Muamba |
KIUNGO Fabrice Muamba, wa klabu ya Bolton Wanderers, yumo
katika hali mahututi baada ya kuzimia Jumamosi katika mechi ya raundi ya tano
ya Kombe la FA dhidi ya Tottenham.
Mchezaji huyo anaendelea kupata matibabu katika hospitali
inayohusika zaidi na magonjwa ya kifua, London Chest Hospital.
Madaktari walijaribu kumsaidia kuvuta pumzi kwa kipindi cha
dakika 10 mara tu alipozimia uwanjani, lakini hayo yaliposhindikana, ilibidi
akimbizwe hospitali.
"Bolton Wanderers inathibitisha kwamba Fabrice Muamba
amelazwa katika kituo cha mshituko wa moyo cha London Chest Hospital na akiwa
katika hali mahututi", ilieleza taarifa ya pamoja iliyotolewa saa 2130 GMT
Jumamosi kutoka kwa klabu ya Bolton na vile vile hopitali hiyo.
"Hakuna maelezo zaidi ambayo yatatolewa wakati huu.
Klabu na vile vile hospitali vinatoa mwito kwa vyombo vya habari na umma
kuiheshimu familia yake wakati huu na kuwapa nafasi katika kushughulika na
suala hili".
Mechi hiyo ya Kombe la FA kati ya Tottenham na Bolton
Wanderers ilisimamishwa ghafula baada ya Fabrice Muamba kuzimia ghafula.
Madaktari walijaribu kwa dakika 10 kumfanya mchezaji huyo
mwenye umri wa miaka 23 aweze kupumua, na hilo liliposhindikana, ilimlazimu
mwamuzi Howard Webb kusimamisha mchezo.
Mwandishi wa BBC Radio 5, Ian Dennis, alielezea kwamba
mchezaji huyo inaelekea alikuwa katika hali ya taabani.
Mchezo ulikuwa ni sare ya 1-1 wakati mechi iliposimamishwa
katika dakika ya 41.
Muamba alizaliwa tarehe 6 Aprili mwaka 1988 mjini Kinshasa,
Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, na aliimarika kisoka katika chuo cha vijana
wadogo cha Arsenal, na akiiwakilisha England katika mechi mbalimbali, tangu
zile za vijana wa miaka 16, hadi zile za wale wa miaka 21.
Alijiunga na Birmingham mwaka 2007, na kuhamia Bolton mwaka
uliofuata.
Muamba alicheza katika mechi za Ulaya mwaka 2011, za vijana
wa chini ya umri wa miaka 21, akiichezea England katika mashindano
yaliyofanyika nchini Denmark.
Wachezaji wenzake wa ligi ya Premier katika mitandao ya jamii
wamekuwa wakimtakia nafuu.
"Tunakuombea Fab. Tunatumaini yuko salama. Mawazo yetu
ni juu ya familia yako. Tunasubiri kwa matumaini habari zako kutoka kwa
wenzetu. Fab ni mtu anayejizatiti!" aliandika kiungo cha kati wa Bolton,
Stuart Holden.
"Tumuombee Fab. Kwa mapenzi ya Mwenyezi Mungu,
atapona." aliandika mshambulizi wa Tottenham, Jermain Defoe
0 comments:
Post a Comment