“MWANAMKE kucheza mpira watu wasichukulie kama ni uhuni, ni
kazi kama zilivyo kazi nyingine, na mimi sitarudi nyuma, nitazidi kusonga mbele
zaidi”.
Ndivyo alivyoanza kuzungumza, mshambuliaji wa timu ya taifa
ya wanawake Tanzania, Twiga Stars, Mwanahamisi Omary Sharuwa, ambaye pia
anachezea klabu ya Mburahati Queens.
Mwanahamisi, aliyepachikwa jina Gaucho kutokana na uchezaji
wake, akifananishwa na mwanasoka bora wa zamani wa dunia, Ronaldinho Gaucho, ni
mchezaji tegemeo wa Mburahati Queens na timu ya taifa, na labda ni maradhi tu
yanayoweza kumuweka nje ya kikosi cha kwanza cha Twiga, au Mburahati.
Uwezo mkubwa wa kusakata kandanda alionao mshambuliaji huyo wa
Mburahati Queens na Twiga Stars, Mwanahamisi Omary uliwahi kuzua utata Machi
mwaka jana, katika mechi ya Ligi ya wanawake
Dar es Salaam iliyofanyika kwenye Uwanja wa Karume na kushuhudia
Mwanahamisi akifunga mabao saba peke yake na kuiwezesha Mburahati Queens
kushinda mabao 10-1 dhidi ya Uzuri Queens.
Uwezo wake mkubwa wa kupiga chenga, kasi na kufunga mabao
zaidi ya matatu katika kila mechi aliyokuwa akicheza katika ligi hiyo,
uliwafanya mashabiki wanaofika uwanjani hapo kushuhudia soka la wanawake kudai
kuwa huenda mchezaji huyo ana jinsia mbili na kwamba yawezekana kuwa jinsia ya
kiume ndiyo yenye nguvu zaidi hivyo kumfananisha na mwanariadha mahiri nchini
Afrika Kusini, Caster Semenya.
Katika tukio ambalo halitakuja kusahaulika kwa mashabiki wa kandanda nchini, ni pale
mchezaji huyu alipokuwa ni mmoja wa wafungaji wa bao kati ya mawili
waliyoifunga Namibia katika kampeni za kusaka tiketi za kufuzu kwa fainali za
wanawake za Afrika.
Wakiwa ugenini huko Windhoek nchini Namibia, timu ya Taifa
ya wanawake ya Twiga Stars iliweza kuondoka na pointi zote tatu muhimu baada ya
kuwachapa wenyeji wao kwa mabao 2-0. Huku wakicheza kwa kujiamini na umahiri
mkubwa, kinadada hao wa Tanzania waliweza kujiweka vyema kwenye duru ya kwenda
kucheza fainali ya Mataifa ya Afrika kwa upande wa wanawake, bao lingine
lilifungwa na Asha Rashid, maarufu kama Mwalala.
Katika mahojiano yake maalumu aliyoyafanya na DIMBA hivi
karibuni, Mwanahamisi ‘Gaucho’ anasema hakuna kitu ambacho kinamsikitisha kwa
baadhi ya mashabiki kuchukulia soka la wanawake kama uhuni.
“Mimi nasema naomba mashabiki waone mpira kwa wanawake ni
kitu cha kawaida, nchi nyingi za wenzetu
zinauthamini sana mpira wa wanawake, hivyo na Tanzania inatakiwa tuuige
utamaduni huo.
“Wengine huwa wanatuona kama madume, jamani sisi wanawake
kama wengine ni mpira tu ndio unaotufanya tuwe hivi, lakini hakuna kitu kingine
chochote, mpira kwetu ni kama jeshini tu, kwani jeshini watu wote ni sawa,”
anasema Gaucho.
Gaucho aliyezaliwa mwaka 1992 mkoani Tanga na kupata elimu
yake ya msingi Pangani Tanga, anasema alianza kupenda soka tangu akiwa shuleni,
na hata alipomaliza masomo yake ya msingi, moja kwa moja akajikita katika soka.
“Nakumbuka nilikuja Dar es Salaam kwa mama yangu mdogo na
baba mdogo, siku hiyo nikaenda kuangalia mechi za wanawake katika Uwanja wa
Benjamini Mkapa, nilipoiona timu ya Mburahati Queens nikavutiwa nayo.
“Baada ya mchezo wao kumalizika nikazungumza na kocha wao,
ambaye aliniomba niungane nao, wakati huo nilikuwa na umri wa miaka 15 tu,
lakini uwezo niliokuwa nao ulimvutia sana kocha wangu, hivyo akaniweka katika
kikosi cha kwanza,” anasema.
Anasema siku za mwanzo alipojiingiza katika soka, walezi
wake walimkataza kucheza, lakini yeye akawa anajiiba hivyo hivyo, wazazi wa
Gaucho wote wawili walifariki, hivyo akawa analelewa na mama yake mdogo na baba
mdogo.
“Nilikuwa nikijiiba tu kucheza, kwa kweli mwanzo ulikuwa
mgumu, lakini baadaye ilibidi waniachie tu, kwani waligundua kuwa nilikuwa
nikicheza kwa kificho, lakini kwa sasa wananipa ushirikiano mkubwa, hivyo baada
ya kufanya mazoezi na Mburahati Queens kwa kificho hatimaye nikasajiliwa
rasmi,” anasema.
