Niyonzima kulia akimiliki mpira mbele ya Nassor Masoud 'Chollo' wa Simba |
KATI ya
wachezaji wapya wa kigeni walioingia kwenye Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara,
Haruna Hakizimana Fadhil Niyonzima ndiye ambaye alikuwa gumzo zaidi, kwa sababu
wengi hawakuamini kama klabu yake, APR ya Rwanda ingeweza kumuachia.
Lakini
historia imetimia, Niyonzima maarufu kama Fabregas kwa mashabiki wa Tanzania
amejiunga na Yanga ya Dar es Salaam na sasa anaonyesha cheche zake katika ligi
hiyo.
Baada ya
kucheza mechi kadhaa za ligi ya Tanzania, Niyonzima anasema kwamba amegundua
kwa sasa ligi ya nchi hii imeipiku ligi ya Rwanda.
“Ligi yetu
(Rwanda) ilikuwa juu sana, lakini mwaka jana imeshuka mno. Baada ya kucheza
hizi mechi mbili, nimegundua ligi ya Tanzania ni ngumu na ina msisimko mkubwa.
Niyonzima
anasema msisimko wa kishabiki, morali ya wachezaji na maandalizi ya ligi
yenyewe ni miongoni mwa vitu vinavyoifanya ligi ya Tanzania iwe bora kwa sasa,
hata yeye anaicheza huku akiifurahia.
“Yaani sasa
hivi hakuna mechi ndogo kwenye ligi ya Tanzania, kila mechi ni ngumu. Ni ligi
yenye ushindani haswa, ninafurahia kucheza,” anasema.
Kabla ya
kuja Yanga, Niyonzima amewahi kufanya majaribio mara mbili Ufaransa, mara moja
Sweden na mara moja Ujerumani na kote alifuzu, lakini hadi leo bado analikoga
vumbi la Afrika, kwa nini?
“Majaribio
ya Sweden, Ujerumani na Ufaransa kote APR walinifanyia roho mbaya, waliziwekea
vikwazo zile timu zikaamua kuachana na mimi. Nikapata timu ya kuninunua ya
Morocco, lakini APR ikaniwekea ngumu pia,” anasema.
Kutokana na
kuzibiwa riziki zake za kucheza Ulaya na timu hiyo ya jeshi la Rwanda,
Niyonzima anasema aliweka nadhiri akimaliza mkataba wake asiongeze tena.
“Nikiwa bado
APR wakati nimekwishazungumza na Yanga, nikapata nafasi ya kwenda Ubelgiji kwa majaribio, lakini nikashindwa
kwenda kwa sababu nilijua hata nikienda APR hawataniruhusu, nikaona nimalizane
nao kwanza, nije Yanga.
“Yanga
katika mkataba wao na mimi tumekubaliana nikipata timu tu nje, wananiruhusu niondoke,
hakuna tatizo. Na ninapenda niwaambie mashabiki wa Yanga najisikia furaha sana
kuchezea timu hii,” anasema Niyonzima, mume wa Wimezanaila, aliyezaa naye
watoto wawili wa kiume, Niyonzima na wa kike Halila.
Je,
Niyonzima angependa mwanae wa kiume arithi mikoba yake kwenye soka? “Hapana,
sitaki kabisa acheze mpira,” anasema.
Kwa nini? “Sitaki
tu acheze, mimi ninataka asome sana, ila ikitokea yeye mwenyewe akaamua
kucheza, sitamzuia, sitaki kwa sababu soka yetu hii tunacheza ina machungu
mengi sana ambayo sitaki mwanangu ayapate,” anasema.
Mchezaji
gani Tanzania anamvutia Niyonzima? “Mrisho Ngassa, nasikitika nimekuja Yanga
sikumkuta. Wakati nikiwa APR niliushawishi uongozi umsajili, ukashindwa, na
mimi ilikuwa nije Yanga tangu mwaka juzi kwa sababu yake, ila APR wakanibania,”
anasema.
Ulaya je,
Niyonzima anavutiwa na mchezaji gani? “Yes, Andres Iniesta,” anasema
akimaanisha anavutiwa na nyota huyo wa Hispania na Barcelona.
Anazungumziaje
mechi ijayo ya watani wa jadi katika soka ya Tanzania, ambayo kwake itakuwa ya
pili kucheza baada ya ile ya Ngao ya Jamii, Agosti 17, ambayo Yanga ilifungwa
mabao 2-0.
“Tuko vizuri
kwa sasa na tumejiandaa vema, tuna matumaini ya kushinda Jumamosi. Simba ni
timu nzuri, lakini na sisi tuko vizuri kwa sasa na watu watajionea
Jumamosi,”alisema.
Aidha,
Fabregas huyo wa Yanga ameweka nadhiri ya kupigana kufa na kupona kuhakikisha
anatikisa nyavu za Simba Jumamosi.
“Nataka
niwape raha Yanga, nataka niwafunge Simba. Nitaingia uwanjani kwa nia ya
kuwafunga,”anasema.
Naam, huyo
ndiye kiungo mpya wa Yanga, Haruna Hakizimana Fadhil Niyonzima, aliyepania
kuwatungua Simba kwenye ligi, ili kulipa kisasi cha kipigo cha Ngao ya Jamii.
Je, ataweza
kutimiza nadhiri yake hiyo? Bila shaka hilo ni jambo la kusubiri na kuona.
WASIFU WAKE:
JINA: Haruna
Hakizimana Fadhil Niyonzima
KUZALIWA: Aprili
7, 1991
ALIPOZALIWA:
Kigali, Rwanda
KLABU YAKE:
Yanga SC
KLABU ZA
AWALI:
Mwaka Klabu
2009-2011 APR
FC
2006-2008 Rayon Sport
(Tangu 2006, ameichezea Rwanda mechi 35 ameifungia mabao 12)
0 comments:
Post a Comment