zake, kwa nini?
“Bila kurudishwa nchini kwa
kukosa kibali sasa hivi ningekuwa Norway nacheza mpira, ” anasema Ramadhan
Suleiman Chombo ‘Redondo’ katika mahojiano na DIMBA wiki hii.
Kiungo huyo ambaye alikuwemo
kwenye kikosi cha timu ya Tanzania Bara ‘Kilimanjaro kilichokuwa kinashiriki
michuano ya CECAFA Tusker Challenge, anasema ataendelea kucheza kwa kujituma
katika timu yake ya Azam FC ili aone faida ya mpira hapo baadaye.
“Wengi wanapenda kusema kuwa
ndoto zao za baadaye ni kuwa mchezaji wa kulipwa, hilo sikatai hata mimi
napenda kuwa hivyo, lakini pia nataka kuona mpira utanipa nini katika maisha
yangu hasa nitakapostaafu kucheza,” anasema Redondo.
Akielezea historia yake ya
soka, Redondo anayemudu kucheza nafasi ya kiungo na winga kulia na kushoto,
anasema anakumbuka ilikuwa ni mwaka 2000 alipokuwa kwenye kituo cha Dar es
Salaam Youth Olimpic Centre, wakati huo timu yao ilienda Sweden kwenye
mashindano ya vijana.
“Wakati huo ndio nilikuwa
natoka kumaliza elimu yangu ya msingi, nilishindwa kuendelea na masomo kwani
nilikuwa napenda sana mpira hivyo ningeshindwa kusoma, baada ya kumaliza eilimu
ya msingi timu yetu ilikwenda Sweden, bahati nzuri tukatwaa ubingwa wa Gothia
nchini humo baada ya kuwafunga Rusia katika fainali,” anasema
Kiungo huyo anasema michuano
hiyo iliyokuwa ikishirikisha nchi mbalimbali yalijulikana kama Gothia, na timu
yao ilikuwa ni tishio sana kwa nchi mbalimbali zilizoshiriki michuano hiyo na
bahati nzuri wakachukua ubingwa.
Redondo ambaye wiki iliyopita
alisherehekea siku yake ya kuzaliwa sambamba na sherehe za miaka 50 ya Uhuru
(Redondo alizaliwa Desemba 9 mwaka 1987, anasema anakumbuka ilikuwa mwaka 2002
wakati timu yao ya vijana Dar es Salaam Youth Olimpic Centre ilipokwenda kwenye
michuano mingine nchini Norway, anasema aliwahi kuzamia nchini humo.
“Nilizamia Norway kuanzia
mwaka 2003 hadi 2007 nilikuwa nikichezea timu ya Lyngdal iliyokuwa ikishiriki
daraja ya pili nchini humo, bahati mbaya katika msako ikabainika kwamba sina
kibali cha kuishi nchini humo, hivyo nikarudishwa hapa Tanzania,” anasema
Anasema alirudi nchini
mwanzoni mwa mwaka 2007, baada ya kutoka
Norway akawa anacheza Ligi ya TFF kinondoni katika timu ya Tambaza, mwaka huo
huo akajiunga na timu ya Ashanti United iliyokuwa ikishiriki Ligi Kuu ya
Vodacom Tanzania Bara ambayo alicheza nusu msimu na 2008 akasajiliwa na Simba.
“Unajua mpira ni malengo na
ili uwe mchezaji mzuri ni lazima ufuate misingi bora ya soka, hapo ndipo utakapotimiza
ndoto zako, hasa kama unajua kuwa mpira ndio ajira yako ya kudumu,” anasema.
Redondo anasema alidumu
katika timu ya Simba tangu 2008 hadi 2010 aliposajiliwa na Azam FC ambayo ndio
anaichezea hadi sasa.
Katika siku ambazo Redondo
anasema hata kuja kusahau katika maisha yake ni pale alipopata ajali ya
pikipiki siku ya Simba Day, anasema alikuwa akitokea kambini siku hiyo walikuwa
wanacheza na timu ya URA ya Uganda.
“Ilikuwa ni mwaka 2008 siku
ya Simba Day na mimi nilipanga kuonyesha vitu adimu katika mechi yetu na URA,
lakini bahati mbaya sikuweza kucheza na tulifungwa na timu hiyo bao 1-0, siku
hiyo huwa siisahau maishani mwangu,” anasema.
Redondo anasema alikaa nyumbani
mwezi mmoja kwani aliumia kiuno hivyo daktari akamtaka apumzike mwezi mzima kwa
ajili ya matibabu ndio arejee tena uwanjani.
Anaishauri nini TFF?
“Wawe na maandalizi ya muda
mrefu kwa timu pindi yanapokaribia
mashindano mbalimbali kwani itasaidia kuwa na timu nzuri ya kiushindani, mbali
na hilo pia wazisaidie klabu zinazoshiriki Ligi Kuu ili ziweze kupata wadhamini
kwani kuna timu ambazo hazina wafadhili na zimekuwa zikishindwa kujiendesha
zenyewe,” anasema.
Anasema TFF wajaribu kuongea
na makampuni mbalimbali ili yaweze kuzisaidia timu ambazo hazina uwezo, kwani
nyingi zinashindwa kuleta upinzani kwa saababu hazina uwezo.
“Kila siku tutakuwa
tukishuhudia upinzani kwa timu za Simba, Yanga, Azam FC na zile za majeshi kwa
kuwa ndizo zinazoweza kujiendesha, na ili soka liwe na ushindani mkali timu
hizi ambazo hazina wafadhili zitafutiwe ili ligi iwe na upinzani kwa kila
timu,” anasema.
Akizungumzia matatizo ambayo
wachezaji wengi wamekuwa wakikumbana nayo, anasema kwanza kabisa ni viwanja,
anasema mikoa mingi viwanja vyao ni vibovu hivyo wanapotakiwa kucheza mechi
mikoani huwa wanakumbana na tatizo hilo.
“Pia utakuta mechi ni
keshokutwa, timu inasafiri leo kutoka Dar es Salaam kwenda Bukoba tena kwa
basi, hivyo mchezaji akifika anakuwa amechoka na safari na hata uwanjani hawezi
kujituma vizuri,” anasema.
Redondo anasema lakini kuna
timu ambazo zinauwezo kama kuna mechi sehemu ya mbali wanapanda ndege hivyo
hata akifika anakokwenda hawezi kuwa na uchovu kama yule aliyepanda basi.
Wachezaji ambao Redondo anasema
wanamvutia kwa hata Tanzania ni viungo Haruna Niyonzima, Haruna Moshi ‘Boban’
Mwinyi Kazimoto na Nurdin Bakari.
“Wapo wengi zaidi ya hao,
lakini hao ndio nawapa nafasi kubwa kwa hapa Tanzania,” anasema.
WASIFU WAKE:
JINA: Ramadhan Suleiman
Chombo
JINA LA UTANI: Redondo
KUZALIWA: Desemba 9, 1987
(miaka 24)
ALIPOZALIWA: Dar es Salaam
NAFASI: Kiungo/winga
KLABU YAKE: Azam FC
Mwaka Klabu
2000-2002
DSM
Youth Olimpic Centre (kituo)
2003-2006
Lyngdal
(Norway)
2007 Ashanti United
2008-2010 Simba
Tangu 2010:
Azam FC
0 comments:
Post a Comment