Anasema tangu siku hiyo akawa mchezaji wa Mburahati Queens,
wakati huo ilikuwa ni mwaka 2003, na akiwa katika timu hiyo ndani ya mwaka huo
akaitwa kwenye timu ya taifa akiwa na umri huo huo wa miaka 15, huku wenzake
wakiwa na umri mkubwa kidogo.
Baada ya kuitwa katika timu ya taifa, anasema aliongeza
bidii uwanjani na ndio maana hadi leo makocha wamekuwa wakimtegemea katika
kikosi cha kwanza katika timu yake ya taifa na klabu yake ya Mburahati Queens.
Anasema malengo yake katika soka ni kufika mbali, lakini
wasiwasi wake ni kwamba ndoto zake zitashindwa kutimia kwa kuwa timu nyingi za
wanawake hazina wafadhili, kitu ambacho kinawaangusha.
“Sio katika klabu tu kwani hata timu yetu ya taifa haina
wafadhili zaidi ya kuwategemea TFF tu (Shirikisho la Soka Tanzania), lakini
kama wangekuwa na wafadhili wangefika mbali sana,” anasema.
Gaucho atakumbukwa kwa mengi
hata katika michuano ya Shirikisho la Soka Kusini mwa Afrika (COSAFA).
Katika mechi yao na Botswana iliyochezwa kwenye Uwanja wa
Gwanzura jijini Harare, Zimbabwe, Twiga walishinda mabao 3-1 na waliong’arisha
mechi hiyo alikuwa ni Gaucho aliyetupia nyavuni mabao 2 na Fatuma Mustafa ‘Kitu
Nini’ alifunga moja.
Pia katika michuano hiyo Twiga walipocheza na Afrika Kusini,
walitoa sare ya mabao 2-2, na aliyesawazisha bao la pili ni Gaucho, ni mchezaji
ambaye ana uchu na mabao pindi timu yake inapocheza.
Pia Mei mwaka 2010 timu hiyo ilipokuwa ikicheza mchezo wa
kutafuta tiketi ya kufuzu kwa fainali za Mataifa ya Afrika kwa wanawake,
iliwahi kutoa kipigo cha mbwa mwizi kwa Eritrea mabao 8-1, kati ya mabao hayo
Gaucho alifunga manne. Akizungumzia mechi yao ya marudiano dhidi ya Namibia
itakayochezwa Dar es Salaam leo, Gaucho anasema kama waliweza kushinda ugenini,
bila shaka hata nyumbani wataleta raha, na kwa kushirikiana na wachezaji
wenzake anaamini hilo litawezekana.
“Muhimu ni mashabiki kujitokeza kwa wingi uwanjani ili
kutupa sapoti, kwani ugenini tulicheza tukiwa wakiwa, hivyo mechi ya marudiano
tunaomba sapoti kutoka kwa Watanzania,” anasema.
Twiga inahitaji hata sare leo ili kusonga mbele katika
kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Mataifa ya Afrika kwa Wanawake, kwani
katika mchezo wa kwanza ilishinda 2-0 ugenini.
Wachezaji wanaomvutia kwa Tanzania ni Mrisho Ngassa wa Azam
FC na Cristiano Ronaldo wa Real Madrid ya Hispania.
Katika tukio ambalo anasema hatakuja kusahau katika maisha
yake, ni mwaka 2003 alipoitwa katika timu ya taifa ya wanawake, Twiga Stars, kwani alikuwa na
umri mdogo sana wa miaka 15, hivyo kwake lilikuwa ni tukio la aina yake.
“Tukio hilo kwangu huwa ni la kukumbukwa sana, kwani
sikuwahi kuota kama ipo siku nikiwa na umri mdogo kama ule ningeitwa kwenye
timu ya taifa,” anasema.
Gaucho amewaomba watu wenye uwezo wazisaidie na timu za soka
za wanawake, kama ilivyo kwa timu za kiume, anaamini kama watapata wafadhili
watafika mbali sana, na watatoa burudani nzuri sana kwa mashabiki wa soka
nchini.
Kuhusu maisha yake binafsi, Gaucho huyo wa Mburahati anasema
kwamba hana mume wala mtoto, lakini ana rafiki wa kiume, ambaye hata hivyo
anasema hataki kumuanika- hiyo ni siri yake na huyo ni mwandani wake.
Naam, huyo ndiye Mwanahamisi Omary Sharuwa au Gaucho, binti
wa Mburahati anayeibeba Twiga Stars kwenye michuano ya kimataifa.
Je, leo ataendelea kung’ara na jezi za bendera ya nchi? Bila
shaka hilo ni jambo la kusubiri na kuona jinsi mambo yatakavyokuwa pale Taifa.
WASIFU WAKE:
JINA: Mwanahamisi Omary Shuruwa
KUZALIWA: Desemba 12, 1992 (miaka 20)
ALIPOZALIWA: Tanga
KLABU YAKE: Mburahati Queen
KLABU ALIZOCHEZEA:
Mwaka Klabu
2003
Mburahati Queen
0 comments:
Post a Comment