Nsa aliyebinuka tik tak enzi zake akiwa Yanga |
MSHAMBULIAJI wa zamani wa Yanga, Nsa Job ameendelea kufunga
mabao Ligi Kuu ya Bara, baada ya jana pia kuifungia timu yake, Villa Squad
katika ushindi wa 2-1 dhidi ya Moro United, Uwanja wa Chamazi.
Kwa matokeo hayo, Villa imepanda kutoka nafasi ya mwisho
mkiani hadi nafasi ya 12 na kuishusha Moro United kwa nafasi moja.
Villa imefikisha pointi 19 na Moro 18, nafasi ya 14 sasa
inashikiliwa na Polisi Dodoma yenye pointi 17.
Timu hizo tatu zinapigania 'uhai' wa kubaki kwenye ligi hiyo
kwani zipo kwenye hatari ya kushuka daraja.
Bao la Moro United lilifungwa na Rajab Zahir katika dakika
ya 44.
Mabao ya Villa yalifungwa na Nsa katika dakika ya 23 na
Omari Issa dakika ya 90.
Katika mchezo mwingine, Mtibwa Sugar jana ilichezea kichapo
ugenini kwenye uwanja wa Mabatini Mlandizi baada ya kuchapwa mabao 3-1 na Ruvu
Shooting.
Matokeo hayo yameifanya Mtibwa iendelee kubaki nafasi ya nne
kwenye msimamo wa ligi hiyo ikiwa na pointi 34, huku Ruvu Shooting ikibaki
nafasi ya nane baada ya kufikisha pointi
27.
Katika mechi hiyo iliyokuwa ya vuta nikuvute Ruvu ilipata
mabao yake kupitia kwa Hassan
Dilunga aliyefunga mawili dakika ya 34 na 47 na Mohamed
Kijuso alifunga katika dakika ya 43.
Kwa upande wa Mtibwa Sugar ilipata bao lake la kufutia
machozi kupitia kwa Thomas Mourice
dakika ya 90.
Ligi hiyo inatarajiwa kuendelea tena mwishoni mwa wiki hii
ambapo vigogo wa soka nchini
Simba na Yanga watakuwa kwenye viwanja viwili tofauti
kuendeleza mbio za kuwania ubingwa.
Yanga inayotetea ubingwa itakuwa ngeni wa Coastal Union
kwenye uwanja wa Mkwakwani
Tanga na Simba itakuwa kwenye uwanja wa Taifa Dar es Salaam
ikiikaribisha African Lyon.
0 comments:
Post a Comment