SHIRIKISHO la Soka Afrika (CAF) limewateua waamuzi kutoka
Rwanda kuchezesha mechi ya kwanza ya raundi ya kwanza kuwania Kombe la
Shirikisho kati ya Simba na ES Setif itakayochezwa Machi 25 mwaka huu.
Mwamuzi wa kati ni Hudu Munyemana wakati wasaidizi wake ni
Felicien Kabanda, Theogene Ndagijimana na Edouard Bahizi. Kamishna wa mechi
hiyo ni Felix Tangawarima kutoka Zimbabwe.
Mechi hiyo namba 45 itafanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam
kuanzia saa 10 kamili jioni. Mechi ya marudiano ambayo ni namba 46 itachezwa
Aprili 6 mwaka huu nchini Algeria.
Iwapo Simba itafanikiwa kusonga mbele itacheza mechi ya
kwanza nyumbani Aprili 29 mwaka huu na mshindi kati ya El Ahly Shandy ya Sudan
na Ferroviario de Maputo ya Msumbiji ambapo ya marudiano itachezwa kati ya Mei
11, 12 na 13 mwaka huu.
Wakati huo huo: Semina elekezi kwa ajili ya mashindano ya
Copa Coca-Cola 2012 itafanyika Machi 25 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es
Salaam ambapo washiriki ni makatibu wakuu wa vyama vya mpira wa miguu vya mikoa
au wawakilishi wao ambao wanatakiwa kuwa na utambulisho rasmi.
Washiriki kutoka nje ya Mkoa wa Dar es Salaam wanatakiwa
kuwasili Machi 24 mwaka huu na watapokelewa katika hoteli ya Itumbi iliyoko
Magomeni-Mwembechai.
TFF itawagharamia washiriki kwa chakula, malazi na nauli za
kuja Dar es Salaam na kurudi kwa usafiri wa basi au meli.
Michuano ya mwaka huu itaanza Machi 31 hadi Mei 5 katika
ngazi ya wilaya. Usajili kwa ngazi ya mkoa utaanza Mei 6 hadi 15 wakati
mashindano yake yatafanyika kuanzia Mei 16 hadi 25.
Usajili na maandalizi kwa michuano ya ngazi ya Taifa utaanza
Mei 26 hadi Juni 7. Usajili wa timu za mikoa unatakiwa kuwasilishwa Shirikisho
la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kati ya Juni 8 na 14 mwaka huu.
0 comments:
Post a Comment