Abidal |
BILBAO, Hispania
BEKI wa Barcelona, Eric Abidal ameingia katika wakati mgumu
juu ya mustakabali wake kisoka baada ya leo kutangazwa kwamba anatakiwa kufanyiwa
operesheni ya ini, karibu mwaka mwaka mmoja tangu afanyiwe operesheni nyingine
kama hiyo.
Mfaransa huyo mwenye umri wa miaka 32, anayecheza beki ya
kushoto alifanyiwa upasuaji Machi 17, mwaka 2011, lakini alirejea kumalizia
msimu na amekuwa akiendelea vizuri tangu wakati huo.
Kwa heshima, Abidal aliteuliwa kunyanyua Kombe la nne la Ligi
ya Mabingwa, baada ya klabu hiyo kulitwaa kwenye Uwanja wa Wembley baada ya kuiwezesha
Barcelona kuifunga Manchester United mabao 3-1 kwenye fainali Mei mwaka jana.
Abidal amekuwa chaguo la kwanza katika kikosi cha mabingwa
hao wa Hispania na Ulaya kwa msimu wote huu na amekuwa akiwavutia wachezaji
wenzake, lakini walipigwa butwaa wakati kocha Pep Guardiola alipowapasulia
habari kabla ya mazoezi kwamba anatakiwa kufanyiwa upasuaji.
Habari hizo zinamaanisha kwamba Abidal hata nafasi yake ya kucheza
michuano ya Euro mwaka huu huko Poland na Ukraine kuanzia Juni 8 hadi Julai
katika kikosi cha Ufaransa iko shakani.
Abidal amekuwa mchezaji wa kikosi cha kwanza cha Barcelona tangu
ajiunge nayo akitokea Lyon mwaka 2007.
Ameisaidia klabu hiyo ya Catalan kutwaa mataji 13 kati ya 16 kwa
zaidi ya misimu mitatu iliyopita, yakiwemo mawili ya Ligi ya Mabingwa, Klabu
Bingwa ya Dunia na Super Cup za Ulaya, sambamba na mataji matatu mfululzo ya
Ligi ya Hispania na Copa del Rey.
Abidal aliyeumia nyonga akiichezea Ufaransa mechi ya kirafiki
wiki mbili zilizopita, alikuwa miongoni mwa wachezaji ambao Barcelona iliwategemea
sana katika vita ya kutetea ubingwa wa la Liga, ambao wanazidiwa pointi 10 na
vinara Madrid.
Barcelona imefuzu Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa na
itacheza na Athletic Bilbao katika fainali ya Copa del Rey Mei 25.
0 comments:
Post a Comment